Ushirikiano na uhusiano kati ya China nan chi za Afrika umedumu kwa miongo mingi sasa, na kuzinufaisha pande hizo mbili kidhahiri. China imekuwa mwenzi wa kutegemeka kwa nchi za Afrika, na imetekeleza ama inatekeleza miradi mingi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, bandari, na viwanja vya ndege.
Wakati Issah Abiola alipokuwa mdogo katika miaka ya 1990, aliona treni ikipita katika makazi yake nchini Nigeria. Mlio wa treni uliamsha hamu yake ya kuifahamu zaidi na akamuuliza baba yake kama treni hiyo, ambayo ilikuwa ndefu, inaendeshwa na mtu. Baba yake alipomwambia kuwa ni kweli inaendeshwa na mtu, Abiola akasema anatamani siku moja awe dereva wa treni, lakini baba yake alimkatisha tamaa na kumwambia haiwezekani. Jibu hili lilitokana na ukweli kuwa, wakati huo, kulikuwa na treni chache tu zilizokuwa zikifanya kazi nchini Nigeria, na kulikuwa hakuna madereva wanawake wa treni nchini humo. Lakini miaka 30 baadaye, ndoto ya Abiola imetimia, na amekuwa mwanamke wa kwanza nchini Nigeria kuwa dereva wa treni, na anafanya kazi katika kampuni ya Usafiri wa Umma wa Reli ya Abuja (ARMT) yenye makao yake makuu mjini Abuja.
Reli nyepesi ya mjini, iliyojengwa na kampuni ya Ujenzi na Uhandisi ya China (CCECC), ni ya kwanza katika mfumo wa usafiri wa kasi nchini Nigeria na Afrika Magharibi kwa ujumla. Pia ni mradi wa kwanza wa ustawi wa jamii chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI). Mwezi Mei mwaka huu, reli hiyo ilianza rasmi kufanya kazi baada ya kufanyiwa ukarabati na kutumia aina mpya ya mafuta ya dizeli yanayotengenezwa nchini China.
Sambamba na maendeleo ya usafiri wa treni, Nigeria pia imeshuhudia ongezeko la mtandao wa usafiri wa treni katika miongo ya karibuni chini ya BRI, jambo ambalo limeongeza maingiliano ya miundombinu katika bara la Afrika na kusaidia ukuaji wa uchumi katika njia za reli.
Mwaka huu ni miaka 11 tangu Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja lilipotolewa na China, ambalo chini yake ushirikiano kati ya China na Afrika umepata matunda mengi. Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) pia unatarajiwa kufanyika hapa Beijing kuanzia Septemba 4 hadi 6. Wafanyabiashara wanatarajia kuwa mkutano huo utaweka jukwaa jipya katika ushirikiano wa pande mbili, hususan katika maeneo kama elimu, mageuzi ya viwanda, maendeleo endelevu na uhamishaji wa teknolojia mpya, huu maeneo ya jadi ya ushirikiano kama maingiliano ya miundombinu yataendelezwa zaidi.
Maendeleo ya miradi iliyo chini ya BRI yameleta mabadiliko makubwa kwa Nigeria na Afrika kwa ujumla, na kuwezesha kuleta msukumo kuelekea mageuzi ya viwanda wakati huohuo yakiboresha maendeleo na ustawi wa kikanda. Mpaka kufikia mwezi Oktoba mwaka jana, kampuni za China zimesaidia kujenga zaidi ya kilomita 10,000 za reli, karibu kilomita laki moja za barabara, pia zimejenga madaraja karibu 1,000, bandari 100 na hospitali kadhaa pamoja na shule barani Afrika.
Wakati wa mkutano wa FOCAC uliofanyika hapa Beijing mwaka 2018, China ilitangaza Hatua Nane kubwa za ushirikiano na Afrika, huku muunganiko wa miundombinu na mawasiliano ya watu na watu yakipewa kipaumbele.
Wachambuzi wanasema, katika miaka michache iliyopita, FOCAC imejikita katika miradi midogo lakini yenye athari kubwa inayoboresha maisha, kuondokana na umasikini, mabadilishano katika masuala ya uongozi na maendeleo ya miundombinu. Wanatarajia kuwa mpango makini wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Afrika utajumuisha kasi ya sasa ya ushirikiano na kujumuisha Nyanja nyingine kama mafunzo ya pamoja ya kukuza vipaji, ujenzi wa uwezo na uratibu wa pamoja wa teknolojia zinazoibuka.