Kundi Kazi la Umoja wa Mataifa kitengo kinachoangazia, Kuwekwa Kizuizini Kinyume cha Sheria ( Arbitrary Detention ), limeeleza kuwa kufungwa kwa Kiongozi wa Upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ni kinyume cha sheria na limetaka aachiliwe mara moja.
Katika maoni yake yaliyopitishwa katika kikao cha 104, Kundi Kazi hilo lilibaini kuwa kukamatwa na kuendelea kuzuiliwa kwa Lissu kwa tuhuma za uhaini hakuna msingi wa kisheria na kunakiuka viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Lilitaja kuwa utaratibu wa kisheria wa Tanzania wa kuweka mahabusu kwa makosa yasiyo na dhamana unapingana na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.
Aidha, paneli hiyo ilisisitiza kuwa kumfungulia Lissu mashtaka ya uhaini kwa kauli alizotoa katika mkutano wa kisiasa ni kizuizi kisichokubalika kwa uhuru wa kujieleza na kukusanyika.
Kundi Kazi la Umoja wa Mataifa limeitaka Serikali ya Tanzania kumwachia Lissu bila kuchelewa na kuhakikisha fidia kwa kifungo chake kisicho halali, likionya kuwa kesi yake ni sehemu ya mtindo mpana wa kukandamiza sauti za upinzani nchini.