MAONI YALIYOKAA SAWA
17- MAONI YALIYOKAA SAWA
Alipokuja Nabii Muhammad s.a.w. mambo yote yaliwekwa sawa. Mafunzo safi ya Musa yalirejeshwa pahala pake, na dini ya Yesu ilisafishwa na kutolewa takataka za Upaulo. Zote dini hizo mbili, Uyahudi na Ukristo, bali dini zote zilizogeuka zilirejeshwa kwenye umbo lao la asli lisiloharibika, umbo la Uislamu. Muhammad s.a.w. alifunza kwa uwazi kabisa juu ya dhambi, na akalegeza mikazo iliyokuwa imewabana Mayahudi. Alifahamisha kuwa baadhi ya mikazo hiyo ni matokeo ya inda yao wenyewe na uasi wao, na mingine ilizuliwa na makuhani wao tu ili wazidi kuwakandamiza na kuwaendesha watakavyo wafuasi wao. Upande mwingine hakuwaacha watu wakitangatanga gizani bila ya uwongozi, wala hakuwaacha watu watende horera watakavyo au kuwaambia watazame maandishi ya kale ambayo jinsi yalivyo chafuliwa kwa maongezo na mabadiliko hata mtu hawezi kutambua lipi la kweli na lipi la uwongo, lipi la Mungu na lipi la matamanio ya binaadamu. Kuachia mambo hivyo huzidisha zogo penye fujo. La! Muhammad alikuja na Qur'ani, kitabu cha kusomwa, au kwa jina jingine, Furqan, yaani Kitabu cha kufarikisha, yaani kupambanua, baina ya haki na baatili, baina ya kweli na uwongo. Alileta Sharia, Sharia ya Kweli ya Mwenyezi Mungu, iliyomkomboa binaadamu kutokana na minyororo iliyowatatiza Mayahudi, lakini haikuacha mambo ovyo kila mtu atende atakavyo kama alivyofanya Paulo kuivunja sharia kabisa. Huo ni utumwa mwingine ambao ni mbaya zaidi, kwa kuwa ni utumwa wa ubongo na roho, kuuwachilia mwili utende upendalo na kuifunga akili isifikiri na roho isinawirike. Sharia ya Qur'ani ni sharia ya kati na kati. Dini ya Kiislamu ni ya kati na kati. Si ya kulia wala kushoto lakini ya kuongoza mbele moja kwa moja kumfikilia Mwenyezi Mungu. Anasema Mola Mlezi katika Qur'ani:
Adhabu yangu nitamfikishia nimtakaye, na rehema yangu imekienea kila kitu. Lakini nitawaandikia wale wanaomcha Mungu, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini Aya zetu, ambao wanamfuata Mtume, Nabii asiyejua kusoma na kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomuamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.
(Qur'ani) Al Aaraf 7.156-57
Huyu ndiye Roho wa Kweli aliyetolewa bishara yake na Yesu kama ilivyo katika Injili ya Yohana sura ya 16. Ni yeye ambaye amesimuliwa kuwa "akisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu...huyo roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote." Ni huyu Muhammad s.a.w. ndiye aliyeambiwa Nabii Musa a.s. na Mwenyezi Mungu katika Kumbukumbu la torati sura ya 18:
Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe.
Kumbukumbu 18.18
Mafunzo ya Nabii Muhammad ndiyo yale ya Nabii Isa na ndio yale ya Nabii Musa na Nabii Ibrahim na kila Nabii aliyetokana na Mwenyezi Mungu. Msingi wao ni mmoja. Sharia zaweza kukhitilafiana kwa mujibu wa zama na hali, ama Imani na mambo ya kiroho na wema na ubaya hayo ni mamoja. Qur'ani imetilia nguvu sana juu ya Imani, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu, Imani kamili ya fadhila na neema ya Mwenyezi Mungu.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu asingelitakasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja.
(Qur'ani) An Nur 24.21
Lakini kumuamini Mwenyezi Mungu ni kutenda yale ayapendayo. Kama asemavyo Jalaludin Rumi, mshairi sufi mkubwa: "Ukimuamini Mwenyezi Mungu muamini kwa vitendo vyako! Atika mbegu, tena ndio mtegemee Mwenyezi Mungu!" Mswahili akichukua jembe kwenda kondeni husema: "Nenda omba Mungu."
Alikuwapo mtu mmoja akamuuliza Mtume s.a.w. amwachilie ngamia wake naye akimtegemea Mwenyezi Mungu? Mtume alimjibu: "Mfunge ngamia wako, ukisha ndio mtegemee Mwenyezi Mungu."
Qur'ani imejaa maneno kama haya: "Wanaoamini wakatenda mema". Na Yesu naye amefunza haya haya kama yaliyomo katika maneno yake mwenyewe, sio ya Paulo. Na waraka wa Yakobo, nduguye Yesu, unasema hivyo hivyo.