Kuna wakati, nilipokuwa nimemaliza masomo yangu ya kidato cha 6, ikiwa ni pamoja na masomo ya biblia, nilialikwa kwenye mkutano wa wasabato. Nilienda huko nikiwa sijui kuwa ningepewa nafasi ya kuongea.
Cha ajabu, nikawekwa kama mtu wa kujibu maswali waliyokuwa wakiyaelekeza kwa Kanisa Katoliki. Nilijibu, kwa kadiri Roho alivyoniongoza.
Wote wakawa kimya kabisa. Nilishangaa mwishowe kufuatwa na viongozi wao kuwa eti wananiomba nijiunge nao na kisha niwe mchungaji wa Kanisa lao. Nilishangaa sana, nikawauliza kuwa tangu mwanzo wamelituhumu Kanisa Katoliki kuwa limepotoka, inakuwaje tena mimi Mkatoliki naweza kuwa kiongozi wao? Hawakuwa na jibu.
Nilivyomaliza masomo yangu ya shahada ya pili, nilipofika Dar, nikaalikwa na jamaa mmoja, aliwahi kuwa mtu mkubwa kwenye ngazi ya kitaifa kwenye Serikali. Yeye ni muislam. Nikaitikia mwaliko, nikaenda. Kufika huko nikashangaa walikuwa wamejaa wasomi wa dini ya Kiislam. Pekee yangu nilitengewe kiti, huku wao wote wakiwa wameketi kwenye majamvi. Nikaanza kuulizwa mambo ya Ukristo. Sikuwa nimejipanga kwa hilo. Lakini kwa utulivu niliwajibu kadiri nilivyoweza, hata wakaishiwa swali lolote.
Nilitafakari sana kwa nini niliitwa mimi, lakini baadaye nilikuja kutambua kuwa kuna ndugu zangu, nao walikuwa wasomi wazuri kwenye elimu ya Dunia, lakini hawakuwa vizuri sana kwenye mafundisho ya kiimani. Na kuna watu walitaka kuwabadilisha wale ndugu zangu kwenda uislam, na ikaelezwa kwamba kikwazo ilikuwa mimi. Hivyo wakinibadilisha mimi, basi wale wengine watanifuata.
Nashukuru mpaka leo wote tupo katika imani yetu.
Na neno la mwisho nililowaambia wale wasomi wa dini ya Kiislam ni kwamba sisi katika Ukristo tunaamini sana katika neema. Na neema hiyo inaweza kumwangukia yeyote, na ukashangaa aliyekuwa imamu au hata mpagani, siku nyingine anaweza kuja kuwa mkristo, tena kukuzidi hata wewe uliyedhania unaujua zaidi ukristo, akawa mwalimu wako.
Kwa hiyo usighadhabike Kanisa likinenewa vibaya. Kristo pamoja na ukuu wote, na mamlaka yote, alidhalilishwa, alitukanwa, alipigwa, alivuliwa nguo, alitemewa mate, hakuhangaika na waliomtendea hayo. Alipofufuka neno lake la kwanza lilikuwa Shalom, yaani muwe na amani, nimekamilisha, msiwe na mashaka. Mkristo unatakiwa kuyaiga maisha ya Kristo. Hatushindani katika kumjua au kumwabudu Mungu. Hata anayetusi, ujue Mungu ameruhusu, asipotaka, hawezi hata kuupanua mdomo wake.