Mimi bado kwa mtizamo wangu presha bado ni kubwa sana kwa Simba kwa usajili wa wachezaji wa kigeni. Ukiangalia kwa haraka haraka kwa hao wachezaji wa kigeni utaona wapo sawa lakini ni kwa ligi ya ndani tu pale unapopambana na Yanga mbovu na akina Ihefu huko lakini sio kwa CL. Pia mpira unabadilika na mwakani fedha za udhamini zimeongezwa kwa hiyo usitegemee kabisa ligi itakuwa rahisi. Pia usitegemee Yanga na Azam mbovu mwakani kwani kwa mafanikio iliyopata Simba mwaka huu kwenye CL jua wazi timu hasa Yanga wanakwenda kujiimarisha sana tu vinginevyo wasipotoa ushindani msimu ujao lazima bakora zitembee Jangwani na ni lazima GSM atatafutiwa mlango wa kutokea.
Tukija kimataifa bila kupepesa macho Simba itahitaji isajili wachezaji watatu wa kimataifa:-
1. Beki wa kati mmoja mwenye uwezo zaidi ya Onyango na Wawa. Kwenye CL japo Simba ilifika robo fainali kulikuwa na makosa yanaonekana wazi hasa kwenye krosi na kona hivyo inahitajika beki ambaye ataweza kufuta hayo makosa kwani wakati mwingine ilikuwa ni bahati tu washambuliaji wa timu pinzani walishindwa kuyatumia hayo madhaifu ya mabeki wa kati wa Simba.
2. Kiungo mmoja mwenye uwezo wa kukaba kweli kweli na ujuzi wa kushambulia "box to box midfield" ambaye ana umbo kubwa. Ukiangalia kwenye CL Simba ilikuwa inapata shida sana katikati kutokana na viungo wengi wa timu ya Simba wana maumbo madogo na wa timu pinzani wengi wao walikuwa mafundi lakini pia walikuwa na kitu cha ziada ambacho ni maumbo makubwa. Na hapa ashukuriwe sana aliyemleta Lwanga kwani kwa kiasi kikubwa ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyekuwa na uwezo wa kupambana nao kwenye zile 50/50.
3. Simba pia itahitaji mshambuliaji wa kimataifa mmoja mwenye uwezo zaidi ya Kagere na Mugalu. Ukiangalia kwenye CL Simba ilitengeneza nafasi nyingi sana lakini zilikuwa zinapotea. Kwa hiyo basi kuna uhitaji wa kumuondoa mshambuliaji mmoja kati ya Kagere na Mugalu na kuleta mwingine ambaye atakuwa anatumia hizo nafsi kwa usahihi sana. Pia uwezo mdogo wa Kagere na Mugalu kwenye kufunga kwa vichwa ni tatizo ukizingatia mabeki wa pembeni na viungo wa pembeni wa Simba wanapiga krosi nyingi sana tena kwa usahihi mkubwa.
Kwa vyovyote ilivyo kwa wachezaji kigeni waliopo Simba wanaweza leta ushindani kwenye ligi ya ndani na Simba ikafanya vizuri hata kwa misimu miwili ijayo. Lakini iwapo kweli Simba inataka kufika zaidi ya robo fainali kwenye CL basi lazima ilete wachezaji wapya wa kimataifa wasiopunguwa watatu. Sasa presha kwa Simba inakuja aachwe nani kati ya waliopo? Mbaya zaidi ni huu uswahili wetu kuwa Simba ikimuacha fulani ataenda Yanga. Lakini ili Simba wafanikiwe kwenda zaidi ya robo fainali ya CL ni lazima uongozi ujilipuwe ulete wachezaji wapya watatu wenye uwezo zaidi ya waliopo. Na kujilipuwa maana yake unaweza acha mchezaji akaenda fanya vizuri na yule uliyemleta japo mzuri zaidi akashindwa kuingia kwenye mfumo wako kama ilivyotokea kwa Chikwende. Haya ni maoni tu lakini naamini viongozi wa Simba wapo makini zaidi na watafanya yaliyo sahihi kwenye usajili ujao.