SoC01 Umuhimu wa kuwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotekelezeka kwa wakati na kwa kuzingatia rasilimali zilizopo

SoC01 Umuhimu wa kuwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotekelezeka kwa wakati na kwa kuzingatia rasilimali zilizopo

Stories of Change - 2021 Competition

Abrianna

JF-Expert Member
Joined
Mar 30, 2021
Posts
4,696
Reaction score
15,390
Utangulizi
Dira kwa maana fupi ni muelekeo. Dira ya Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Development Vision (TDV) 2025 ilianzishwa mwaka 1994 na kuzinduliwa rasmi mwaka 1999 ambapo utekelezaji wake ulianza mwaka 2000 lengo kuu likiwa kuongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii zitakazoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2025. 'www.tanzania.go.tz' (tovuti kuu ya serikali)

Melengo makuu matano yalioainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025 ni pamoja na kuboresha hali ya maisha ya kila Mtanzania, kuwepo kwa mazingira ya amani usalama na umoja,kujenga utawala bora,kujenga jamii iliyoelimika na kujenga uchumi imara unaokabiliana na ushindani. (Nukuu kutoka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025).

Katika andiko hili, nitaangazia malengo makuu matano kama yalivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025. Andiko langu litaangazia pia utekelezaji wa malengo haya na uhalisia wa maisha ya Mtanzania.

Katika uhalisia, Maendeleo ya Nchi yetu kwa asilimia kubwa yamekua yakitegemea Ilani ya chama tawala pamoja vipaumbele vya Rais aliye madarakani. Mfano halisi ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa madaraja ambao uliingiza nchi katika madeni makubwa na umaskini. Ni wazi kwamba Dira ya Maendeleo ni kijarida tu ambacho kimetengenezwa kutimiza wajibu lakini hakina nafasi kubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Serikali imeunda mipango mingi kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo kama vile mpango wa maendeleo wa miaka mitanpo (Five Year Development Plan), MKUKUTA, Mpango wa Big Results Now (Matokeo Makubwa Sasa), Mpango wa maboresho ya utumishi wa Umma,pamoja na Maleongo ya Maendeleo ya Millenia chini ya nchi za Umoja wa Mataifa.

Katika mipango tajwa, yote ina malengo yanayolandana kwa maana ya kutokomeza umaskini kwa kuboresha huduma za afya, elimu, nishati, kilimo, maji, biashara, mahusiano ya kimataifa, ajira, kuboresha utumishi wa umma, kuweka usawa wa kijinsia pamoja na mengine mengi.

Hebu tuangazie miaka kumi nyuma tulinganishe na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na hali halisi ya Watanzania mpaka leo hii.

Hali ya maisha ya Mtanzania imezidi kuwa duni pamoja na kwamba nchi yetu ipo katika uchumi wa kati wa chini, Mtanzania wa kawaida anashindwa kumudu gharama ndogo za mlo wa siku ilhali tunatangaziwa uchumi wetu umekua kwa asilimia 7% ( NBS 2019/2020).

Katika kujenga utawala bora, hali imezidi kuwa tete, ni wazi kwamba utawala wa sheria umekua jambo gumu katika nchi yetu hali inayopelekea kutokuwajibika kwa pamoja na ubadhirifu wa mali za umma (Rejea ripoti ya CAG 2020).

Katika Dira ya Mendeleo 2025, serikali imeonyesha nia ya kujenga jamii iliyoelimika na inayojifunza kila siku kulingana na mazingira na nyakati tulizopo, tukirudi kwenye uhalisia, kiwango cha ubora wa elimu zetu hakikidhi viwango vitakavyowawezesha wasomi wetu kuingia katika ushindani ndani na nje ya Tanzania, shule zetu nyingi hazina waalimu wa kutosha wala vifaa vya kufundishia, matamko ya kisiasa kwa upande mwingine yamekua yakiathiri mifumo ya elimu.

Kwa mfano mnamo mwezi Desemba 2020, Rais JPM aliagiza somo la historia ya Tanzania lianze kufundishwa katika shue za msingi mpaka sekondari, Wizara ya elimu iliandaa machapisho kwa ajili ya somo husika lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani somo hilo lilisitishwa rasmi.

Kwa upande mwingine serikali ilichangia kupotosha jamii badala ya kuelimisha. Nitoe mfano mdogo wa janga la Covid 19. Serikali ilisimama kidete kuuaminisha umma kwamba janga hili ni vita ya mabeberu dhidi yetu badala ya kutumia wataalamu wa afya kutoa elimu kuhusu namna bora ya kujikinga ili kuepuka maambukizi. Serikali ilienda mbali zaidi na kuhamasisha tiba mbadala na njia za asili ambazo zilitumika katika vituo vya afya pia.

Kauli ya serikali pamoja na viongozi wakuu wa nchi imeleta mkanganyiko pamoja na hisia tofauti juu ya janga hili na kusababisha watu kuishi pasipo kuchukua tahadhari hata baada ya serikali kubadili msimamo na kuamua kufuata njia za kitaalamu. Ukijaribu kuongea na watanzania kumi, tisa kati yao wanaogopa chanjo na kuamini kwamba mabeberu wanataka kutumaliza.
1626861526209.png
1626861576665.png

(picha kutoka mtandaoni)

Katika uboreshaji wa utumishi wa umma, vilio vimekua vingi, utekelezaji wa dhima hii umesahaulika kwa miaka zaidi ya mitano iliyopita, vilio vingi vya wafanyakazi kuhusu nyongeza za mishahara pamoja na kupanda madaraja, makato makubwa, na mishahara duni ambayo haikidhi maisha ya kila siku.

Mambo ya muhimu yaliyotajwa katika utekelezaji wa malengo ya milenia ni pamoja na kukuza mahusiano ya kimataifa, kutokomeza umaskini wa kipato na njaa. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepuuza kwa kiasi kikubwa sana mahusiano ya kimataifa kutokana na misimamo ya kiongozi aliyekua madarakani. Vipato vya wananchi vimeshuka kutokana na tozo kubwa katika bidhaa na huduma, mfumuko wa bei umeathiri pembejeo za kilimo na bidhaa mbalimbali, uonevu kwa wafanyabiashara,ubambikaji wa kesi na kodi uliosababisha biashara nyingi kufungwa. Tunao mfano halisi wa sasa katika tozo ya miamala ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi masikini ambao hata kula yao ni ya tabu.

Mapendekezo
• Serikali ianzishe taasisi maalumu kwaajili ya kuandaa na kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa. Chombo hicho kiwe na kazi ya kuandaa, kusimamia pamoja na kuishauri serikali iliyopo madarakani bila kujali chama.Taasisi hii ihakikishe sera sera na mipango ya taasisi mbalimbali za serikali pamoja na wizara zina uelekeo mmoja na zinashirikiana ka ukaribu. Kwa mfano suala la kuzalisha wahitimu wenye weledi ni lazima liendane na uboreshaji mfumo wa elimu, kwa hiyo ni lazima wizara ya kazi na wizara ya elimu zishirikiane kubaini mapungufu yanayoonekana kwa wahitimu wanaoajiriwa ili waweze kubaini njia bora ya kuboresha.

Taasisi hii ipewe mamlaka ya kusimamia serikali kama ilivyo bunge na mahakama na kwamba ilani ya chama cha kiongozi aliyeko madarakani ilenge kutafuta au kuonyesha njia sahihi za kuipeleka nchi kule ambako dira inaonyesha, hii itasaidia kutekeleza miradi iliyoachwa au iliyoanzishwa na kiongozi aliemaliza muda wake, mfano wakati Rais JPM naingia madarakani alisitisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kwa madai kwamba mikataba ilikua mibovu na iliyojaa unyonyaji, siku chache baada ya Rais Samia kuingia madarakani mapitio ya ujenzi wa bandari yameanza, hii ni kwa sababu hakuna mfumo wa kusimamia viapaumbele vya maendeleo ya Taifa badala yake kila kiongozi anajiamulia kile anachopenda.

• Ipatikane katiba imara ambayo itasaidia kudhibiti na kusimamia viongozi walioko madarakani na hata baada ya kustaafu kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Marekani na Afrika ya Kusini. Hii itahakikisha viongozi wote wanafanya kazi kwa kuheshimu haki za binadamu na sheria na taratibu zilizopo bila kuathiri malengo ya Taifa kwa ujumla. Katiba imara pia itasaidia kuweka uwajibikaji na usawa kati ya watumishi/viongozi, kuondoa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

• Serikali ijikite zaidi katika kuvumbua vyanzo vipya vya mapato badala ya kujikita katika kuongeza kodi katika huduma mbalimbali za kijamii ili kupunguza mzigo mkubwa wa kodi kwa wananchi na badala yake wananchi wapate unafuu wa maisha. Mfano sekta ya utalii na madini zinaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato kama tukiweka usimamizi mzuri na mifumo ya kuaminika ili kuepusha mianya ya ubadhirifu. Pia serikali ijikite katika kuboresha mfumo wa elimu ili kuruhusu vijana wengi kujiajiri katika nyanja mbalimbali badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

• Bajeti za maendeleo zilizoidhinishwa na bunge zisitumike kinyume na lengo ili tuweze kutekeleza mipango iliyopangwa katika mwaka wa fedha wa serikali. Huko nyuma tulishuhudia pesa zikipelekwa katika matumizi ambayo hayakuidhinishwa na bunge hali iliyochangia kukwamishwa kwa miradi mingi ya maendeleo iliyoidhinishwa na bunge. Bajeti inayoidhinishwa pia iende sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

• Serikali iunde mfumo shirikishi utakaosaidia wananchi kushiriki katika kuonyesha vipaumbele vya maendeleo pamoja na utekelezaji. Hii itasaidia wananchi kuwa wasimamizi wa moja kwa moja wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

• Serikali iwatumie wataalamu wa masuala ya uchumi walioko nchini badala ya kutumia wanasiasa pekee katika kuandaa bajeti na matumizi ya serikali, pia serikali ijenge utamaduni wa kuwatumia wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali nchini katika kuandaa na kusimamia sera mbali mbali kwaajili ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa pamoja na kuheshimu mawazo na maelekezo ya wataalamu katika sekta mbalimbali hata pale yanapotokea majanga yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu. Kwa kufanya hivi, tutapunguza au kudhibiti matamko ya kisiasa katika mambo nyeti yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu kama vile Afya, Elimu na Uchumi.

Hitimisho
Natoa wito kwa viongozi/wenye mamlaka, na watunga sera wa nchi, maamuzi yoyote wanayofanya yanaathiri au kufaidisha jamii nzima, wao ni sehemu ya jamii na hivyo wataathirika au kufaidika na maamuzi hayo kwa namna moja au nyingine. Ni vyema kufanya uchambuzi yakinifu kabla ya kufanya maamuzi ili kuepuka athari zozote zitakazoisababishwa na maamuzi yao ikiwa ni pamoja na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Asanteni Sana​
 
Upvote 1.3K
Nimesoma tena uzi,
hivi wenzetu wanaweza kuvunja wizara kweli au kuzihamisha? Yaani raisi wa marekani aseme anahamisha wizara au anaunda wizara mpya?

Kuna mambo ambayo tunafanya ni ya kienyeji sana. Yanakosa mipangilio.

Hivi uliwahi kujiuliza ni kwa nini tusiwe na mfumo mmoja wa miundombinu. Hapa unachimbua kuweka bomba, pale unachimbua kuweka gesi, huku nguzo ya umeme huku nguzo ya simu, huku cable ya taa.
Tatizo ni kwamba mambo mengi ya msingi yanayohitaji utatuzi wa kitaalamu yanatatuliwa kisiasa au kwa matamko ya siasa ndio maana kila jambo linakwenda hovyo kwa sababu tunapuuza wataalamu ambao wanaweza kuishauri na kuisaidia serikali kujenga mifumo mizuri katika sekta mbalimbali
 
Mkuu hili jukwaa ni geni kwangu, sijapata sana wasaa wa kulipitia...

Ngoja nitenge wasaa wa kupitia huku na kqa kuanzia nitaanza na uzi huu...

Ni kweli jukwaa geni na lipo kwa makusudi maalum na kipindi maalum.
Wanascholar wameandika mada zao na kuzileta hapa, lengo ni kuona jinsi gani maandiko yatabadili jamii katika nyanja tofautitofauti.
 
Dira ni nini? Ni muongozo wenye kuonesha uelekeo kutoka mahali ulipo kuelekea mahali pengine unapopataraji kupafikia

Maendeleo ni nini? Mabadiliko chanya ya kihatua yenye kuonyesha maboresho ya vitu au watu

Ili kuendelea, lazima kuwa na mikakati ya namna ya utekelezaji wa hatua moja baada ya nyingine, hii mikakati kwa lugha nyingine huitwa vipaumbele

Sasa ili mikakati iweze kutekelezwa inabidi uwe na Watu, Siasa, Rasilimali, Teknolojia, Elimu n.k

Sasa sisi kama taifa tumekuwa tukikwama sana kwenye eneo la Siasa, Elimu na Teknolojia
 
Umeandika vyema na kutoa suluhisho kwa mambo mengi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Je wenye mamlaka na watunga sera watazingatia haya mawazo yako mapana?

Natamani kama ipo namna ya kufikisha mawazo haya kwa wahusika.

Kama sio moja kwa moja basi hata upate sehemu tu ya kuchapisha kwenye majarida na magazeti.

Magazeti yetu yamejaa makala zisizo na tija na kuacha mambo ya msingi.

Hongera sana.
 
Najaribu kuvote, using mobile extension...lakini inaniletea mauzauza tu hapa

Cha muhimu zaidi ilikua kupata maoni na mchango wako mkuu, kwakua pia umependa kupigia kura bandiko, kwa web inakua rahisi zaidi. Ikiwa ni desktop view, kwa pembeni juu kulia kuna kimshale kitaonyesha kupigia kura bandiko, ikiwa ni mobile view, kwa chini kwenye reaction za kawaida, kuna ki alama cha mshale kikielekea juu pia.
 
Dira ni nini? Ni muongozo wenye kuonesha uelekeo kutoka mahali ulipo kuelekea mahali pengine unapopataraji kupafikiali

Maendeleo ni nini? Mabadiliko chanya ya kihatua yenye kuonyesha maboresho ya vitu au watu

Ili kuendelea, lazima kuwa na mikakati ya namna ya utekelezaji wa hatua moja baada ya nyingine, hii mikakati kwa lugha nyingine huitwa vipaumbele

Sasa ili mikakati iweze kutekelezwa inabidi uwe na Watu, Siasa, Rasilimali, Teknolojia, Elimu n.k

Sasa sisi kama taifa tumekuwa tukikwama sana kwenye eneo la Siasa, Elimu na Teknolojia

Na hii ndio sababu kubwa nilipenda kusikia maoni ysko. Kimsingi sio jambo rahisi kwa sababu linahusisha vitu vingi lakini pia matokeo yake yanagusa maeneo mengi ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Lakini pakiwa na nia, inawekekana.
 
Viongozi waliopo hawana uwezo wa kimaarifa kuweka na kutekeleza wazo lililopo mezani

Je, tuendelee kudumu katika hiyo hali?
Hakuna kitu tunaweza kufanya kama taifa?

Nafikiri ndio maana JF wamekuja na hizi stori za mabadiliko ili kuleta mwamko kwa jamii kufanya mabadiliko.
Nakubaliana kabisa na wewe kwamba, hawa waliopo, wanaweza wasilipokee hili wazo.
 
Dira ni nini? Ni muongozo wenye kuonesha uelekeo kutoka mahali ulipo kuelekea mahali pengine unapopataraji kupafikiali

Maendeleo ni nini? Mabadiliko chanya ya kihatua yenye kuonyesha maboresho ya vitu au watu

Ili kuendelea, lazima kuwa na mikakati ya namna ya utekelezaji wa hatua moja baada ya nyingine, hii mikakati kwa lugha nyingine huitwa vipaumbele

Sasa ili mikakati iweze kutekelezwa inabidi uwe na Watu, Siasa, Rasilimali, Teknolojia, Elimu n.k

Sasa sisi kama taifa tumekuwa tukikwama sana kwenye eneo la Siasa, Elimu na Teknolojia
Asante sana mkuu Watu8 umefafanua vizuri maana ya maneno muhimu sana yanayobeba maana halisi ya uzi huu, hii itakua kwa faida ya wengi.
 
Umeandika vyema na kutoa suluhisho kwa mambo mengi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Je wenye mamlaka na watunga sera watazingatia haya mawazo yako mapana?

Natamani kama ipo namna ya kufikisha mawazo haya kwa wahusika.

Kama sio moja kwa moja basi hata upate sehemu tu ya kuchapisha kwenye majarida na magazeti.

Magazeti yetu yamejaa makala zisizo na tija na kuacha mambo ya msingi.

Hongera sana.
Asante sana willpower

Huku Janvini tunao watunga sera, watafiti, wanasiasa na watu mbalimbali ambao wametamani kupata hili andiko, mmoja amesema anataka aliweke kwenye hansad ya bunge, nadhani ni hatua nzuri na tutazidi kufanya mawasiliano ya namna bora ya kupata andiko langu, kuna watu wa asasi za kiraia na watunga sera ambao wameonyesha interest ya kupata hili andiko, kwangu mimi naamini ni mwanzo mzuri na pia kuna maandiko mengi ambayo katika hili jukwaa ambayo yakiwafikia walengwa basi kutakua na mabadiliko chanya
 
Je, tuendelee kudumu katika hiyo hali?
Hakuna kitu tunaweza kufanya kama taifa?

Nafikiri ndio maana JF wamekuja na hizi stori za mabadiliko ili kuleta mwamko kwa jamii kufanya mabadiliko.
Nakubaliana kabisa na wewe kwamba, hawa waliopo, wanaweza wasilipokee hili wazo.
Lazima tutumie nguvu ili kuwapa nguvu watu wenye ari ya kufanya mabadiliko
 
Back
Top Bottom