Hapa ninazungumzia Neno la Mungu la kwenye Biblia.
Wanasaikolojia wanakiri kuwa maneno yana uwezo mkubwa sana wa kumwathiri mtu. Ikiwa maneno ya kawaida yanaweza kusababisha mabadiliko, ni kwa kiwango gani Neno la Mungu linaweza kuleta matokeo yaliyoahidiwa na Mungu Mwenyewe? Kama unataka kusikia jibu, basi ujue ni kwa asilimia mia moja. Halijawahi kushindwa, na haitatokea lishindwe.
Ushauri nasaha unaweza ukashindwa. Sayansi inaweza ikakwama. Hata maombi yanaweza yakakwama, lakini si NENO LA MUNGU. Halijawahi kushindwa, halitakaa lishindwe.
Lakini nimeshawahi kuwasikia watu, tena wengi tu, wakikalamika kuwa Neno la Mungu halitendi kazi kwao. Hata mimi nilishawahi kupitia hiyo hali. Nilikuwa nikishangaa kwa nini pamoja na jitihada zote nilizokuwa nikizifanya, sikuwa nikipata matokeo! Kumbe ulikuwa ni ujinga wangu ndiyo uliokuwa ukinikwamisha kupata matokeo niliyoyatamani sana. Mungu hakuwa tatizo, tatizo lilikuwa kwangu, ujinga.
Niliugua vidonda vya tumbo kwa muda mrefu. Nilitibiwa hospitali mbali mbali bila mafanikio. Niliomba na kuombewa lakini bado vidonda viliendelea kuling'ang'ania tumbo langu. Lilionekana kama vile ni tatizo ambalo ningedumu nalo siku zote za maisha yangu.
Niliendelea kutumia dawa na kufuata maelekezo ya madaktari, yakiwemo ya kutokula vyakula fulani. Niliendelea pia kuomba, na hata kuombewa ilipopatikana fursa ya aina hiyo, lakini ilikuwa kama kutimiza wajibu tu. Sikutarajia kama ningeweza kupona tena. Ilikuwa kama vile nilikuwa nimekata tamaa, japo nilitamani sana kuondokana na hayo mateso. Lakini kwa sababu ya kuomba na kuombewa mara nyingi bila mafanikio, kulinifanya nikate tamaa ya kupona.
Mambo yalibadilika nilipoamua kujikita kwenye Neno la Mungu. Baada ya muda, niliyekuwa mateka wa vidonda vya tumbo, niligeuka kuwa mbabe dhidi ya magojwa. Vidonda vya tumbo havikuweza tena kuendelea kulifanya tumbo langu makazi yake. Viliisha kabisa. Ni miaka kumi sasa tangu nipone vidonda vya tumbo kwa imani. Sikuomba wala kuombewa. Neno la Mungu liliumbika moyoni mwangu, nikaamini nimeshapokea uponyaji, nikatenda kama aliyeponywa, na ikawa hivyo. Kesi ikawa imefungwa. Vilianza kunisumbua kwenye mwaka 2002 hivi, nikapona kwa imani mwaka 2013. Hatimaye vidonda vya tumbo kwangu vikawa Historia.
Neno la Mungu ni kama gari. Ni usafiri ulio wazi kwa kila msafiri. Litakufikisha kule alikosema Mmiliki Wake, Mungu. Lakini ni mpaka tu ulipande ndiyo utaweza kufika huko. Nje na hapo, utakuwa mtazamaji na msindikizaji .
Alichosema Mungu ndicho alichomaanisha.
Neno Lake linaponya, linafanikisha, ni ulinzi, ni hekima, ni kila kitu ilichosema.
JINSI GANI UNAWEZA KULIPANDA HILI GARI LIITWALO NENO?
Nitakueleza njia mojawapo ninayoifahamu! Ni kwa kulipa muda.
Kitu chochote cha thamani kinahitaji kupewa muda. Ndivyo ilivyo pia kwa Neno la Mungu. Ni muhimu kulisoma, lakini haitoshi kulisoma tu, ikiwa unataka kuona uthihirisho Wake katika maisha yako. Ni lazima kulitafakari.
Yoshua 1:8 inasemaje?
KITABU HIKI CHA TORATI KISIONDOKE KINYWANI MWAKO, BALI YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU, UPATE KUANGALIA KUTENDA SAWASAWA NA MANENO YOTE YALIYOANDIKWA HUMO; MAANA NDIPO UTAKAPOIFANIKISHA NJIA YAKO, KISHA NDIPO UTAKAPOSITAWI SANA.
Litafakari Neno. Hilo ni la muhimu sana, tena sana, kama shauku yako ni kuyapata matokeo iliyoyaahidi. Kusoma haitoshi! Kulifundisha haitoshi! Ni lazima na ni muhimu sana kulipa muda kwa kulitafakari
Ukifanya kiusahihi kama ilivyoelekezwa na Yoshua 1:8, utapata matokeo sahaihi. Mungu anamaanisha anachosema.
Kwa hiyo basi, chukua Andiko lenye Ahadi ya Mungu na uanze kulitafakari usiku na Mchana. Unachokihitaji kimo ndani ya Hilo Neno. Kadiri unavyolitafakari, ni kama vile unalifyonza kuingia rohoni mwako. Likiingia vya kutosha litajidhihirisha katika mazingira yako ya nje. Kama ni ugonjwa utayeyuka. Kama ni hofu itaondoka bila kuaga. Chochote kile unachokihitaji unaweza kukipata kwenye Neno. Kama imeahidiwa na Mungu, ni kwa ajili yako. Inakusubiria uichukue.
Na kutafakari Neno la Mungu kwa mujibu wa Biblia, ni pamoja na kulitamka. Usilitafakari kimya kimya tu, bali, ulitamke kwa sauti ya chini kwa kulirudia rudia mara nyingi sana kadiri iwezekanavyo. Hiyo ndiyo tafakari mojawapo ya Kibiblia.
Labda ni mgonjwa? unaweza ukatumia Isaya 53:5 kwa kujisemea kwa sauti, KWA KUPIGWA KWAKE YESU KRISTO NIMEPONA... Tuchukulie, kwa mfano, una mafua. Unaweza ukasema, KWA KUPIGWA KWAKE YESU, NIMEPONA MAFUA.
Unapata upinzani kwenye shughuli zako halali? unaweza ukatumia Zaburi 1:2-3 kwa kujisemea mara kwa mara kila siku, NINAPENDEZWA NA SHERIA YA BWANA, KWA HIYO KILA NINALOLIFANYA LINAFANIKIWA. Au 1Yohana 4:4; HAKUNA AWEZAYE KUNIKWAMISHA KWA SABABU ALIYE NDANI YANGU NI MKUU KULIKO YEYE ALIYE KATIKA DUNIA HII.
Unafanya kazi halali, labda umeajiriwa au unafanya biashara, lakini hupigi hatua kimaendeleo? Tumia Wafilipi 4:19. Jisemee mara nyingi kila siku, MUNGU AMENIJAZA KILA NINACHOKIHITAJI KWA KADIRI YA UTAJIRI WAKE KATIKA UTUKUFU NDANI YA KRISTO YESU.
Nisikuchoshe! Itoshe kusema kuwa NENO LINATENDA. Lilitenda kwa wengine, litatenda na kwako pia.
Kumbuka, MUNGU HANA UPENDELEO; Matendo 10:34.