Mkuu Maalim, historia ya TANU ilianzia TANU ilipozaliwa mwaka 1954 na mwenye kadi nambari moja ndie mwasisi Mkuu.
Naomba tuzilazimishe kuichomekea historia ya TAA. Utanisamehe sana nikikueleza hata hao kina Skyes hapa Tanganyika sio kwao kwa sababu nao ni watu wa kuja tuu kama alivyokuja Zongendamba kutoka kule alikotokea.
Ukiwataja kwenye historia ya TAA ni sawa. TAA ni TAA, TANU ni TANU na CCM ni CCM na kila kimoja kina historia yake!.
Kama ukiulizwa TANU ilianzishwa lini na muasisi ni nani, ukijibu 1954 na mwasisi ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, utapata 100%. Ukiulizwa TANU ilianzishwa lini wewe ukaanza kuzunguka kuwa ilianzia TAA mwaka 1929, na Ukiwataja kina Skkes, utapata buyu!.
Thamani ya historia ya Tanzania ni kwa Watanzania, kama Watanzania kupitia Kivukoni wanamtambua Nyerere kama muasisi na mwanzilishi wa TANU, then Tanzania ni Nyerere, yafaa nini hiyo historia ya DAB?!. What is it for?!.
Historia ni mwanzo wa kitu husika, not a peny more, not a peny less!.
Paskali
Paskali,
Mimi sina nguvu ya kulazimisha chochote kwako au kwa mtu yeyote awae yule.
Nilichonacho mimi ni mantiki na ukweli katika historia ya Tanganyika ambayo
nimetafiti na kuandika kitabu, na ''paper,'' kadhaa ambazo watu wamesoma
bila ya kulazimishwa.
Wala mimi sijakataa kuwa
Mwalimu Nyerere ni muasisi wa TANU.
Ila ninachosema mimi ni kuwa ikiwa utaifunga akili yako ibakie hapo bila ya
kutaka kuisoma historia nzima atakaepunjika ni wewe.
Ukweli ni kuwa
Nyerere haiwezekani mgeni mno afike Dar es Salaam, awe na
ofisi, awe na wanachama na aanzishe TANU huu ni sawa na muujiza.
Haiingii akilini kuwa wewe uione kadi ya TANU ya
Nyerere no. 1 lakini usitake
kujua nani ana kadi no. 2, 3, 4 na kuendelea hasa kwa mtu mwenye ''A'' ya
historia.
Hili haliwezekani lakini ukipenda kuamini hivyo hakuna wa kukulazimisha vinginevyo
hasa kwa kuwa una ''A'' ya historia ya Kivukoni.
Hii maana yake ni kuwa wewe ni mjuzi.
Kuna kitu kipya umekileta kuwa African Association ni ya kina
Sykes na wao hapa
si kwao kwa hiyo ni sawa kwa historia hiyo kufutwa.
Mantiki ya hoja yako inakuwa kwa kuwa hawa ni Wazulu ''watu wa kuja,'' na
wameanzisha African Association basi historia hii haitakiwi.
Hoja hii itatambaa hivyo hivyo hadi kufikia wao kuunda TANU 1954.
Katika historia ya uhuru wa Tanganyika na mwamko wa Waafrika wa Tanganyika
kupambana na ukoloni utakutana na Waafrika wengi ambao Tanganyika si kwao.
Katika hiyo African Association utakutana na
Kleist Mzulu aliyezaliwa Pangani na akina
Plantan waliokuja kutoka Mozambique lakini ni Wazulu pia.
Utakutana na
Ibrahim Hamisi Mnubi wa wazee wake wametokea Dafur, Sudan.
Utakutana na
Erica Fiah Mganda kutoka Uganda, utakutana na
Mzee bin Sudi
Mmanyema wazee wake wametokea Belgian Congo.
Hawa nimekutajia wachache tu katika historia ya kupambana na wakoloni katika
miaka ya 1920 hadi kufikia mwisho wa Vita Vya Pili 1945.
Katika hiyo TANU halikadhalika wako pia ''wakuja,'' wengi tu.
Tuanze na
Patwa Muhindi
, Saadan Abdul Kandoro, Mmanyema,
Sheikh
Mohamed Ramiya Mmanyema,
Dome Okochi Budohi Mluya kutoka Kenya,
Patrick Aoko Mjaluo Mkenya,
Denis
Phombeah Mnyasa kutoka Nyasaland,
Iddi Faiz Mafungo Mmanyema kwa
kukutajia majina machache.
Kulikuwa na
Earle Seaton kutoka Bermuda, haonekani lakini yuko aliyetiwa katika
siasa za Tanganyika na
Abdul Sykes kizazi cha pili Mzulu kuzaliwa Tanganyika na
palikuwa na
Mufti Sheikh Hassan bin Amir kutoka Zanzibar.
Hawa wote wana historia zao ukizisoma mwili lazima ukusisimke.
Namaliza na babu yangu
Salum Abdallah, Mmanyema aliyezaliwa Shirati Musoma
aliyekuwa mmoja wa wa wapigania uhuru wa Tanganyika kuanzia 1947 na 1955
akawa Mwenyekiti muasisi wa Tanganyika Railway African Union (TRAU).
Najua haya huyajui labda kwa kuwa waandishi wa historia kutoka Kivukoni kama
wewe hawakuwa wanayajua.
Inawezekama kwa kuwa una ''A'' ya historia ya Kivukoni ukaona Dictionary of
African Biography iliyochapwa na Oxford Univeristy Press, 2011 si chochote lakini
hii ni katika rejea muhimu sana katika historia ya Afrika.