Ukweli ni upi kuhusu Oscar Kambona?

Ukweli ni upi kuhusu Oscar Kambona?

Hebu Tujuze Maggid,
inavyoelekea, mtu yeyote mwenye kujiamini ilikuwa akimchallenge Mwalimu kidogo tu, anakupoteza, yeye alitaka ma yes yes tu wamzunguuke!!
 
Nyerere alimtumia Kawawa kumshugulikia Kambona. Kambona alikua anagain popularity zaidi ya Rashidi na hata Nyerere na hakua yes man. Hadithi inasema kutokana na umaarufu wa Oscar aliweza kuzima Mutiny kwa kushirikiana wanamaji wa uingereza wakati Nyerere akiwa kajificha Kingamboni. This is to say Nyerere alishapinduliwa bila Kambona kuweka mambo sawa. Unfortunately Julius felt undermined by the incidence na huo ukawamwanzo wa tofauti zao.
 
Ndugu zangu,


Yumkini kwa baadhi, kuwa kwangu mimi kuandika upande wa pili wa simulizi juu ya ‘ mapacha’ watatu; Kambarage, Kambona na Kawawa, yaweza kutafsiriwa ni kuchagua kuwa ‘ Wakili wa Shetani’; Oscar Kambona.
Lakini , siku zote, wanadamu tunapaswa kufanya jitihada ya kuitafuta kweli. Tufanye hivyo ili tuyapate maarifa mapya.
Nimesimuliwa, nimesoma na sasa nimejiridhisha, kuwa Oscar Kambona alikuwa na atabaki kuwa Mtanzania mzalendo wa nchi. Tunavyoendelea na simulizi hii natumaini msomaji utaelewa maana ya mimi kusema hivyo.


Na ni historia inayompa hukumu hiyo ya haki. Nimekumbusha mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Na kwa mwanadamu, ili uweze kuyaelewa yanayotokea leo na kubashiri yatakayotokea kesho, ni vema na ni busara ukajitahidi kuyajua yaliyotokea jana.


Tunasoma, kuwa Mandela alikaa gerezani kwa miaka 26, lakini, katika nchi yetu hii, tunaweza kabisa kuandika, kuwa Oscar Kambona alikaa gerezani miaka 25. Mandela aliwekwa kisiwani kule ‘Robin Island’ na Kambona nae aliwekwa ‘Kisiwani London’. Tukumbuke, Uingereza ni kisiwa kilichozungukwa na bahari.


Hakika, Kambarage, Kambona na Kawawa ni kisa cha ‘ mapacha’ watatu ambacho Watanzania wengi wa kizazi cha sasa hawajapata kukisikia. Kama taifa, ya Kambarage, Kambona na Kawawa ni sehemu ya historia yetu . Maana, sio tu historia ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na hata kuanzishwa kwa TANU, bali historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila kutajwa kwa jina hili; Oscar Kambona.


Kama nilivyobainisha awali, kuwa utotoni nimesimuliwa habari za ugomvi wa mapacha hao matatu, hususan, Julius na Oscar. Nimewasikia kaka zetu pia wakimwimba Oscar Kambona kwenye nyimbo za mchakamchaka shuleni. Nikajengewa kiu ya kutaka kujua zaidi ya Oscar Kambona na wenzake.


Siwezi hapa nikasema nimefanya utafiti wa kina, bali, nimejitahidi kujua. Ndio, mathalan, nimesoma na nimejaribu kutafsiri picha nyingi za mapacha hao watatu katika miaka ya mwanzoni ya uhuru. Picha ya Kambarage, Kambona na Kawawa hapo juu ni mfano wa picha inayoonyesha dalili ya kile ambacho nimekisoma juu ya urafiki ulioanza kuwa wa mashaka baina ya Julius, Oscar na Rashid.


Katika wakati ule wa harakati za kudai uhuru na kuijenga TANU, watatu hawa; Julius, Oscar na Rashid ndio walioonekana zaidi mbele ingawa ni ukweli , kuwa kazi ya kuianzisha TANU na kuijenga ilifanywa pia na watu ambao majina yao ni nadra kusikika.


Watatu hawa walikuwa na mvuto na wenye haiba, na kama wanasiasa walihitaji mvuto kwa wananchi. Na Oscar ndiye aliyeonekana kuwa na mvuto zaidi ya wenzake. Hili nalo laweza kuwa moja ya nadharia ya mfarakano wa Oscar, Julius na Rashid.


Mama yangu mzazi wakati huo alifanya kazi Government Press. Ni Idara ya Kupiga Chapa ya Serikali. Nakumbuka alipokuwa akisumulia jinsi Oscar alivyokuwa akiwavutia wasichana wa wakati huo. Oscar was a handsome guy! Na alikuwa na staili yake ya nywele, ikaitwa ‘ Kambona Style!’. Na si hata kwenye dhifa za kitaifa pale Ikulu ya Magogoni, Oscar hakupata tabu kupata wanawake wa kucheza nao rhumba.


Na isije ikasemwa, kuwa Julius na Rashid walikuwa na ’ wivu’ kwa pacha mwenzao, Oscar.
Si kaka zetu waliimba kwenye mchakamchaka;
” Kambona, ah, ah!
Kambona, ameolewa,
Wapi?
Huko Ulaya, ’wivu’ wamkereketa!”


Julius, Oscar na Rashid; Urafiki wao ulianzaje?
Julius alikutana na Oscar Tabora mwishoni mwa miaka ya 40. Inasemwa, kuwa Julius alimtangulia kiumri Oscar kwa kupishana miaka mitatu tu. Kule Tabora Julius alikutana pia na Rashid, naye alimzidi kiumri kwa miaka mitatu hivi. Hivyo basi, twaweza kusema, kuwa urafiki wa Julius, Oscar na Rashid ulianzia Tabora, na harakati zao za pamoja za mapambano ya kisiasa zilianzia huko huko Tabora.


Julius alikuwa Mkatoliki na hodari sana shuleni, akafika mpaka Uingereza kimasomo. Aliporudi akafanya kazi ya Ualimu pale Pugu. Alipoambiwa achague kati ya Ualimu na siasa, Julius akachagua siasa. Oscar naye alikuwa Anglican na hodari sana shuleni. Naye akafika mpaka Uingereza kusomea sheria. Hakumaliza masomo yake, Nyerere alimshawishi akatishe masomo yake, arudi nyumbani kuimarisha TANU kwenye Uchaguzi uliokuwa mbele yao. Rashid, Mwislamu, alisoma mpaka Tabora, hakufika Uingereza, lakini alikuwa Trade unionist mahiri, na katika TANU alikuwa ni mpiganaji wa kuaminika. Rashid alikuwa maarufu mjini. Alipata hata kucheza filamu maarufu ya ’ Muhogo Mchungu’.
Watatu hawa walikuwa marafiki, hilo halina shaka. Na baada ya uhuru wa Tanganyika, Julius na Oscar walijenga nyumba zao pale kijijini Msasani kwenye pwani ya bahari. Naam. Walikuwa karibu sana kikazi na walichagua kuwa majirani.


Inasimuliwa, kuwa nyakati za jioni, Oscar na Julius walipenda sana kutembea pamoja ufukweni pale Msasani wakijadiliana mambo mbali mbali. Bila shaka, wake zao, Maria na Flora, walitembeleana na hata kuombana chumvi.


Na ikafika wakati, Oscar na Julius hawakuonekana tena wakitembea pamoja ufukweni. Na pengine Maria na Flora hawakutembeleana na kuombana chumvi. Ikafika wakati pia, Oscar na familia yake wakafungasha mizigo yao na kuondoka nchini kupitia Namanga. Nyumba yao ikaja kupata mpangaji mpya; Milton Obote, rafiki mwingine wa Julius.


Na mjini Dar es Salaam ukatawala uvumi zaidi kuliko ukweli wa kilichotokea. Ikasemwa, kuwa Kambona ametoroka akiwa na sanduku limejaa pesa. Na pesa yetu wakati ule ilikuwa na thamani sana. Fikiri sasa kama sanduku la Kambona lilijaa manoti!


Na utotoni pale Ilala, nilipata kusikia uvumi, kuwa huko Ulaya, Kambona amekuwa tajiri mkubwa. Wengine wakasema alishinda Bahati Nasibu. Wengine wakasema ni fedha alizotoroka nazo. Na kuna wakati ukaenea uvumi, kuwa kuna meli bandarini imezuiliwa kushusha shehena ya vitanda. Ni vitanda ambavyo Kambona alivituma Tanzania ili vitumike mahospitalini. Kwa vile ukweli hasa kuhusu ugomvi wa Kambarage na Kambona haukupata kusemwa, basi, uvumi ukaendelea kusambazwa.


Mpaka hii leo, bado kuna Watanzania wengi hawajui ukweli wa kilichotokea. Na maswali bado yanaulizwa; Ni kitu gani kiliwatokea ’ mapacha’ hawa watatu? Angalia picha hiyo ya juu, Oscar anaonekana kuanza kuwa mbali na Julius wakati Rashid yu karibu sana na Julius. Na kwanini Oscar hakushika fimbo? Nitaanza na kwenye safari yao ya China mwaka 1965. Naam. Simulizi hii na ituweke katika kundi la wale wanaojitahidi kujua. Itaendelea.


Maggid,
Sweden,
Jumapili, Junu 19, 2011
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
 
Asante mkuu ni vema ukatuambia itaendelea lini tena
 
Hadithi zako ni kama za tamthilia za Shigongo ni za kufikirika zaidi kuliko ukweli wenyewe japo zinavutia.
 
Na Maggid Mjengwa,

”KAMBONA, ah, ah! Kambona, ameolewa, Wapi? Huko Ulaya! Wivu, wamkereketa!”


Yumkini kwa baadhi kuwa, kwangu mimi kuandika upande wa pili wa simulizi juu ya marafiki watatu; Kambarage, Kambona na Kawawa, yaweza kutafsiriwa ni kuchagua kuwa ‘Wakili wa Shetani’: Oscar Kambona.

Lakini , siku zote, wanadamu tunapaswa kufanya jitihada ya kuitafuta kweli. Tufanye hivyo ili tuyapate maarifa mapya. Wimbo huo hapo juu ni wa mchakamchaka.
Uliimbwa na kaka na dada zetu mashuleni. Kuna wengi tuliousikia. Tukaamini, lakini kuna tuliojengewa kiu ya kutaka kujua ukweli wa jambo zima.

Naam. Mwaka huu tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wetu. Na kwa mwanadamu, ili uweze kuyaelewa yanayotokea leo, na uweze kubashiri yatakayotokea kesho, basi, ni vema na ni busara ukajitahidi kuyajua yaliyotokea jana.

Kizazi cha sasa cha Watanzania kitapata maarifa mapya na hata kusaidiwa kuyaelewa yanayotokea leo kwa kukumbushwa na kusaidiwa kuyajua yaliyotokea jana. Maana; kuna waliojenga msingi wa nchi hii.
Mapungufu mengine tunayayaona leo yanatokana na makosa ya jana yaliyofanywa na waliojenga msingi wa nchi hii. Ni makosa ya kibinadamu.Ni mwanadamu gani asiyekosea?

Na hakika, kisa cha marafiki watatu; Kambarage, Kambona na Kawawa kinatoa somo muhimu kwa Watanzania wengi wa kizazi cha sasa.

Tutafanya makosa kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu bila, japo kwa uchache, kujadili kilichowatokea marafiki hawa watatu na athari zake kwa Tanzania yetu ya leo.

Utabaki kuwa ni ukweli kuwa, kama Taifa, ya Kambarage, Kambona na Kawawa ni sehemu ya historia yetu . Maana; sio tu historia ya harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na hata kuanzishwa kwa TANU, bali historia ya nchi yetu haiwezi kukamilika bila, mathalan, kutajwa kwa jina hili: Oscar Kambona.

Lakini, kwa miaka hamsini sasa, ukweli juu ya nini kilichotokea mpaka Oscar Kambona akaikimbia nchi yake aliyozaliwa haujawekwa hadharani umma ukaelewa. Kwa Watanzania wengi, Oscar Kambona na kukimbia kwake nchi inabaki kuwa simulizi ya upande mmoja.
Na kwa vile shilingi ina pande mbili, hata ukichukia pande moja ya shilingi, si busara ukakaa na kuubondabonda upande unaouchukia. Bado ni shilingi yako.

Utotoni nimesikia simulizi za Oscar Kambona. Shuleni hatukusoma habari za Oscar Kambona na mchango wake katika kuanzishwa kwa TANU na ujenzi wa chama hicho na hata ushiriki wake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Tuliosikia simulizi za Oscar Kambona tuliaminishwa kuwa, Kambona alikuwa msaliti kwa nchi yake. Kambona alikuwa bepari na alichukia Ujamaa. Kambona alikuwa mhaini na hata huko Ulaya alikokimbilia, alipanga njama za kumpindua rafiki yake wa zamani, Julius Nyerere. Naam, kulikukwa na simulizi nyingi mbaya juu ya Oscar Kambona.
Na katika dunia hii kuna wanaodhani wanajua, na kuna wale ambao wanajitahidi kujua. Nimechagua kuwa katika kundi hilo la pili; wanaojitahidi kujua.

Kazi hii ya kuutafuta ukweli hasa wa nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, ni moja ya jitihada tunazopaswa kuzifanya wakati tukiwa hai; kujitahidi kujua.

Nimesikia simulizi za utotoni juu ya Oscar Kambona. Katika utu uzima wangu huu nimejitahidi kuyatafuta maandiko yenye kumhusu Kambona na wenzake wa enzi za Tanganyika.

Nimejiridhisha kuwa Oscar Kambona alikuwa Mtanzania mzalendo wa nchi hii. Alitofautiana kimisimamo na rafiki yake Julius Nyerere juu ya namna ya kuendesha mambo katika Tanganyika huru, akaamua kuondoka yeye na familia yake.

Kilichofuata, ndani ya propaganda na uvumi ule dhidi ya Kambona kwa jinsi alivyoondoka, kulikuwa na ’ kimya kizito’. Ni kimya kilichodumu kwa nusu karne sasa. Ni kimya kwa vile hakukuwa na nafasi ya kusikia kutoka kwa Oscar kambona mwenyewe, jibu la swali hili muhimu; Kwanini Kambona aliondoka?

Na kulitafuta jibu la swali hilo kutatusaidia kuyaona makosa yaliyofanyika nyuma ili kuepuka kuyarudia tena. Maana, kimya kile cha miaka hamsini kwa namna moja au nyingine, kimesababisha kuyarudia baadhi ya makosa yaliyofanywa na waliojenga msingi wa taifa hili.

Tunajua leo, kuwa Kambona alitofautiana na Nyerere juu ya utekelezaji wa Azimio la Arusha. Alikuwa na mtazamo tofauti; hivyo basi, hakukuwa na dhambi ya kufikiri tofauti.

Kambona alihoji mantiki ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja bila upinzani wa kisiasa. Hakukuwa na dhambi ya kufikiri hivyo.

Tunaona sasa, msingi huo huo uliojengwa wa kuamini kuwa upinzani wa kisiasa ni uadui, ni dhambi, ndio kwa kiasi kikubwa umelifikisha taifa letu hapa lilipo.

Kwa nusu karne sasa, chini ya chama kimoja tawala, imejengeka misingi ya viongozi kulindana. Na fursa ilipopatikana, baadhi ya viongozi wetu wamekuwa matajiri wakubwa kwa njia haramu.

Tujiulize; Kambona alifanya dhambi gani kubwa kiasi cha kupata adhabu ile kubwa ya kukaa uhamishoni kwa miaka 25? Mandela alimzidi Kambona kwa mwaka mmoja katika ‘kutupwa gerezani’.

Na katika hili la Kambona na Nyerere kuna mengi ya kujiuliza: Hivi inawezekanaje marafiki wawili walioshibana wakafikia kufarakana kwa kiasi tulichokishuhudia? Ikukumbukwe, Nyerere na Kambona walikuwa marafiki kiasi cha Kambona kumfanya Nyerere kuwa ‘Mpambe wa Bwana Harusi’ kwenye harusi ya Kambona iliyofanyika London, Uingereza.

Labda utajiuliza; urafiki wao ulianzaje? Nyerere alikutana na Oscar Kambona wakati Kambona alipokuwa shuleni Tabora mwishoni mwa miaka ya 40. Inasemwa kuwa Nyerere alimtangulia kiumri Oscar kwa kupishana miaka mitatu tu.
Kule Tabora Nyerere alikutana pia na Rashid Kawawa; naye alimzidi kiumri kwa miaka mitatu hivi. Hivyo basi, twaweza kusema kuwa urafiki wa Julius, Oscar na Rashid ulianzia Tabora, na harakati zao za pamoja za mapambano ya kisiasa zilianzia huko huko Tabora.
Julius Nyerere alikuwa Mkatoliki na hodari sana shuleni, akafika mpaka Uingereza kimasomo. Aliporudi akafanya kazi ya ualimu pale Pugu.

Alipoambiwa achague kati ya ualimu na siasa, Julius akachagua siasa.

Oscar naye alikuwa mwumini wa kanisa la Anglican na hodari sana shuleni. Naye akafika mpaka Uingereza kusomea sheria. Hakumaliza masomo yake, Nyerere alimshawishi akatishe masomo yake, arudi nyumbani kuimarisha TANU kwenye uchaguzi uliokuwa mbele yao.
Rashid Kawawa alikuwa Mwislamu. Alisoma mpaka Tabora, hakufika Uingereza, lakini akawa kiongozi mahiri wa vyama vya wafanyakazi . Katika TANU alikuwa ni mpiganaji wa kuaminika. Rashid alikuwa maarufu mjini. Alipata hata kucheza filamu maarufu ya ’ Mhogo Mchungu’.

Watatu hawa walikuwa marafiki, hilo halina shaka. Na baada ya Uhuru wa Tanganyika, Julius na Oscar walijenga nyumba zao pale kijijini Msasani kwenye pwani ya bahari. Naam. Walikuwa karibu sana kikazi na walichagua kuishi pamoja kama majirani.

Inasimuliwa kuwa nyakati za jioni, Oscar na Julius walipenda sana kutembea pamoja ufukweni pale Msasani wakijadiliana mambo mbalimbali. Bila shaka wake zao - Maria na Flora walitembeleana na hata ‘kuombana chumvi’.
Lakini ilifika wakati Oscar na Julius hawakuonekana tena wakitembea pamoja ufukweni. Na pengine Maria na Flora hawakutembeleana na kuombana chumvi. Ikafika wakati pia Oscar na familia yake wakafungasha mizigo yao na kuondoka nchini kupitia Namanga. Nyumba yao ikaja kupata mpangaji mpya; Milton Obote, rafiki mwingine wa Julius Nyerere.

Na mjini Dar es Salaam ukatawala uvumi zaidi kuliko ukweli wa kilichotokea. Ikasemwa kuwa Kambona ametoroka akiwa na sanduku limejaa pesa. Na pesa yetu wakati ule ilikuwa na thamani sana. Fikiri sasa kama sanduku la Kambona lilijaa manoti!

Na utotoni pale Ilala, nilipata kusikia uvumi kuwa huko Ulaya, Kambona amekuwa tajiri mkubwa. Wengine wakasema alishinda bahati nasibu. Wengine wakasema ni fedha alizotoroka nazo.

Na kuna wakati ukaenea uvumi kuwa kuna meli bandarini imezuiliwa kushusha shehena ya vitanda. Ni vitanda ambavyo Kambona alivituma Tanzania ili vitumike mahospitalini.

Kwa vile ukweli hasa kuhusu ugomvi wa Kambarage na Kambona haukupata kusemwa, basi, uvumi ukaendelea kusambazwa. Hivyo basi ’kimya kikuu’.
Makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, na nini cha kujifunza.
Itaendelea toleo lijalo.
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
 
Kwa vile ukweli hasa kuhusu ugomvi wa Kambarage na Kambona haukupata kusemwa, basi, uvumi ukaendelea kusambazwa. Hivyo basi 'kimya kikuu'.
Makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea miaka hamsini iliyopita, na nini cha kujifunza.
Itaendelea toleo lijalo.

Kwahiyo mkuu haya utakuwa umeyapata wapi? au ni mwendelezo tu wa hapo kwenye green?
 
Oscar was very right when it comes to National Interests, Mwalimu decided to turnish the Image of Kambona deliberately... but Kambona had national Interests in a different way...
 
Na Maggid Mjengwa,

Julius Nyerere alikuwa Mkatoliki na hodari sana shuleni, akafika mpaka Uingereza kimasomo. Aliporudi akafanya kazi ya ualimu pale Pugu.

Oscar naye alikuwa mwumini wa kanisa la Anglican na hodari sana shuleni.

Rashid Kawawa alikuwa Mwislamu.

Hili kabati ya udini utalifunga lini Maggid....

Hujui lolote kuhusu Kambona kwa nini ukae upande mmoja badala ya kubalance makala yako, Halafu kuna kitu cheap sana unakifanya hapa, kukusanya maoni ya watu humu jamvini ili umalizie makala yako na kuonekana muandika historia.

Namwelewa vizuri sana Mzee Kambona RIP lakini sitakujuza chochote.
 
Hili kabati ya udini utalifunga lini Maggid....

Hujui lolote kuhusu Kambona kwa nini ukae upande mmoja badala ya kubalance makala yako, Halafu kuna kitu cheap sana unakifanya hapa, kukusanya maoni ya watu humu jamvini ili umalizie makala yako na kuonekana muandika historia.

Namwelewa vizuri sana Mzee Kambona RIP lakini sitakujuza chochote.

Ndugu yangu Bado Niponipo,
Asante kwa maoni, nami nikuambie tu, kuwa , kuna wanaodhani wanajua, na kuna wanaojitahidi kujua, mie niko kwenye kundi hilo la pili.
Nilichokiandika ni mchango wangu wa kidogo nilichojitahidi kukijua.
 
-Ziara mbili za ughaibuni zilizovunja urafiki wa Nyerere na Kambona

Na Maggid Mjengwa,

KUNA wakati nilimsikia Ahmad Rashid akitoa hoja bungeni. Wakati huo mbunge huyo wa CUF alikuwa kiongozi wa upinzani bungeni. Ahmad Rashid aliomba kambi ya upinzani bungeni ibadilishwe jina na badala yake iitwe kambi ya ushindani bungeni. Ni kwa vile neno ‘upinzani’ linatafsiriwa vibaya na wananchi. Spika Samwel Sitta alisimama na kutamka; “ Mtaendelea kuitwa hivyo hivyo kambi ya upinzani, kwa vile nyinyi ni watu wa kupingapinga tu!”


Na maneno haya ya Samwel Sitta yanatokana na historia yetu. Maana, haya ni makosa ya kihistoria yaliyofanywa na waliojenga msingi wa taifa letu. Na ndio tunayoyaona hata katika mfarakano wa miaka hamsini iliyopita kati ya Julius Nyerere na Oscar Kambona.

Na mara ile, mwaka 1965, TANU ilipoaachana na mfumo wa vyama vingi na kuasisi mfumo wa Chama kimoja Kambona alipata kutamka; ” Kwanini tupige marufuku ya vyama vingine vya siasa wakati tunajua wananchi walio wengi wanaipigia kura TANU?” Kambona akaongeza kusema; ” Bila shaka, umaarufu wa TANU utabaki kwa muda mrefu, lakini, je, pale umaarufu wa TANU utakapopungua, ina maana tuwe madikteta?” Alihoji Kambona.

Nimepata kukumbushia mara kadhaa, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Na wanadamu hatupaswi kuwa vipofu wa historia yetu wenyewe. Kuifumbia macho historia yako ni kujiandalia njia ya kutumbukia korongoni, kwa kujitakia. Tunapoadhimisha miaka hamsini ya uhuru wa Tanganyika tuna lazima ya kuipitia na kuitafakari historia yetu. Kwa macho makavu na maangavu, tuangalie nyuma tulikotoka. Tuangalie tulipo sasa. Ndio, tufanye hivyo ili tuutafute mwelekeo mwema wa nchi yetu hata kwa miaka mingine hamsini ijayo.


Tuna maswali mengi ya kujiuliza, moja kuu ni hili; Je, ni nchi ya namna gani tutayotaka kuijenga na hata kuvirithisha vizazi vijavyo? Kwa maneno mengine; ni jamii gani tunayotaka kuijenga? Sisi wa ’ Kizazi Cha Azimio’ tulikuwa wadogo sana katika miaka kumi ya mwanzo ya uhuru na hata utekelezaji wa Azimio la Arusha. Nimezaliwa Ilala, Dar es Salaam, Machi 11, 1966.


Ndio, kuna mema mengi tuliyoyaona, lakini, tukitafakari sasa, kuna mabaya mengi pia tuliyoyashuhudia. Tuna wajibu wa kusimulia mema na mabaya hayo kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Kati ya kumbukumbu zangu mbaya za wakati huo ni jinsi tulivyowaona wazazi wetu wakiishi kwa hofu. Waliogopa kushutumu mamlaka hadharani na kwa sauti. Waliishutumu Serikali na hata kiongozi mkuu wa nchi kwa kunong’ona. Wazazi wetu walimwogopa hata mjumbe wa nyumba kumi.

Ni ukweli, kuwa kwa wakati ule, Serikali na chama tawala havikuwa na uvumilivu wa sauti za upinzani.

Na siku zote, mamlaka bila upinzani huzaa kiburi na majigambo. Huzaa hali ya kutokujali na kukosa usikivu. Taratibu, huzaa hali ya kujisikia u-bwana mkubwa. Hali hii ikiachwa ikaendelea, basi, husababisha madhara makubwa kwa nchi. Huleta hasara kubwa kwa nchi, kiuchumi na kijamii.

Juma la jana nilimalizia kwa kuandika, kuwa makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa juu ya nini kilitokea takribani miaka hamsini iliyopita. Ni mmoja tu wa mfano , wa jinsi umma ulivyofichwa ukweli wa juu ya nini hasa kilitokea kikasababisha mfarakano wa waliopata kuwa viongozi wa mstari wa mbele kwenye harakati za kuanzishwa kwa TANU na kudai uhuru wa Tanganyika; Julius Kambarage Nyerere na Oscar Salathiel Kambona.


Kuna aliyesoma makala yangu ya juma la jana na kuniuliza; ” Maggid, hivi wewe huogopi?” Ni kweli, kama ningeandika haya mwaka 1976 nilipokuwa mtoto wa umri wa miaka kumi tu, basi, vyombo vya dola vingenishukia mithili ya mwewe anayekishukia kifaranga cha kuku. Sio tu mimi ningeswekwa rumande ya watoto, bali hata mama na baba yangu wangetikiswa na dola kwa ’ dhambi’ ya kumzaa mtoto mwenye fikra za ’ kipinzanipinzani ’ na ’ kihainihaini’. Mtoto ’ anayepingapinga’ tu!


Na hapa ndipo kwenye moja ya mapungufu makubwa ya waliojenga msingi wa taifa letu; kuchukia wenye kufikiri tofauti na watawala. Na zaidi kuwachukia wenye ’ akili’ ya kufikiri na kuutumia vema welewa wao- hostility towards execelency. Si tunajua, kuwa utotoni tulisikia kuna maadui wa nchi wa aina mbili; maadui wa nje na wa ndani. Wapinzani ama wenye kufikiri tofauti ndimo walimowekwa wanaoitwa ’maadui wa ndani!’


Niseme tu, mfulilizo wa makala haya ni moja ya makala zangu muhimu tangu nianze kushika kalamu na kuandika makala magazetini. Na naandika nikiwa sina hata chembe ya hofu. Ni kwa sababu moja kuu; kuwa yanahusu historia yetu na mustakabali wa nchi yetu. Sote tuna wajibu wa kuandika historia yetu.


Hii ni nchi yetu. Hatuna sababu za kuionea aibu historia yetu, badala yake, tujivunie, kuwa tuna historia. Na ni unyonge na utumwa kusubiri wasomi kutoka Marekani na Ulaya waje kutafiti na kutuandikia historia yetu. Historia yako isimulie mwenyewe. Hivyo basi, tuna wajibu wa kuifanya kazi hiyo. historia itusaidie kutukumbusha machungu na furaha ya tuliyoyapitia kama taifa. Si kwa kuandika tu, hata kwa kusimulia machache tuliyoyashuhudia.


Niliahidi kuchambua zaidi juu ya marafiki hawa watatu; Kambona, Nyerere na Kawawa. Nitafanya hivyo sasa.

Naam. Julius na Oscar walikuwa viongozi vijana sana katika Tanganyika huru ya wakati huo. Ikumbukwe, wakati tukipata uhuru, Nyerere alikuwa na miaka 39 na Oscar alikuwa na miaka 36. Hawa walikuwa ni vijana waliokabidhiwa dhamana kubwa ya kuingoza nchi kubwa ya Tanganyika. Naamini, walikuwa ni wenye dhamira njema kwa taifa hili; Julius, Oscar, Rashid na wenzao wengine katika TANU.
Ukweli unabaki, kuwa Oscar Kambona hakuikimbia nchi yake kwa kashfa ya kuiba fedha ya Serikali au ufisadi mwingine. Na kwa utafiti mdogo tu niliofanya, nilichobaini, ni ukweli kuwa marafiki hawa wawili; Oscar na Julius walikuwa na mgongano wa tofauti ya kimaono ya kisiasa yaliyoathiri hata urafiki wao.

Maana, haiyumkini Kambona aliyeaminiwa na Nyerere akaja kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa TANU, akawa Waziri wa kwanza wa Elimu wa Tanganyika huru, akaja kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na hata kwa wakati mmoja kushika wizara mbili; Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Nje. Kwamba, aje tena baadae kutuhumiwa uhaini na hata kushukiwa uraia wake.


Ndio, kwangu mimi, ya Kambona na Nyerere ilihusu zaidi mgongano wa tofauti za kimaono ya kisiasa . Na ukiingia kwa undani kwenye maandiko na simulizi utaupata ushahidi wa haya. Na kwa hakika, ili siasa ya nchi istawi, basi, inahitaji uwepo wa migongano ya kifikra. Hivyo basi, siasa ni migongano ya kifikra yenye kuhitaji majadiliano endelevu.


Tunaona, kuwa migongano ya kifikra kati ya Oscar na Julius ilianza kuonekana dhahiri katika ziara mbili walizozifanya kwa pamoja katika mataifa mawili tofauti. Ziara ya Marekani mwaka 1963 na ziara ya Uchina mwaka 1965. Na hapo katikati kuna jambo lililoopelekea uwepo wa mahusiano ya mashaka kati ya Julius na Oscar. Ni uasi wa jeshi wa Janauri 20, 1964.


Uasi ule ulipelekea Nyerere na Kawawa waende mafichoni, inasimuliwa walijihifadhi eneo la Kigamboni. Mjini alibaki Oscar Kambona aliyeshiriki kikamilifu kuwatuliza wanajeshi wale. Kimsingi, katika kipindi kile cha maasi, Kambona, kama angetaka, alikuwa na fursa ya kutwaa mamlaka ya nchi akisaidiwa na jeshi. Inasemwa, kuwa akiwa Waziri wa Ulinzi, Kambona alikubalika sana jeshini.


Baada ya ziara ya Marekani akiwa na Oscar Kambona mwaka 1963 ambako Rais John Kennedy alimsifia sana Nyerere kwa kuonyesha uwezo wa kiungozi , miaka miwili baadae, mwaka 1965, Nyerere na msafara wake akiwamo Oscar Kambona walikwenda China kwa mara ya kwanza na kulakiwa na Mwenyekiti Mao Tse Tung. Nyerere akiwa kwenye gari la wazi na mwenyeji wake Mao , alishangiliwa na Wachina wapatao milioni moja waliojipanga barabarani.

Pale Ilala tulikoishi, nakumbuka nikiwa na umri wa miaka sita tu, usiku mmoja pale viwanja vya shule ya msingi Boma tuliangalia sinema ya ziara ya Julius Nyerere Uchina . Nyerere aliiona China na alivutiwa sana. ” What we have seen in China is relevant to us”. Nimemsikia Nyerere akiongea hayo kwenye kipande cha filamu ya zamani kilichopo mtandaoni . ” Ana maana, walichokiona China kinaweza kikafanyika kwetu. Na Julius alianza kwa kubadilisha hata staili yake ya mavazi, yakafanana na ya Mwenyekiti Mao, na wengine katika TANU wakamwiga.

Ni nini kilitokea kwenye Mkutano wa TANU wa Januari, mwaka 1967 na kabla ya hapo. Mkutano uliopelekea kumalizika kabisa kwa urafiki wa Nyerere na Kambona. Fuatilia toleo lijalo.

http://mjengwa.blogspot.com/ http://mjengwa.blogspot.com
 
Nice story..., but to make it credible I think more facts are needed which am afraid if you have them... Soo Many inasemwa na Inasemekana....
 
Nimezaliwa Ilala, Dar es Salaam, Machi 11, 1966...................kama ningeandika haya mwaka 1976 nilipokuwa mtoto wa umri wa miaka kumi tu, basi, vyombo vya dola vingenishukia mithili ya mwewe anayekishukia kifaranga cha kuku. Sio tu mimi ningeswekwa rumande ya watoto, bali hata mama na baba yangu wangetikiswa na dola kwa ’ dhambi’ ya kumzaa mtoto mwenye fikra za ’ kipinzanipinzani ’ na ’ kihainihaini’. Mtoto ’ anayepingapinga’ tu!

Na sasa Maggid akiwa na miaka 45, ameamua kuandika yale anayodai aliyashuhudia lakini hangethubutu kuyaandika nyakati hizo akiwa na miaka 10 ! Kweli mwenye macho haambiwi tazama.
 
Taarifa:Mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF haitwi Ahmad Rashid bali Hamad Rashid
 
Nimemsikia Nyerere akiongea hayo kwenye kipande cha filamu ya zamani kilichopo mtandaoni . "
Unaweza kutupa hiyo link Maggid?Ningeshukuru.
 
Ahmed Rashad Ali alikuwa radio announcer ya Sauti ya Cairo miaka 1950s/1960s halafu alirudi Tanzania na akafanya kazi kwa Idara ya Maelezo....
 
Mods something wrong somewhere this post is supposed kuwa UKWELI KUHUSU KAMBONA
Naona kuna some matatizo yametokea please rectify it
 
Back
Top Bottom