Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani

Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani

Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 02.




Kwakuwa muda ulikuwa umekwenda sana na kwakuwa nilikuwa mshamba wa jiji,niliona ni vema nisihangaike kuzurura huo usiku bali niendelee kusubiri na kuvumilia hadi muda ambao yule muhudumu aliniambia vyumba vingekuwa tayari kwa kukodishwa.

Sasa pale ndani kulikuwa na madumu ya maji yaliyokuwa na maji na mengine yalikuwa tupu,niliamua kuvuta dumu moja lililokuwa tupu nikakalia,wakati nimekaa nilichukua tena simu yangu nikaanza kumpigia mwenyeji wangu lakini bado hakukuwa na mafanikio,niliwaza nimpigie mama yangu lakini kwakuwa ilikuwa usiku sana sikutaka kumsumbua.Niliendelea kuvumilia pale uani huku nikishuhudia madada poa ambavyo wakibadirisha wanaume kama mvua,ilikuwa kila baada ya dakika moja kuna ambao walikuwa wanatoka vyumbani na wanaume na wengine wakiingia,ilikuwa ni kuingia na kutoka!.Kelele za muziki na mioshi ya sigara ilifanya nikalichukia lile eneo kwa ule muda lakini sikuwa na namna ilibidi nivumilie tu angalau pakuche.

Baada ya uvumilivu wa muda mrefu,ilipofika muda wa saa 9 usiku,yule muhudumu aliyeitwa Asteria alikuja akawa ameniambia ni muda sasa wa mimi kuingia kulala!.

Asteria "Kaka chumba hiki hapa nadhani unapaswa ulipie ili uweze kulala"

Mimi "Ni shilingi ngapi?"

Asteria "Ngoja nikuitie mtu anayehusika na vyumba"

Asteria " Aminaaaa"

Aliendelea " Wewe Aminaaa"

Amina "Abeeeee"

Asteria "Haya mteja wako huyu"

Amina " Anataka chumba?"

Asteria "Eeeh"

Amina "Jamani mapema yote hii!"

Asteria "Huyu kaka amesubiri sana msaidie bhana"

Amina "Haya anipe Elfu 20"

Basi kwakuwa nilikuwa nimechoka sikutaka kabisa majibizano na mtu,nilichomoa elfu 20 nikampatia huyo muhudumu kisha nikaingia zangu kwenye chumba nilichokuwa nimeonyeshwa na Asteria.

Nilipoingia mle ndani kwenye kile chumba kiukweli hakustahili mwanadamu mwenye akili timamu kulala kwasababu kilikuwa kichafu sana,uchafu ninaouzungumzia hapa si uchafu wa takataka bali ulikuwa uchafu wa taka mwili,nilikuta kondomu zimetupwa ovyo japo kulikuwa na kidastibini kidogo lakini sijui ilikuwa ni dharau au ni nini maana kondomu zilitupwa tu chini zikiwa na shahawa ndani yake,dirisha la kile chumba pia kulikuwa na pazia lililokuwa chafu kupita kiasi,nilipotazama ukutani ndiyo usiseme,nadhani ule ukuta watu waliokuwa wakiingia mle ndani walikuwa wakiiutemea mate au kuukojolea kwasababu ulikuwa umejaa michirizi ya rangi ya kahawia na njano iliyokuwa imekauka na hivyo kuufanya ukuta kuonekana mchafu.

Godoro lenyewe pia lilikuwa na kava tu llililokuwa limechakaa na lilikuwa limechoka hatari!.,kiukweli kutokana na ile harufu ya ule uchafu nilitoka ndani nikaelekea kwenye korido aliyokuwa amekaa yule dada aliyeitwa Amina.

Mimi "Sista mbona kile chumba ni kichafu!"

Amina "Kaka vyumba vyote hapa ndivyo vilivyo kama hutaki kulala unaweza kukaa nje!"

Mimi "Kwani hakuna chumba ambacho angalau ni kisafi?"

Amina "Hebu twende"

Basi yule dada alinyanyuka kwenye kiti akawa ametangulia na mimi nikamfuata nyuma kama mtu na mke wake!.Alianza kufungua chumba kimoja baada ya kingine vile ambavyo havikuwa na watu.

Amina "Je hiki kitakufaa?"

Nilikisogelea kile chumba na kutazama kwa ndani ili nione kama kitafaa.

Mimi "Angalau hiki"

Amina "Sawa"


Niliingia ndani ya kile chumba nikafunga mlango kisha nikakaa zangu kitandani nikiendelea kukitazama.Kile chumba hakikuwa na tofauti kubwa na kile cha kwanza,sema hiki cha pili angalau sikukuta kondomu chini na godoro lake halikuchoka sana kama lile la kwanza,japo kulikuwa na kiharufu fulani cha kukera lakini sikuwa na namna ilibidi nivumilie pakuche!.Nilivua viatu kisha nikapanda kitandani kujiegesha,mle ndani hakukuwa na shuka wala taulo,mimi niliamua kulala na nguo zangu angalau zikanisitiri na kiubaridi kile cha Alfajjri.

Mida ya saa 3 asubuhi nilishitushwa na kelele za watu wakiwa wanafokeana hapo nje,niliamka zangu nikavaa viatu kisha nikachukua begi langu nikalitia mgongoni nikatoka nje,nilipotoka nje nikawakuta kina dada wawili wakiwa wanatambiana kwa matusi kedekede!,niliwashangaa namna walivyokuwa wakiporomosheana matusi ya nguoni bila aibu,sikutaka kupoteza muda kwenye mambo ya kijinga,niliondoka zangu kuelekea nje nione nitaianza vipi siku kwenye hili jiji ambalo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika!.

Nilichukua simu yangu nikaanza kumtafuta mwenyeji wangu lakini simu haikupatikana hewani kabisa,kiukweli nilibaki najiuliza maswali mengi sana ambayo hayakuwa na majibu.Jamaa ndiye aliyefanya mimi kuondoka Tarime na kuja Dar es salaam na wakati nikiwa kwenye gari tulikuwa tukiwasiliana naye kutwa nzima,sasa sikufahamu ni kitu gani ambacho kilimpata hadi asipatikane kwenye simu.Niliamua kumtafuta mama yangu na kumueleza kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Mama "Sasa utafanyaje?"

Aliendelea "Ndugu wa upande wa baba zenu niliwahi kuwaambia huwa wanatabia za kijinga lakini huwa hamnisikii !"

Mama "Sasa kama mliongea na akajua unaenda kwanini hapatikani kwenye simu?"


Aliendelea "Mpigie mjomba wako Nicholaus"

Mimi " Sinaga namba yake mimi"


Mama "Hebu subiri"

Basi baada ya mazungumzo ya muda mfupi na mama yangu alikata simu,Mama yangu alishangaa sana mimi kwenda Dar es salaam bila taarifa na kibaya zaidi alikuwaga hapendi kabisa sisi wanae kwenda upande wa baba zetu kwasababu hawakuwaga na msaada zaidi ya masimango na manyanyaso.

Baada ya dakika kama 10 kuna namba ngeni ilinipigia simu ikabidi nipokee kwa uharaka na nilidhani uenda atakuwa jamaa ametumia namba nyingine.

Sauti ya Kiume "Wewe uko wapi?"

Mimi "Nani mwenzangu?"

Sauti ya kiume "Mjomba wako Nico hapa"

Mimi " Ooh Anko shikamoo!"

Anko Nico "Kwahiyo sikuhizi umesahau kikurya hadi uniamkie kiswahili?"

Mimi "Hapana Anko"

Anko Nico "Haya bhana"

Aliendelea "Wewe unakujaje mjini bila taarifa?,au unadhani hapa ni Mogabiri?"

Mimi "Niliwasiliana na Kileri Anko sema nilipofika nimejaribu kumpigia hapatikani!"

Anko Nico "Huyo Kileri ni nani?"

Mimi "Ni mtoto wa Ba'mkubwa"

Anko Nico "Hapa ni mjini hebu acha ujuaji wa kijinga,sema uko maeneo gani nitume mtu aje akachukue"

Basi nilisogea eneo moja nikamuuliza jamaa mmoja pale ni wapi akawa ameniambia ni Ubungo Maziwa,ndipo nilimpa Anko Nico taarifa.

Anko Nico "Uliza mtu yeyote hapo jirani akuonyeshe jengo la Ubungo Plaza lilipo na uende hapo ukasubiri kuna mtu namtuma anakuja kukuchukua"

Mimi "Sawa anko"


Niliuliza watu bahati nzuri nikawa nimeonyeshwa jengo la Ubungo Plaza na nikaliona kwakuwa lilikuwa refu,nilitembea mdogo mdogo huku nikiwa makini sana na begi langu mgongoni asije kibaka yeyote akanikwapua akakimbia.Nilipofika hapo Ubungo Plaza nilimpigia Anko Nico simu kisha akawa ameniambia kuna mtu amempatia namba yangu ya simu akifika hapo atanipigia simu.


Itaendelea...

Muendelezo soma Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani
Umughaka ktk ubora wake
 
Back
Top Bottom