SI KWELI UN yawataka wanawake wawe makini na wanaume kwa sababu, wanaume ni wchache sana?

SI KWELI UN yawataka wanawake wawe makini na wanaume kwa sababu, wanaume ni wchache sana?

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Source #1
View Source #1
Kumekuwepo na ujumbe unaosambazwa kwenye mitandao , hususan WhatsApp, ukidai kuwa Umoja wa Mataifa (UN) ulitoa ripoti katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 ikisema kuwa dunia ina watu bilioni 7.8, wakiwemo wanawake bilioni 5.6 na wanaume bilioni 2.2.

Ujumbe huo pia unadai kuwa UN iliwashauri wanawake kuwa makini katika mtazamo wao kuhusu wanaume, kwa sababu kati ya wanaume bilioni 2.2, bilioni moja tayari wameoa, milioni 130 wako gerezani na milioni 70 wana matatizo ya afya ya akili au magonjwa mbalimbali. Kwa mujibu wa ujumbe huo, baada ya kuwaondoa makundi hayo, kuna takriban wanaume bilioni moja pekee wanaopatikana kwa ajili ya ndoa.

Ujumbe huo unaendelea kudai kuwa kati ya wanaume hao bilioni moja, asilimia 56 hawana ajira, asilimia 3 wanafanya mapenzi ya jinsia moja, asilimia 1 ni mapadri wa Kikatoliki, asilimia 10 ni wazazi au ndugu wa karibu, huku asilimia 30 wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 65.

Kwa kutumia ufuatiliaji wa World Population Prospects 2024: Summary of Results, iliyochapishwa na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (UN DESA), imebainika kuwa ripoti hiyo haitoi takwimu wala ushauri unaodaiwa katika ujumbe huo. Ripoti hiyo ni toleo la mwaka 2024 la World Population Prospects na inahusu makadirio na mwenendo wa idadi ya watu duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watu duniani mwaka 2024 ilikadiriwa kuwa 8,126,964,000, sawa na takriban bilioni 8.13, na si bilioni 7.8 kama inavyodaiwa kwenye ujumbe huo. Ripoti hiyo pia inakadiria kuwa idadi ya watu duniani itafikia takriban bilioni 9.80 mwaka 2054 na bilioni 10.19 mwaka 2100.

Hivyo, takwimu ya msingi kuhusu idadi ya watu duniani katika ujumbe huo haiendani na takwimu rasmi za zinazodaiwa kutolewa UN.

Uchunguzi zaidi kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa instgram na ukurasa Tanzania National Bureau of Statistics (NBS) pia unaonyesha tofauti na madai yaliyomo kwenye ujumbe huo. NBS imenukuu makadirio ya idadi ya watu duniani kuwa bilioni 8.3, ambapo wanawake ni takriban bilioni 4.13, sawa na asilimia 49.7, huku wanaume wakiwa takriban bilioni 4.17, sawa na asilimia 50.3.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa uwiano wa wanawake na wanaume duniani uko karibu kuwa sawa, tofauti na madai ya ujumbe huo kwamba kuna wanawake bilioni 5.6 dhidi ya wanaume bilioni 2.2.

Katika hilo pia Madai kuhusu wanaume waliooa Ujumbe huo unadai kuwa kati ya wanaume bilioni 2.2, bilioni moja tayari wameoa. Hata hivyo, World Population Prospects 2024 haitoi takwimu hiyo wala kufanya hesabu ya wanaume wanaopatikana kwa ajili ya ndoa.

Ripoti ya UN inalenga kutoa makadirio ya ukubwa wa watu pamoja na mabadiliko na mwenendo wa idadi ya watu kwa kuzingatia mambo kama vile uzazi, vifo, uhamiaji, umri na jinsia. Haifanyi tathmini ya idadi ya wanaume ambao wako tayari au wanaostahili kuingia katika ndoa.

Ujumbe huo unadai kuwa wanaume milioni 130 wako gerezani.

Hata hivyo, hakuna takwimu hiyo katika World Population Prospects 2024. Ripoti hiyo haijaweka idadi ya wanaume walio gerezani kama sehemu ya makadirio yake ya idadi ya watu duniani. Kwa hiyo, madai hayo hayawezi kuhusishwa na ripoti hiyo ya UN.

Madai kuhusu afya ya akili Ujumbe huo pia unadai kuwa wanaume milioni 70 wana matatizo ya afya ya akili au magonjwa mbalimbali.

Uchunguzi wa ripoti ya UN haujaonyesha takwimu hiyo. Ingawa World Population Prospects 2024 inajadili masuala yanayohusiana na vifo, umri wa kuishi na mwenendo wa afya ya watu, haitoi takwimu inayosema wanaume milioni 70 wana matatizo ya afya ya akili au magonjwa mbalimbali.

Kwa mfano, ripoti inaonyesha kuwa wastani wa umri wa kuishi duniani ulikuwa takriban miaka 73.3 mwaka 2024, na unatarajiwa kufikia takriban miaka 77.4 mwaka 2054.

Madai kuhusu wanaume wanaopatikana kwa ajili ya ndoa

Kwa mujibu wa ujumbe huo, baada ya kuwaondoa wanaume waliooa, walio gerezani na wenye matatizo ya afya, kunabaki takriban wanaume bilioni moja wanaopatikana kwa ajili ya ndoa.

Hata hivyo, hakuna sehemu katika ripoti ya UN inayofanya hesabu hiyo. World Population Prospects ni ripoti ya makadirio ya idadi ya watu na mwenendo wake, si ripoti ya idadi ya watu wanaopatikana kwa ajili ya ndoa.

Ujumbe huo unaendelea kudai kuwa kati ya wanaume bilioni moja wanaodaiwa kupatikana kwa ajili ya ndoa, asilimia 56 hawana ajira, asilimia 3 wanafanya mapenzi ya jinsia moja na asilimia 1 ni mapadri wa Kikatoliki.

Hata hivyo, hakuna takwimu hizo katika World Population Prospects 2024. Ripoti hiyo haitumii takwimu za ajira, mwelekeo wa kijinsia au idadi ya mapadri wa Kikatoliki kufanya hesabu ya wanaume wanaopatikana kwa ajili ya ndoa.

Ujumbe huo pia unadai kuwa asilimia 10 ya wanaume hao ni wazazi au ndugu wa karibu, huku asilimia 30 wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 65.

Uchunguzi wa World Population Prospects 2024 haujaonyesha takwimu hizo. Ingawa ripoti inatoa takwimu kuhusu mgawanyo wa watu kwa umri, haitoi hesabu ya wanaume wanaopatikana kwa ajili ya ndoa kwa kuwaondoa wazazi, ndugu au watu wenye umri fulani.

Ripoti inaonyesha kwa ujumla kuwa idadi ya watu wenye umri wa miaka 65 au zaidi inaongezeka duniani, lakini hilo ni tofauti na madai kwamba asilimia 30 ya wanaume wote duniani wana umri wa zaidi ya miaka 65.

Uchunguzi umebaini kuwa ujumbe unaosambazwa WhatsApp unatumia jina la Umoja wa Mataifa na mada ya takwimu za idadi ya watu kuwasilisha madai ambayo hayajaungwa mkono na World Population Prospects 2024.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya UN, idadi ya watu duniani mwaka 2024 ilikadiriwa kuwa bilioni 8.13, si bilioni 7.8.
Aidha, hakuna ushahidi katika ripoti hiyo unaothibitisha madai kwamba wanawake ni bilioni 5.6 na wanaume bilioni 2.2, wala kwamba UN ilisema wanaume bilioni moja wameoa, milioni 130 wako gerezani au milioni 70 wana matatizo ya afya ya akili.

Kwa hiyo, madai kwamba Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti inayowashauri wanawake kuwa makini na wanaume kutokana na mgawanyo huo wa idadi ya wanaume ni UONGO.
IMG-20260825-WA0024.jpg
IMG-20260824-WA0001.jpg
 
Back
Top Bottom