SoC01 Uongozi bora ni chachu ya maendeleo chanya Tanzania na Afrika

SoC01 Uongozi bora ni chachu ya maendeleo chanya Tanzania na Afrika

Stories of Change - 2021 Competition

Kaladero

Member
Joined
Jul 16, 2021
Posts
6
Reaction score
3
UTANGULIZI
Viongozi wanaojitambua na kuzitambua vizuri kazi na majukumu yao ndilo jicho bora katika kutengeneza nchi yenye maono na muelekeo wa kujenga msingi mzuri wa maendeleo kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho .
Uongozi ni wajibu ,dhamana, jukumu, deni unalopaswa kulilipa kwa watu waliochini yako .Ni kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine huku tukikubali kuumia kwa manufaa ya watu .
Uongozi ni kuvaa hali za wengine kama hali yako ; kujitahidi kuishi katika hali ya wote bila kuliacha tabaka lolote katika malalamishi .Ni kukubali hali za watu ,taasisi au jumuiya katika nyanja zote na kuwa tayari kupambana kwa nguvu zote kuleta mabadiliko chanya .

Mambo yanazosababisha kukosa viongozi bora .

1.Shida kubwa imekuwa ni viongozi kutotambua vyema majukumu yao huku wengi wakichukulia uongozi kama ajira zaidi kuliko huduma inayotegemewa na jamii kutokana na nafasi hiyo. Jambo hili limesababisha sana kutokutimia kwa matakwa ya jamii huku ikiacha watu wakigombania nafasi hizi .

2.Changamoto pia imekuwa katika kutengeneza viongozi bora na hasa vijana ambao kwa namna moja au nyingine kutokana na ukosefu wa ajira , uongozi unatumika hasa kama fursa muhimu ya kujiongezea kipato na kutafuta umaarufu ili kujiimarisha na kujitengenezea mazingira kiuchumi kuliko kutumikia na kutatua changamoto nyingi zinazowakumba watu. Mfano ni baadhi ya viongozi vyuoni ambapo wengi utanguliza maslahi binafsi na kushindwa kuwasilisha changamoto zinazowakibili wanafunzi ili zitatuliwe.

3.Kukosaa dira maalumu ya maendeleo
katika kuliongoza taifa au taasisi mbalimbali imesababisha kukosa muunganiko mzuri pindi viongozi wanapoachia ngazi. Mataifa mengi ya Afrika na hata Tanzania​
tunaongozwa na vipaumbele vya kiongozi husika kuliko dira zilizowekwa .Hii imesababisha kutofautiana kiutendaji baina ya awamu za uongozi .

Mambo ya kuzingatia na kufuata katika kujenga uongozi bora na wenye tija .
1.Lengo la kila kiongozi bora ni kupiga hatua na kuleta maendeleo chanya kwa taasisi, jumuiya au nchi anayoiongoza. Kutekeleza hili inahitaji mipango mizuri na ya kimkakati ya maendeleo . Mipango inayolenga mafanikio kiuchumi ,kisiasa ,kibiashara na kijamii. Viongozi wengi katika mataifa ya Afrika wanakosa mipango mizuri ya kimaendeleo.

2. Mwanzo wa kila kiongozi na uongozi pindi tu uingiapo madarakani ni kuweka bidii katika kuendeleza mazuri yote yanayoachwa na watangulizi; tukiamini huo kuwa msingi mzuri katika kuendeleza kazi iliyoanza. Hii inaleta muunganiko mzuri na kuleta daraja zuri na imara la maendeleo katika kuvuka kipindi kimoja kwenda kingine. Wote ni mashuhuda wa maswali yanayoulizwa kwa sasa " kwanini kile hatukisikii kikiendelea?" Ni kwa sababu vipaumbele na mazuri yanayoachwa hayafuatiliwi vilivyo na viongozi husika , hii inasababisha miradi kudolola na kutumia muda mrefu kukamilika.

3. Kujiamini, uwazi, kujithamini na kuthamini wadhifa ni msingi bora katika uongozi .Uwazi ni pamoja na kutoa taarifa husika kwa watu na kwa muda sahihi. Hii inafanya watu wajione wahusika katika bidii mbalimbali zinazofanywa na viongozi. Ni vizuri kutoa taarifa za maendeleo ya miradi mbalimbali.Huu ni wajibu wa kila kiongozi.

4. Kuwaza zaidi katika kujenga misingi mizuri ya maendeleo endelevu kuliko kujikita zaidi katika kutatua matatizo kwa muda mfupi bila kuweka njia halisi za kuyaondoa matatizo hayo kiujumla. Mfano barabara nyingi huwa mbovu wakati wa mvua hivyo utengenezwa mara kwa mara na tatizo hujirudia kila mwaka ; kwanini bajeti ya ukarabati isiende kwenye utengenezaji kwa kiwango cha lami ili kusudi kidogo kidogo tatizo liishe mazima .

5 .Kukubali kujifunza huku tukiwa na tamaa ya kufanya kwa mafanikio mazuri tunayoyaona kwa wenzetu. Muda mwingi tunashindwa Kutekeleza miradi mbalimbali na mara nyingi kusubiria misaada yenye masharti kwa kujificha kwenye mwavuli wa umaskini. Ndugu zangu umaskini ni uwiano ,tajiri atapata elfu kumi kwa siku moja na maskini kupata mia tano kwa siku ,maskini huyu atakuwa sawa na tajiri baada ya siku ishirini. Kumbe tofauti ni muda lakini elfu kumi ni ile ile hivyo tusijiweke nyuma tunuie katika kufanya.

6. Uthubutu katika kutenda .Neno maskini limekuwa kificho na kufanya muda mwingi tukose uthubutu na maamuzi kwa mambo mbalimbali. Ni lazima kiongozi uweze kuthubutu bila kujishusha kutokana na hali yako.

7. Kiongozi kuwa mshawishi, ushawishi unaotoa muelekeo kwa maendeleo yanayoonekana, tusikubali kuwa wanasiasa wasio watendaji katika kazi .

8. Kuwa na uchu katika kufumbua matatizo mbalimbali. Umia kuona tatizo fulani linaendelea na wewe upo thubutu katika kuweza chochote kisicho na athari hasi kwa watu. Tusikubali kuyatunza matatizo . Barabara ina mashimo katikati yazibe haraka tusisubiri awamu ya vifusi ipite.

9. Furaha ya kiongozi ipo katika mafanikio ya anaowaongoza na si zaidi kwa mafanikio yake . Furahi kuona umekuwa daraja kwa wengine, watu wanafuraha kwa sababu yako, watu wanapiga hatua kwa mgongo wako ,kwa mawazo na usimamizi wako watu wanafanikiwa. Furahi kuona haki inapatikana kwa maamuzi yako kila mtu anahukumiwa kwa aliyoyatenda bila uonevu.

10. Jenga mahusiano mazuri na watu, watu waone uso wa kuelekea pindi wawapo na matatizo. Wewe unawaongoza watu na uko kati yao. Maendeleo ni kwa ajili yao usiwadharau waheshimu ,heshimu mawazo yao na kuyatafakari. Waliapo wengi tafakari kilio chao kwa kina na waliapo wachache kumbuka nao wako chini yako usiwaache. Usichukie kusemwa jitathimini kwa usemwacho lakini usichukue yaliyosemwa ni sahihi nayo yatathimini.

Hitimisho.
Tutengeneze viongozi bora hasa vijana ambao watakuwa na uelewa na uzalendo kwa mahitaji halisi ya nchi yetu. Malezi ya kupata viongozi yaanzie kwenye familia na taasisi za mafunzo kwa watoto na vijana ili kujenga kizazi chenye maadili , uaminifu na uchapakazi .

Tuwajengee mazingira mazuri vijana katika kujifunza na kuona uhitiji na umuhimu wa viongozi bora .

Tuyatunze mazuri tuliyonayo na kuyalinda.Tusiiharibu miradi mizuri ya kimaendeleo tunazorotesha uchumi wetu. Si vyema kutengeneza tunaharibu. Viongozi wawajibike katika kutunza miradi na miundombinu mbalimbali ndani ya nchi yetu. Ukarabati ufanyike kwa haraka pindi miradi hii inapoharibika. Inaumiza kuona watu wanagonga tu uzio kwenye daraja la kijazi na viongozi wanacha tu.
Kuibia umma si ujanja turekebike.

Nashukuru kwa usomaji wako ; usisahau kukomenti na kulifanyia kazi wazo ulilolipata ndani ya andiko hili. Asante.

Na, Kaladero
 
Upvote 0
Back
Top Bottom