Kama wewe wakati ule wa EAC ya zamani ulikuwa hujazaliwa, uwe unasoma basi angalao historia ya EAC kabla ya kuja na mawazo kama haya. Tunatakiwa kwanza kujua tulikotoka, mahali tulipo kabla ya kuamua tunakotaka kwenda.
Mara baada ya nchi za Uganda chini ya rais Milton Obote, Kenya (Jomo Kenyatta) na Tanzania (Julius Nyerere) kupata uhuru wake kutoka kwa muingereza ziliungana pamoja na kuunda EAC ambapo shughuli zote za kiuchumi na maendeleo za nchi hizi ziliendeshwa kwa pamoja kupitia umoja huo wa EAC. Hata pesa (currency) ilikuwa ni moja = East Africa shilling chini banki kuu moja ya EAC. Njia za mawasiliano, reli, ndege, meli, bandari na anga zote zilimilikiwa kwa pamoja. Viwanda vyote vilivyokuwa vinazalisha bidhaa mbali mbali hususani zana za kilimo, mafuta ya kula, blue band, beer na kadhalika vyote vilikuwa vinamilikiwa na EAC.
Lengo la waasisi wa umoja wa EAC lilikuwa baadaye nchi hizo tatu kuja kuungana kuwa nchi moja chini ya rais mmoja. Kilichokuja kutokea ni majonzi ambayo hatupaswi kuyasahau. Nchi ya Tanzania ilikuwa na siasa za kushoto, yaani za kijamaa, hivyo haikuwa inapendwa na nchi za magharibi. Nchi ya Uganda ilikuwa na siasa za kati. Kenya ilikuwa na siasa za kulia yaani za kibepari (capitalism) na hivyo ilikuwa kipenzi cha nchi za magharibi. Hata wazungu waliokuwa wakoloni wengi wao hawakuondoka Kenya baada ya uhuru. Wazungu hao walibaki huko wakimiliki mashamba makubwa makubwa (estates) na njia kuu za kiuchumi. Kwa kuwa wafadhili wakuu wa maendeleo ya nchi hizo za EAC walikuwa ni kutoka nchi za magharibi, walihakikisha karibu viwanda vyote vya EAC vilikuwa vinajengwa nchini Kenya - Nairobi, Mombasa etc. Ili kutupumbaza, kitu pekee kilichojengwa Tanzania ni jengo la makao makuu ya EAC pale Arusha.
Janja janja nyingi zifanyika kwenye jumuiya hiyo zikiendeshwa na upande wa Kenya walianza na kujitoa kwenye currency ya EAC. Wakaanzisha KSh na benki kuu yao. Mwaka 1977 wakati Tanzania tukigombana na Nduli Iddi Amini wa Uganda, Kenya walipora mali zote za EAC na kuvunja jumuiya hiyo. Kabla ya kuivunja walihakikisha vitu kama ndege zote za EAC, meli zote na train zote ziko nchini kwao. Hivyo tukajikuta hatuna hata kiwanda cha kutengeneza sabuni, bia, kiberiti, sindano wala cho chote kile. Yaani nchi yetu ikawa fukara wa kutupwa. Tukaanza upya from the scratch tena kwenye wakati mgumu sana kwani ilikuwa tunatoka kwenye vita dhidi ya nduli Amini iliyokuwa imetugharimu sana. Baada ya kufanya uporaji huo wa viwanda vya EAC, nchi ya Kenya ikawa ni nchi ya viwanda na soko kubwa la mazao ya viwanda hivyo likawa ni Tanzania na Uganda hadi leo.
Sasa baada ya kupitia yote hayo, tumejikongoja na kujenga viwanda, uchumi wetu unaendelea kupaa kwa spidi kubwa na karibu uchumi wetu utaupita huo wa Kenya: sasa utakuwa ni mjinga kiasi gani kuanzisha tena muungano wa aina hiyo na watu wa aina hiyo hiyo? Wanajifanya tumesahau waje watukwapue tena. Never over our dead bodies!