Huu ni mwaka wa 60 tangu China na Afrika zianzishe ushirikiano katika sekta ya afya. Mwezi Januari mwaka 1963, serikali ya China ilitangaza kupeleka timu ya madaktari wake nchini Algeria, na huu ulikuwa ni mwanzo wa ushirikiano wa afya kati ya China na Afrika. Katika miaka 60 iliyopita, kutoka kupelekwa kwa timu za madaktari na juhudi za pamoja za kukabiliana na Ebola na COVID-19, hadi jengo jipya la makao makuu ya Africa CDC, ushirikiano kati ya China na Afrika katika mambo ya afya umeendelea kuimarika siku hadi siku, na kupata mafanikio mengi.
Mradi wa makao makuu ya Africa CDC ni mradi muhimu wa ushirikiano uliotangazwa kwenye Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Beijing mwaka 2018, na una umuhimu mkubwa katika kuboresha ufanisi wa kuzuia magonjwa, ufuatiliaji na mwitiko wa dharura barani Afrika. Jumla ya eneo la ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo ni mita 23,570 za mraba, ambako kuna ofisi, Idara ya kukabiliana na matukio dharura, Idara ya habari, maabara ya kibaolojia na nyumba za wataalam. Mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa wa Nigeria Charles Onunaiju ameupongeza mradi huo, akisema ukweli umethibitisha tena kwamba, China imetimiza ahadi yake, na inajenga jumuiya ya afya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja.
Mradi wa makao makuu ya Africa CDC ni sehemu ndogo tu ya mafanikio ya ushirikiano wa afya kati ya China na Afrika. Katika miaka 60 iliyopita, pande hizo mbili zimeanzisha ushirikiano wa aina na ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uratibu wa masuala ya afya ya kimataifa, kupeleka timu za madaktari, misaada ya vifaa vya matibabu, ujenzi wa miundombinu, mawasiliano ya wafanyakazi wa afya na kuandaa mafunzo.
Baada ya kupeleka timu ya kwanza ya madaktari nchini Algeria mwaka 1963, kwa nyakati tofauti China imepeleka timu za madaktari nchini Somalia, Zambia, Mali, Tanzania, Ethiopia, Madagascar na nchi nyingine za Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa, kati ya nchi 54 barani Afrika, nchi 45 zimehudumiwa na timu za madaktari za China, pia zaidi ya wafanyakazi 20,000 wa matibabu wa China wamekwenda Afrika kutoa huduma za matibabu, na wametibu zaidi ya Waafrika milioni 220.
Mwaka 2014, ugonjwa hatari wa Ebola ulilipuka Afrika Magharibi. China ilitoa msaada wa dharura kwa nchi 13 zilizoathiriwa, na zaidi ya madaktari 1,200 wa China walikuwa mstari wa mbele kuwaokoa wagonjwa.
Aidha, China pia iliisaidia Sierra Leone kujenga maabara ya kudumu ya usalama wa viumbe, kuisaidia Liberia kuanzisha kituo cha matibabu, na kutoa mafunzo husika kwa takriban wafanyakazi 13,000 wa afya wa Afrika.
Tangu kulipuka kwa janga la COVID-19, China na nchi za Afrika zimeshikamana kukabiliana na janga hilo. Mwaka 2020 wakati China ilipoanza kukabiliwa na virusi vya Corona, nchi za Afrika mara moja ziliungana na China kwa hali na mali, na viongozi wa zaidi ya nchi 50 za Afrika waliipa China salamu za pole. Wakati janga hilo lilipoanza kuenea barani Afrika, China iliisaidia Afrika kwa kadiri iwezavyo kupambana na janga hilo, na pia pande hizo mbili ziliitisha mkutano wa kilele kujadili janga hilo.
Ushirikiano wa afya kati ya China na Afrika umeendelea kwa miaka 60, na umekuwa na mafanikio mazuri. Katika enzi mpya, pande hizo mbili zitaendelea kuimarisha ushirikiano wao, ili kuharakisha ujenzi wa jumuiya ya afya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja.