Wapinzani wasafishiwa njia
na Sauli Giliard
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
BAADA ya vuta nikuvute ya miaka kadhaa, hatimaye serikali imeridhia kuandaa Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2008, ambao pamoja na mambo mengine, utatoa ruhusa ya kisheria kwa vyama kuungana na kusimamisha mgombea mmoja wa urais, ubunge na udiwani.
Uamuzi huo ambao sasa utawezesha muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti kabla ya kuwasilishwa rasmi Novemba mwaka huu, umetangazwa katika gazeti la serikali la Julai 18, mwaka huu.
Kwa sababu hiyo basi, iwapo wabunge watapitisha muswada huo na kuwa sheria, vyama vya siasa vitakuwa na uwezo wa kuungana na kuunda chama kimoja cha siasa, sambamba na kuwa na uwezo wa kusimamisha mgombea mmoja kama ilivyo katika nchi nyingine duniani zinazotumia mfumo wa vyama vingi.
Muswada unatoa mapendekezo ya kutunga sheria ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa kwa lengo la kuondoa kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria. Madhumuni ya kuondoa kasoro hizo ni kudumisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini, unasomeka muswada huo wa sheria.
Muswada huo unakuja wakati kuna jitihada za vyama vya siasa vya upinzani kujaribu kuungana au kuunda ushirikiano rasmi, vikianzia na ule waliopata kuuita NOF na baadaye Umoja wa Demokrasia Tanzania (Udeta) miaka ya 1990 kukwama na kufa. Aidha, muswada huo wa sheria unakuja wakati huu, vyama vinne vya upinzani vilivyounda ushirikiano usio rasmi vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF vikijaribu kutibu majeraha ya kunyosheana vidole na kuhitilafiana katika siku za hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, muswada huo ukipitishwa kuwa sheria, basi lawama ambazo serikali imekuwa ikiandamwa nazo kuwa imekuwa chanzo cha kuzorotesha na kukwamisha kukua kwa demokrasia ya vyama vingi zitapungua kama si kumalizika kabisa.
Mwaka jana Rais Jakaya Kikwete wakati akihojiwa na jarida maarufu la New African, alilazimika kujitetea akipinga tuhuma dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kwamba vimekuwa chanzo na kiini cha kuzorota kwa vyama vya siasa nchini.
Kwa kweli tunauhitaji upinzani. Mimi siwezi kuujenga upinzani, ingawa siwezi kuchukua hatua za kuunyonga. Tuko makini katika kuhakikisha kuwa wanastawi, na tunawapa fursa na uhuru wa kukua. Hilo ndilo jambo pekee tunaloweza kulifanya. Kinachobaki ni jukumu lao, alisema Kikwete wakati akijibu swali la mhariri wa The New African, Baffour Ankomah, wakati wa mahojiano hayo mwaka jana.
Majibu hayo ya Kikwete yanaweza yakawa na maana kubwa leo hii kutokana na uamuzi huo wa serikali kuandaa muswada huo ambao pamoja na mambo mengine utaipa mamlaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya maamuzi makubwa pasipo kupata ridhaa ya waziri mwenye dhamana ya vyama vya siasa kama ilivyo sasa.
Marekebisho yanayopendekezwa yanakusudiwa kumpa uwezo msajili wa vyama vya siasa kusajili viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa katika daftari maalumu na pia kufanya usajili mpya endapo vyama vitakuwa vimeungana na kuwa chama kimoja, inasomeka sehemu moja ya gazeti hilo la serikali.
Juu ya kuungana kwa vyama vya siasa, muswada huo unasema kutakuwa na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa kama ilivyopendekezwa katika vifungu vya 7 na 9, ambao watatakiwa kuomba usajili kwa msajili wa vyama vya siasa, ambaye ndiye atahusika na masuala yote ya vyama.
Muswada ambao umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge), umegawanyika katika sehemu kuu mbili, ambapo sehemu ya kwanza inahusu jina la sheria itakayoundwa wakati sehemu ya pili inahusika na mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa.
Muswada huo utatoa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuondoa kasoro zinazojitokeza, madhumuni ya kuondoa kasoro hizo yanakusudia kudumisha sheria ya vyama vingi vya siasa, inasomeka sehemu ya muswada huo.
Pia imeelezwa kuwa muswada huo, una lengo la kupunguza na kudhibiti maadili na vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Katika hilo, muswada huo unapendekeza kufutwa kwa usajili wa chama cha siasa ambacho kitaonekana kujihusisha na mambo yanayotishia uvunjifu wa amani.
Inapendekezwa kuzuia na kukataza chama cha siasa ambacho kitakachoruhusu wanachama wake kutoa lugha ya matusi ya udhalilishaji dhidi ya chama kingine, unasomeka muswada huo katika sehemu moja.
Muswada huo pia umekusudiwa kuwabana wanachama kuwa na uanachama katika vyama viwili ama zaidi, huku viongozi katika vyama vya siasa, wakitakiwa kuwa na vigezo kama vya mtu anayetakiwa kuwa mbunge kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 67.
Pia inapendekezwa kuwepo kwa baraza la vyama vya siasa litakalokuwa chini ya uenyekiti wa msajili wa vyama vya siasa, wakati wajumbe wake watatoka miongoni mwa vyama vilivyosajiliwa.