Kwanza tunawahesabu waliokufa kwa tabu,bila hata matibabu wengi hawana hesabu waliokufa kwa tabu dunianiiii,
Kambona aliagiza Chipaka na kamalizaa,pindueni mkiweza nitawapeni mafedhaa nikirudi safarini uingerezaaa
Nakumbuka hapo tu....sijui ni nani alikatunga haka kasongi
Ndugu zangu nani ningependa kuchangia kidogo kuhusu Oscar Kambona.
Leo nimefanya kipindi kizima cha TV kuhusu maisha ya Oscar Kambona toka alipojiunga na TANU pale TANU HQ, New Street mwaka wa 1954 hadi alipokosana na Mwalimu Nyerere mwaka wa 1967 na kuondoka kwake kwenda uhamishoni Uingereza.
Nimeeleza yaliyotokea katika maasi ya Tanganyika Rifles (TR) tarehe 20 Janaury 1964 na jinsi Kambona akiwa Waziri wa Ulinzi alivyokabiliana na uasi ule na mwishowe kuweza kuwatuliza askari na wakarudi Colito Barracks.
Msaada ukatafutwa kwa Waingereza na Royal Marines ambao manowari yao haikuwa mbali na pwani ya Tanganyika wakaja na kuwanyang'anya silaha waasi.
Kwa siku tatu zile za maasi kiongozi aliyeonekana na kusikika katika radio akiwatuliza na kuwafariji wananchi alikuwa Oscar Kambona.
Mawaziri wote walijificha.
Baada ya waasi kunyang'anywa silaha ndipo Mwalimu Nyerere akajitokeza hadharani na kuzungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa kwa kipindi chote cha maasi alikuwa Dar es Salaam.
Nyota ya Kambona iling'ara kwa yale aliyofanya katika kukabiliana na maasi lakini haiba ya Mwalimu Nyerere ilikuwa imepungua kwani kulikuwa na minong'ono mitaani kuwa Kambona angelitaka angeliweza kuchukua serikali.
Katika hili wanahistoria kila mmoja katika miaka iliyopita amekuwa na lake la kusema.
Baada ya maasi Kambona akawa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje nafasi aliyoishika hadi mwaka wa 1967 alipokinzana na Mwalimu Nyerere kuhusu Azimio la Arusha.
Katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwaka huo Kambona akateuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Inasemekana Kambona wala hakupata kuingia katika ofisi hii yake mpya na akajiuzulu kutoka serikalini.
Turudi nyuma kidogo.
Mwaka wa 1963 Mwalimu Nyerere alilivunja Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa na wajumbe 126 wote Waislam.
Baraza hili halihitaji maelezo mengi kwani ndilo lililomtia nguvu kubwa Nyerere kukubalika Dar es Salaam.
Sababu zilizotolewa za kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU ni kuwa lilikuwa linachanganya dini na siasa.
Kuanzia hapo Mwalimu Nyerere akawa mbali na wazee hawa na hawa wazee wakajiweka mbali na TANU hakuwarudi tena pale Lumumba ambako wengi walifanya kama baraza yao ya kukutana nyakati za jioni kwa mazungumzo.
Wakati Nyerere kajikata na wazee hawa Kambona alibakia na uhusiano mzuri na wazee wengi wa TANU mmojawapo akiwa Mshume Kiyate.
Mshume Kiyate kwa upande wake hakuweka kinyongo dhidi ya Nyerere kwa kulivunja baraza lao.
Ushahidi wa roho yake nyeupe ni pale baada ya maasi Mshume Kiyate alikwenda kumpa pole Nyerere na kumvisha kitambi kama ishara ya mapenzi yake kwake.
Huenda si wengi wanalijua hili.
Kambona alikuwa mtu karimu sana na wazee wengi walinufaika na mkono wake wa kutoa.
Kambona hakuchusha machoni pa wazee hawa na pengine kwa wananchi wengi wa kawaida. .
Swali la kujiuliza ni kuwa, je, Mwalimu alikuwa anafahamu kuwa alikuwa anaanza kupoteza mapenzi kutoka kwa baadhi ya watu waliompenda sana kuanzia mara ya kwanza alipoka Dar es Salaam mwaka wa 1952 na ugomvi wake na Kambona kule kuvunja Baraza la Wazee kulikuwa kunajenga taswira mpya katika historia ya chama cha TANU?
Nakuwekea hapo chini kipande kifupi cha video katika yale niliyozungumza katika kipindi hiki cha Oscar Kambona:
View: https://youtu.be/VXjj3-_Yyw8