Katika kitabu chake Bw. Bergen, kiitwacho Development and Religion in Tanzania, katika Ukurasa wake wa 98 mwanadishi huyo anasema:- “Catholic Missionaries came to East Africa to find not new churches, but new provinces of the Roman Church” Kwa mujibu wa tafsiri yangu “Wamishionari wa Kikatoliki hawakuja hapa Afrika ya Mashariki kwa minaajili ya kuasisi Makanisa mapya, bali walikuja kuunda majimbo mapya ya Kanisa la Roma”. Ni kwamba, Tanzania (Tanganyika) ipo Afrika Mashariki, na kwa mujibu wa mwandishi Bergen, Tanzania nayo ni moja ya majimbo ya Kanisa la Roma, au kwa lugha nyepesi tuseme Tanzania ni Koloni la Vatican! Je, ni kweli Tanzania (Tanganyika) ni Koloni la Vatican? Padri. Dk. Sivalon, naye katika kitabu chake Kanisa Katoliki na Siasa za Tanzania Bara (1953-1985) anaeleza bayana kuwa Mwalimu Julius Nyerere Rais wa Kwanza wa nchi yetu, alikuwa kiungo pekee kati ya Chama (CCM), Serikali na Kanisa Katoliki.
Na kwa msingi huo viongozi wa Kanisa wamekuja kuwa na nafasi ya pekee kuelekeza hisia, mitazamo na siasa ya Tanzania, na wamefanya hivyo wakipania pia kuwa kuhujumu Uislamu. (Msomoe Sivalon Uk. 5-6,
katika kitabu chake hicho). Naye m mwandishi Bergen katika kitabu chake amemnukuu Mwalimu Nyerere akisema kamwe hawezi kwenda kinyume na kanisa lake. (Bergen Uk. 335). Agosti 3, 1970 Mwalimu Nyerere, alimwita Ikulu Padri Rweyemamu katika mazungumzo maalum ambapo Nyerere alimuahidi Rweyemamu kuwa, hivi sasa Kanisa ndilo lililoshika hatamu za kuongoza dola naye atahakikisha hali inaendelea kuwa hivyo. “Tanzania is not Catholic country, but Catholics is strong, I want to give the church a better chance here”. Akiwa na maana kwamba:- japo “Tanzania si nchi ya Kikatoliki, lakini Ukatoliki una nguvu, hivyo nataka kulipa Kanisa nafasi ya pekee hapa nchini” (Msome, Bergen Uk. 335). Na hali hii ya Kanisa kuwa na nafasi kubwa Serikalini iko wazi.
Waandishi wote hawa wanatuthibitishia kuwa, kuna ukweli fulani kwamba yapo mafungamano ya dhati kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania. Ni mafungamano hayo hayo ndiyo yameendelea kuwapa uweza viongozi wa Kanisa Katoliki kutoa maelekezo, maagizo na vilio vyao Serikalini na wakasikilizwa pamoja na kutekelezwa yale wanayoyahitaji hata kama yamelenga kuleta maafa kwa Waislamu. Mfano, mwaka 1998, Padri Lwambano, ambaye ni Paroko wa Kanisa Katoliki Mburahati Jijini Dar es Salaam, alisema kuiambia Serikali:- “Lazima Serikali ichukue hatua kali sana kwa Waislamu wanaoendesha Mihadhara, sababu ni watu wabaya kabisa, nimepita Sinza na Mwembechai, nimekuta Waislamu hao wanamtukana Yesu wanasema Yesu si Mungu”, alisema Paroko huyo na kuongeza; “Kama Serikali imeshindwa kuchukua hatua kali kukomesha Mihadhara ya Waislamu na kuendelea kutupaka matope kwa mgongo wa chupa, Serikali hii ijue sisi tutalishughulikia jambo hilo kwa nguvu zetu zote”.
Kauli hii ya Padri Lwambano, ilirushwa hewani na Kituo cha Radio Tumaini kinachomilikiwa na Kanisa hilo hapa nchini, Februari 13, 1998. Padri Lwambano bila kujali kuwa imani yake inaamini ‘Yesu ni Mungu’ na Waislamu imani yao inaamini ‘Yesu si Mungu’, aliinyooshea kidole Serikali nayo ilifuata bila kujali yenyewe (Serikali) haina dini na raia wake wana dini, kwa imani tofauti.
Katika utekelezaji wa agizo hilo bila shaka kila mtu anakumbuka kilichotokea. Ama kwa wale ambao walikuwa ni wadogo kipindi hicho ni kwamba Jeshi la Polisi lilifika Msikiti wa Mwembechai na kuuwa Waislamu kwa risasi na kikumbukumbu ni maarufu kwa ‘Mauaji ya Mwembechai’. Kufuatia madai hayo ya Padri Lwambano, viongozi kadhaa wa nchi walifikia hatua ya kuliomba radhi Kanisa Katoliki na Wakristo kwa ujumla. Majina na vyeo vya viongozi hao wakuu wa Serikali yanafahamika.
Baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi, kazi ya kukatili maisha ya Waislamu na kubaka haki zao, kiongozi wa Kanisa Katoliki hapa nchini Polycarp Kadinali Pengo, aliipongeza Serikali kwa upande mmoja na Polisi kwa upande wa pili kufuatia mauaji hayo hayo ya Waislamu, Mwembechai. Pongezi hizo alizitoa April 12, 1998 wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Dar es Salaam (DTV). Kanisa likionekana kuuchukukia vilivyo Uislamu, liliongeza harakati za siri na za wazi na kwa kutumia nguvu za dola ili kupunguza kwa upande mwingine nguvu ya Uislamu, maana kuuzima kabisa ni jambo lisilowezekana.
Askofu Mkuu Pengo alitoa taarifa ya kuenea Uislamu hapa Tanzania huku akihitaji msaada wa hali na mali katika kuhidhibiti hali hiyo. Na kwa kweli, Serikali ilitekeleza kudhibiti Mihadhara na Wahadhiri, ambapo wahadhiri maarufu nchini wakiongozwa na Habib Mazinge, walitiwa mbaroni na kutupwa Magerezani. Aidha sehemu ya taarifa yake ilisema hivi; “Uislamu umekuwa tishio kubwa sana kwa imani ya Kikristo nchini Tanzania, iwapo mihadhara ya Waislamu itaachwa iendelee, Kanisa litegemee kukimbiwa na waumini wake na kusilimu, kwa hiyo juhudi lazima zifanywe kuzuia Mihadhara hiyo.
“Tunashindwa kujibu hoja zao Waislamu sababu zina ukweli ndani yake”, maelezo haya yanapatikana katika kitabu cha Askofu Pengo kiitwacho Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwenye vijilia Sinodi ya Maaskofu wa Afrika kwa ajili ya Afrika.