MWAKYEMBE AWABWAGA MWAKALINGA, LOWASSA NA KYELA FM KWA KISHINDO
Na Malikira S.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Kyela aliyemaliza muda wake, Dk. Harrison Mwakyembe, amewabwaga kwa kishindo kikubwa wahasimu wake wa kisiasa kwenye kura za maoni zilizofanyika wilayani Kyela leo.
Muda wa saa kumi jioni ulipotimu wa kukamilisha upigaji kura, Mwakyembe alikuwa tayari anaongoza kwenye vituo karibu vyote kwa zaidi ya asilimia 75, akiwaacha kwa mbali wagombea ubunge wenzake 9 akiwemo George Mwakalinga anayeishi Uingereza na kuitumia redio yake, Kyela FM, kinyume na taratibu kwa kujitangaza kwa wiki mbili mfululizo kuwa chaguo bora na kumkandia Dk. Mwakyembe kuwa hafai.
Mwakalinga, mhandisi aliyekosa kabisa haiba ya uanasiasa kutokana na uongeaji wake wa taratibu usio na mvuto na hasira kali za papo kwa papo, anadaiwa kuwa karibu na Edward Lowassa, mwanasiasa mkongwe nchini aliyehamia CHADEMA kutoka CCM hivi majuzi, kutokana na kaka yake Mwakalinga kuoa Monduli.
Pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kumtahadharisha asiitumie kisiasa redio yake aliyoisajili kama redio ya jamii kwa kukejeli, kutukana na kudhalilisha wengine, Mwakalinga kwa kushirikiana na wanasiasa wenzake wanane walioungana naye kumkabili Mwakyembe, ameendelea kuitumia Kyela FM kumshambulia Dk. Mwakyembe na kuwasihi wananchi wasimpe kura.
Mwakalinga kwa kushirikiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela, Gabriel Kipija, mwanasiasa mchanga anayefundisha Chuo cha Uhasibu Mbeya, John Mwaipopo na mkandarasi anayetuhumiwa kuchelewesha miradi mitatu ya barabara wilayani Kyela, Vincent Mwamakimbula, wamekuwa wakiwalipa fedha wafuasi wa CHADEMA kumfanyia fujo Dk. Mwakyembe kwenye mikutano ya kujinadi kwa nia ya kumvunja moyo.
Dk. Mwakyembe kama ilivyo kwa wanasiasa wazoefu, hakuteteleka na aliendelea kuelezea utekelezaji wa Ilani za Uchaguzi za CCM za 2005 na 2010 na kuwathibitishia wananchi Kyela kuwa wilaya yao imepiga hatua kubwa ya maendeleo.
Idadi kubwa ya wananchi Kyela hawajafurahishwa na udhaifu wa TCRA wa kushindwa kusimamia sheria zake, hivyo kuiacha Kyela FM ikivuruga mchakato wa kidemokrasia ndani ya CCM kwa zaidi ya wiki mbili.
Taarifa tulizopokea toka kwa mawakala wa vituo karibu vyote wilayani Kyela zinaonyesha Mwakyembe akiwa mbele ya wagombea wengine na huenda akapata zaidi ya asimilia 75 ya kura zote.