Muungano wa Ulaya, Marekani na Uingereza zimeshutumu shambulio dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe siku ya Jumanne.
Katika taarifa tofauti zilizowekwa katika tovuti zao, jamii hiyo ya kimataifa imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuanzisha uchunguzi na hatimaye kukamatwa kwa wale wote waliohusika na shambulio la kiongozi huyo wa upinzani.
Freeman Mbowe alivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma huku viongozi wa chama chake wakidai kwamba shambulio hilo lilishinikizwa kisiasa.
Katika taarifa yake Muungano wa Ulaya umesema kwamba shambulio lolote dhidi ya mwakilishi wa taasisi ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ni shambulio dhidi ya demokrasia.
Na huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa miezi michache ijayo , EU imesema kwamba ni muhimu kuwacha demokrasia kuendelea kushamiri ili kuhakikisha kuwa kuna mazingira ya usawa katika uchaguzi wa haki na ulio wazi.
''Tunaamini kwamba mamlaka itafanya uchunguzi, kuwakamata na kuwashtaki wahusika'', ilisema taarifa hiyo ya EU.
Kwa Upande wake ubalozi wa Marekani umesema kwamba tukio hilo ni la kikatili na lisilo la sababu.
Ubalozi huo umesema kwamba umesjhtushwa na tukio hilo na kutoa pole kwa mbunge huyo na familia yake.
''Ubalozi wa Marekani umeshtushwa na kuhuzunishwa na tukio la kikatili la kushambuliwa kwa mbunge na mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe tarehe 9 Juni, tunatoa pole kwa mbunge huyo na familia yake'',ilisema taarifa hiyo.
Ubalozi huo umelitaja shambulio la kiongozi huyo wa Chadema miongoni mwa mlolongo mrefu wa matukio ya kusikitisha ya utumiaji wa nguvu na unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani.
Aidha ubalozi huo umetambua kwamba mojawapo ya mashambulio hayo ya kikatili dhidi ya viongozi wa upinzani ni jaribio la mauaji lililotokea tarehe 7 mwezi Septemba 2017 dhidi ya Tundu Lissu ambalo ufumbuzi wake haujapatikana hadi leo.
Nao ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania umesema kwamba kila mwansiasai nchini Tanzania anapaswa kuwa na uhuru kuwakilisha eneo bunge lake bila ya hofu ama ghasia , hususan wakati ambao kampeni za uchaguzi wa 2020 zinaanza.
Kwa sasa kiongozi huyo wa Chadema anaendelea kupata matibabu katika moja ya hospitali zilizopo jijini Dodoma.
Shambulio dhidi ya Bwana Mbowe linakuja siku moja baada ya mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu kutangaza rasmi nia ya kuwania urais kupitia chama cha Chadema.
Je Mbowe ni nani?
Freeman Mbowe ni mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Tanzania.
Mbowe ni moja ya wanasiasa walioasisi uanzishwaji wa Chadema mwaka 1992, wakati huo akiwa kijana. Alichaguliwa kuliwakilisha jimbo la Hai kwa mara ya kwanza mwaka 2000.
Mwaka 2005 aligombea urais na kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Prof Ibrahim Lipumba wa CUF na aliyeibuka mshindi Jakaya Kikwete wa CCM.
Mwaka 2010 alirejea kwenye ubunge na kuchaguliwa tena 2015.
Mbowe yupo madarakani kama kiongozi mkuu wa Chadema kwa zaidi ya miaka 15 sasa.
Kwa wafuasi wake, anaonekana ni kiongozi mahiri aliyeweza kuiongoza Chadema kutoka chama kidogo cha upinzani kuwa wapinzani wakuu ambapo chama hicho kilianza na wabunge watano hadi 50.
Mbowe pia amekuwa moja ya wakosoaji wakuu wa serikali ya rais John Pombe Magufuli, hatua ambayo inampa sifa ya uthabiti.
Hata hivyo, kwa wapinzani wake ndani na nje ya Chadema wamekuwa wakimshutumu kiongozi huyo kwa kuminya demokrasia ndani ya chama chake.