Uhusiano na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika umedumu kwa zaidi ya miaka 70, tangu wakati China ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi hizo za Afrika. Katika kipindi hicho, China imedhihirisha lengo lake la kujenga jamii ya binadamu yenye mustakabali pamoja kati ya China na Afrika, na kuwa mwenza wa kutegemeka wa maendeleo kwa nchi hizo. Zaidi ya hayo, mabadilishano ya watu kwa watu, kuaminiana, ushirikiano wa kuzungumzia haki na maendeleo, na kutafuta njia za maendeleo zinazofuatana na hali ya kila nchi, imekuwa lengo kuu la China katika mahusiano na nchi za Afrika.
Rais wa Comoro Azali Assoumani alihojiwa hivi karibuni na Shirika la Habari la China Xinhua, katika ikulu iliyoko Moroni, mji mkuu wa nchi hiyo. Alisema kuwa ushirikiano kati ya Visiwa vya Comoro na China ni mfano wa kuigwa, kwa kuwa umeshinda majaribu ya wakati na kutoa matokeo dhahiri.
Rais Assoumani alieleza kuwa uhusiano wa pande mbili umeshuhudia maendeleo tulivu kwa zaidi ya miaka 50. Pande hizo mbili zinaendelea kuzidisha uaminifu wa kisiasa kwa kina, na matokeo halisi yametimizwa katika maendeleo ya uchumi na jamii, huduma za afya na mabadilishano ya watu kwa watu. Aliongeza kuwa Comoro inatumaini kuendeleza ushirikiano wa kina na China, na kwa pamoja kuanzisha njia ya maendeleo ya muda mrefu kwa uhusiano wa pande hizo mbili.
Rais Assoumani alisema kuwa China ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Comoro baada ya kupata uhuru wake mwaka wa 1975, na pia nchi ya kwanza kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo. Nchi hizo mbili zimeungana mkono kwa miongo kadhaa, zikijenga uhusiano imara na uaminifu wa ngazi ya juu. Aliongeza kuwa Comoro daima imeshikilia kanuni ya China moja.
Akizungumzia Mwaka wa 2026 wa Mabadilishano ya Watu kati ya China na Afrika, Rais Assoumani alisema Taasisi ya Confucius iliyoanzishwa na China nchini Comoro inatoa fursa za thamani kwa vijana wa nchi hiyo kujifunza lugha ya Kichina. Taasisi hii inasaidia mabadilishano ya watu kwa watu, kuimarisha kuelewana kati ya pande hizo mbili, na kuongeza nguvu ya urafiki wa miongo kadhaa kati ya nchi hizo mbili.
Rais Azali alieleza kuwa mwaka wa 2026 ni maadhimisho ya miaka 51 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Comoro na China. Alikumbusha mkutano wake na Rais wa China Xi Jinping mwaka wa 2024, uliofanyika Beijing kando ya mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Katika mkutano huo, viongozi hao wawili walitangaza kupandisha daraja la uhusiano wa pande mbili kuwa uhusiano wa kimkakati.
Uhusiano kati ya Comoro na China una mwenendo unaoenea zaidi ya ushirikiano uliopo sasa, unaoashiria matarajio ya pamoja ya maendeleo ya baadaye. Kwa zaidi ya miongo mitano iliyopita, China imefanya uwekezaji mkubwa unaoonekana kwa dhahiri nchini Comoro, katika sekta za afya, elimu na miundombinu. Kando na kuisaidia Comoro kujenga uwanja wa michezo na kituo cha kuogelea kwa ajili ya Michezo ya Visiwa vya Bahari ya Hindi mwaka wa 2027, China pia imesaidia ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya El-Maarouf. Hili limekuwa msaada mkubwa katika juhudi za kupambana na magonjwa mbalimbali, ikiwemo maralia.
Kwa upande wa uchumi na biashara, ushirikiano wa pande mbili umepata maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni, hasa baada ya sera ya ushuru sifuri ya China kuanza kutekelezwa Mei moja mwaka huu kwa nchi 53 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China. Hatua hii inaonyesha kwa dhahiri lengo la China la kuzisaidia nchi za Afrika kupata maendeleo. Sera hii itazisaidia nchi za Afrika, ikiwemo Comoro, kutoa bidhaa za ubora wa juu na kuongeza mauzo katika soko kubwa la China. Kwa upande mwingine, itazipa nafasi kampuni za China kuanzisha viwanda katika nchi za Afrika kama vile Comoro, na kusaidia uzalishaji wa ndani na kuzidisha mnyororo wa thamani wa bidhaa za hapo.
Rais Azali alimalizia kwa kusema kuwa kwa sababu uhusiano kati ya Comoro na China umepandishwa daraja na kuwa uhusiano wa kimkakati wa kina, pande zote mbili zinapaswa kuweka mkazo mkubwa katika mafunzo ya vijana na mabadilishano ya watu kwa watu, ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili na raia zao.