Utafiti uliofanywa na idara ya magonjwa ya mfumo wa mkojo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa umebaini mitindo ya kujamiiana inaweza kusababisha uume kuvunjika.
Utafiti huo unaeleza miongoni mwa mikao hiyo ni mwanamke kukalia uume.
Utafiti huo uliochapishwa leo Jumanne, Julai 4, 2023 kwenye Jarida la kimataifa la sababu za upasuaji (International Journal of Surgery Case Reports, 108(2023)108415) umeripoti kufanya upasuaji wa kuunga uume wa kijana mwenye umri wa miaka 27 uliovunjika wakati akijamiiana na mkewe.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo, ajali hiyo siyo suala lenye kujitokeza mara kwa mara, lakini lina uwiano wa mwanamume mmoja kati ya 175,000.
Utafiti huo unadokeza kuwa, tafiti zilizofanyika katika mataifa ya Ulaya na Marekani zimeonyesha asilimia 93.3 ya ajali za uume hutokana na kujamiiana, ambacho kilikuwa chanzo cha ajali aliyopata kijana aliyetibiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Sababu inayoshika nafasi ya pili katika ajali hizo ni kujichua ikiwa ni kwa asilimia 10.
Chanzo: Mwananchi