Zikiwa pande mbili kubwa zenye nguvu ambazo ziko tayari kuongoza muundo na mageuzi ya utawala wa hali ya hewa duniani, China na Umoja wa Ulaya zimedumisha mazungumzo juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na bioanuwai pamoja na masuala mengine ya kiuchumi na kisiasa. Ili kuimairisha ushirikiano huu wa pande mbili, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maingiliano makubwa huku zikishudiwa ziara za mara kwa mara baina ya China na Ulaya. Je ushirikiano huu unaiweka Afrika katika nafasi gani?
Umoja wa Ulaya unajiona kuwa ni kundi la juu zaidi katika historia linalotetea mashirikiano ya pande nyingi na kutaka kuwa kitovu cha kazi ya kuhimiza na kulinda ushirikiano huu pande nyingi duniani. Wakati huohuo China imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwepo kwa ushirikiano pande nyingi kupitia kauli mbiu yake maarufu ya ‘kuwa na jumuiya ya binadamu yenye hatima ya pamoja’. Kwa maana hiyo hakuna shaka yoyote kwamba mtazamo huu wa China na Ulaya unaijumuisha Afrika moja kwa moja katika kutafuta ufumbuzi wa masuala ya hali ya hewa pamoja na maendeleo ya dunia.
Suala la hali ya hewa duniani sasa limekuwa likiumiza vichwa vya watu wengi duniani, na hii ni kutokana na kuonesha makali yake karibu kila mahali na zaidi katika nchi za Afrika. Kwa sasa hakuna asiyefahamu kuwa Umoja wa Ulaya una msimamo mkali kwenye eneo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kujaribu kuwa kiongozi wa kimataifa katika eneo hilo. China nayo kama mshiriki katika uongozi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ni mwenzi wa kutegemeka wa Ulaya.
Ulaya na China zinaweza kushirikiana pamoja kupanua sera zao za hali ya hewa na kuongoza katika kuratibu juhudi za usalama wa ikolojia katika ngazi ya kimataifa. Hata hivyo ingawa Ulaya imeunda njia nyingi za kujihusisha barani Afrika, baadhi ya wakati huwa inakabiliana na China kwa sababu ushawishi wa nchi hii umeongezeka kwa kasi katika bara zima la Afrika.
Kupitia Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, China imetoa fursa mpya ya kikanda kwa ajili ya mazungumzo huru na ya moja kwa moja na washirika wake wa Afrika. Maendeleo haya yameitia wasiwasi Ulaya. Hata hivyo, kutokana na maendelo ya hivi karibu ya ushirikiano wa pamoja baina ya China na Ulaya na washirika wao wa Afrika, yameweza kushawishi na kuimarisha malengo ya diplomasia ya ikolojia na hali ya hewa.
Afrika sasa ipo kwenye taharuki kubwa ya majanga ya hali ya hewa na diplomasia ya ikolojia. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) mvua kubwa na mafuriko zimeathiri karibu watu 750,000 katika Afrika Mashariki, huku watu 234,000 wakipoteza makazi yao na zaidi ya 236 wamefariki dunia. Janga hili linaifanya Afrika iwe katika uhitaji mkubwa sana wa misaada.
Katika Pembe ya Afrika ukosefu wa utulivu unaohusiana na hali ya hewa unaongezeka na unatishia kuzorotesha maendeleo ya Afrika, kuondosha matumaini ya vijana na kuchochea wimbi kubwa la uhamiaji kwa sababu ya kuibuka kwa vurugu na ukosefu wa chakula. Kwa maana hiyo uratibu wa mataifa mengine yenye nguvu zaidi kama vile ya Ulaya na China barani Afrika utakuwa muhimu katika kupunguza hatari za mazingira magumu na tete.
Kama sehemu ya juhudi zao za ushirikiano, Ulaya na China tayari zimeanzisha mazungumzo ya kisekta kuhusu Afrika. Uratibu wa Umoja wa Ulaya na China kuhusu Afrika ni mada ya msingi kati ya mada tatu za Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na China kwenye mazungumzo ya Kimkakati ya Ngazi ya Juu. Zaidi ya hayo, waraka wa 2006 wa Tume ya Umoja wa Ulaya unaosema “Ulaya na China: Washirika wa Karibu, Majukumu yanayokua”, unaangazia maendeleo endelevu na uratibu wa misaada katika Afrika kama maeneo ya ushirikiano, pamoja na matokeo yanayotarajiwa kwa bara hili.