Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Mwanahabari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu amesema Tanzania inapaswa kujipa muda katika kujenga mifumo bora ya kidemokrasia, akitolea mfano uchaguzi wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa mapema Januari 2025, kama miongoni mwa chaguzi za mfano zilizofanyika kwa uwazi.
Akizungumza katika Jukwaa la Demokrasia, jana Agosti 28, 2026, Ulimwengu amesema Tanzania itaendelea kuwepo kwa miaka mingi, hivyo hatua zinazochukuliwa sasa zinapaswa kuzingatia pia vizazi vijavyo.
“Tujipe muda, tusiwe na haraka. Tunakwenda wapi? Nchi hii itakuwepo miaka mia tatu, mia tano ijayo. Tunatengeneza si tu kwa ajili yetu sisi, ni hao wanaokuja baada yetu.”
Amesema suala la uchaguzi linapaswa kuangaliwa kwa umakini, akitaja malalamiko ya madai ya Wananchi kunyimwa uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka.
Ulimwengu amesema katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, uchaguzi wa ndani wa CHADEMA umeonyesha kiwango cha uwazi na ushindani ambacho, kwa mtazamo wake, kinaweza kulinganishwa na mifumo ya uchaguzi inayosifiwa katika baadhi ya nchi za Afrika.
Ametaja Botswana, Ghana, Cape Verde na Mauritius kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikisifiwa kwa namna chaguzi zao zinavyoendeshwa.
Kwa mujibu wa Ulimwengu, tofauti kubwa ni namna mchakato wa kupiga na kuhesabu kura unavyosimamiwa kwa uwazi, akisema uchaguzi wa ndani wa CHADEMA uliwahi kuonesha mfano wa utaratibu huo.
“Kura zinapigwa na hakuna ile ya kusema "ukishapiga kura, ondoka nenda nyumbani kajenge nchi". Nakwenda kujenga nchi gani? Najenga nchi kwa kuangalia uchaguzi inakwendaje hapa. Na wakati wa kuhesabu, zinachukuliwa kura moja moja na wananchi wanaona. Kila kura inasopolewa moja moja, inawekwa hapa, nyingine hapa mpaka mwisho, ndivyo wanavyofanya nchi zilizostaharabika"
Ulimwengu amesisitiza kuwa Tanzania inapaswa kutumia muda kujenga mifumo inayowapa Wananchi uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka, badala ya kufanya mabadiliko kwa haraka bila kujenga msingi imara.
Chanzo: Jambo TV