Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 13.
Ile sauti ya mtetemo iliendelea sana kana kwamba hicho kitu kilichokuwa humo chumbani kilikuwa kimekasirishwa,nilisimama taratibu nikatembea kwa kunyata hadi kwenye mlango wa kile chumba,nilipofika kwakuwa muda wa kukifungua ulikuwa bado,nilitegea sikio kwa makini kusikiliza kilikuwa ni kitu gani,nilitulia kimya kabisa lakini ile sauti ya mtetemo ilikoma,niliamua tena kunyata na kurudi sebuleni.
Muda wa kufungua ule mlango ulipowadia nilinyanyuka na kwenda kuufungua,sasa nilipofungua ule mlango kama kawaida niliuacha wazi kisha nikawasha taa za nje nikatoka zangu ndani kuelekea nje.Siku hiyo sikutaka kabisa kutoka kwenda kula kwasababu nilikuwa nimekula muda siyo mrefu hivyo nikawa nimeshiba,kwakuwa bado ilikuwa mapema,niliona nifungue ile gari nikae ndani nitulie hadi nitakapopitiwa na usingizi,nilifungua vioo vya mbele vya ile gari upepo ukaanza kuingia ndani lakini nilipoona mbu wanazidi kuingia kwa kasi nilivifunga kisha nikawasha AC nikaendelea kula upepo.
Ilipofika mida ya saa 3 usiku kukiwa kumetulia,nilianza kusikia sauti ya kitu ambacho sikukielewa kilikuwa ni kitu gani kikiwa kinatafuna kwa sauti na miguno kama ya nguruwe,ile sauti ilikuwa inasikika kwa nguvu sana kiasi kwamba ikabidi nifungue mlango wa gari na kushuka,baada ya kutoka kwenye gari nilisimama kando ili niweze kuisikia ile sauti vizuri.Hali ile hakuna mwanadamu mwenye moyo ambaye asingeiogopa,mimi pamoja na ujasiri wangu wa kikurya lakini ilifika sehemu nikawa naogopa sana lakini niliendelea kuwa mvumilivu na kumdhibitishia Ally Mpemba ya kwamba mimi ni mwanaume na ni mwaminifu,hivyo mategemeo yangu yalikuwa ni ipo siku atanipa fedha au sehemu ya mali zake kutokana na uaminifu wangu kwake.
Ile sauti ilipozidi,nilisogea hadi pale mlangoni kwa kunyata kisha nikawa nasikiliza kilikuwa ni kiumbe wa aina gani aliyekuwa mle ndani,kiukweli ilikuwa ngumu kutambua kama alikuwa mwanadamu au mnyama,kwasababu nilichokuwa najiuliza,kama ni mwanadamu anawezaje kutafuna kwa kasi kiasi kile na miguno kama ya nguruwe?
Kwa watu mliofuga nguruwe au mlioishi na nguruwe nadhani hapa mtakuwa mnanielewa,kile kitu kilichokuwa humo ndani kilikuwa kinatafuna na kuguna kwa utamu kama nguruwe anapokuwa anakula.
Pia kama ni mnyama,Je alikuwa ni mnyama gani?,kiukweli niliendelea kujiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu,niliona nijiondokee zangu nirudi kwenye gari kutulia,nilipitiwa na usingizi nikajikuta naamka saa 12 baada ya kusikia milio ya magari huko nje,niliamka haraka na kwenda kuufungua ule mlango na kuzama ndani,nilipofika ndani niliwasha taa za pale sebuleni na kukuta kile kitambaa kilichokuwa pale juu ya meza kimetupwa chini na nilipoangalia chini nikakuta kuna ute ute mzito kama ambao hutoa ng'ombe akiwa anatafuna nyasi,zile kabeji pamoja na mboga za majani sikuzikuta hata kipande tu,kiukweli niliingiwa na hofu sana na sikutaka kusubiri nilielekea moja kwa moja mpaka kwenye kile chumba na kukifunga.Nilipokifunga kile chumba angalau sasa moyo wangu ulitulia,niliingia jikoni nikachukua dekio (Mop) nikaenda kusafisha ule ute mzito kisha kile kitambaa nikakirudisha jikoni kama kawaida.
Baada ya kumaliza lile zoezi,nilitoka nje nikafunga mlango kisha kuelekea bombani kunawa,nilipomaliza kunawa uso na kusukutua nilirudi kwenye gari kusikilizia hadi mida ya saa 2 ili niondoke niingie Kkoo kufanya kazi yangu ya usajili.Baada ya muda kufika niliondoka nikaelekea Buguruni ofisini ambako vikao vilikuwa vinafanyika kila siku na ilikuwa ni lazima kuhudhuria,baada ya kumaliza kikao nilichukua box la line kisha nikaondoka zangu Kkoo,sasa wakati nipo kariakoo napiga kazi,Ally Mpemba alinipigia simu na kutaka nimpatie taarifa za usiku.
Ally Mpemba "Assalam aleykum"
Mimi "Alekom salam "
Ally Mpemba "Wajionaje na hali?"
Mimi "Niko vema kabisa kaka"
Ally Mpemba "Mambo yalienda vyema?"
Mimi "Ndiyo kaka hakuna kilichoharibika"
Ally Mpemba "Hakukuwa na usumbufu kama wa jana?"
Mimi "Hapana kaka"
Nilitaka nimuulize jamaa ni kitu gani kilikuwa mle ndani lakini nilikuwa nasita sana na niliona ningemuuliza uenda ningeharibu uhusiano wetu ambao tayari ushaanza kuwa mkubwa,niliamua nipige kimya ili mambo mengine mazuri yaliyokuwa mbele yangu nisiyazibe.
Ally Mpemba "Sasa utamwambia Farah akupe elfu 50 na utafanya kama ambavyo ulifanya jana"
Mimi "Sawa kaka"
Baada ya mazungumzo jamaa akawa amekata ile simu.Ilipofika mida ya saa 10 Alasiri,niliamua nifunge nirudishe vifaa vyangu vya kazi mahali ambapo nimekuwa nikivihifadhi,nilirudi hadi dukani pale nikamwambia yule sister Farah anipatie kiasi cha fedha kama ambavyo Ally Mpemba alikuwa ameniambia.
Farah "Mbona sikuhizi wawahi sana kufunga!"
Mimi "Hata muda wa usajili umebaki mchache na kuna mahali inabidi niwahi"
Farah "Ooh ok nambie"
Mimi "Brother Ally aliniambia unipatie elfu 50"
Farah "Ally kaka yangu au Ally yupi!?"
Mimi "Yes,brother Ally"
Farah "Mbona hajaniambia "
Aliendelea "Ngoja nimtafute nithibitishe"
Baada ya kumpigia Ally Mpemba na kumpata hewani walikuwa wakiongea lakini yule demu nikama alikuwa akimuuliza Ally mimi na yeye tunabiashara gani kwasababu jana alitoa elfu 50 akanipa na leo tena anatoa elfu 50 kunipatia,sikujua Ally Mpemba alimjibu kitu gani,alichukua elfu 50 akanipatia kisha mimi nikaondoka kuelekea sokoni kununua bidhaa kama ambazo nilinunua jana,maelekezo yalikuwa ni yale yale.
Kiukweli kwa muda huo nilikuwa napata sana hela kwasababu kununua mahitaji yote yale nilikuwa natumia chini ya elfu 20 na elfu 30 iliyokuwa inabaki ilikuwa yangu na Ally Mpemba hakuwahi kuiulizia kabisa,kila siku nilikuwa napewa elfu 50 kwa ajili ya manunuzi.
Kama kawaida niponunua bidhaa nilirudi hadi nyumbani Kwa Ally Mpemba na kuyaweka kama ambavyo nilikuwa nimeelekezwa.Ilipofika jioni muda wa kufungua kile chumba,niliamua kufungua pazia la pale sebuleni kisha nikawasha taa,lengo langu ilikuwa ni kuhakikisha siku hiyo nakiona kile kiumbe ambacho sikukifahamu kilikuwa kiumbe cha aina gani!;baada ya kufungua pazia na kuwasha taa,nilienda kuufungua ule mlango na kuacha wazi kisha nikatoka nje.
Niliamua kukaa kando ya lile dirisha la pale sebuleni huku nikiwa na shauku kubwa ya kuona ni kitu gani kilikuwa mle ndani,ilipofika mida ya saa 2 usiku,nilitoka nje nikaelekea kununua chips na soda kisha nikawahi kurudi,nilipofika breki ya kwanza ilikuwa ni kwenye dirisha la pale sebuleni,niliangalia kwa umakini na ndipo niliona zile kabeji na mboga za majani uilikuwa hazijaliwa,hivyo nikaa pale pembeni nikaanza kula huku nikisubiri nione ni kitu gani kilikuwa mle ndani.
Nilikaa sana pale chini hadi mida ya saa 5 usiku lakini kila nikichungulia hakukuwa na dalili ya kitu chochote,niliamua kufungua mlango na kisha kuingia ndani ili nikafunge yale mapazia na kuzima taa,nilipomaliza nilitoka nje kisha nikakaa pale mlangoni na kusikiliza,ndipo haukupita muda nikaanza kusikia utafunaji wa ovyo na papara ukiendelea kama kawaida,niliondoka nikaingia kwenye gari kwenda kulala kama kawaida huku kile kiumbe kikiendelea na utafunaji wake wa sauti kama nguruwe.
Asubuhi kama kawaida niliingia ndani nikafunga ule mlango kisha nikaanza kufanya usafi pale sebuleni kama kawaida,nilipomaliza niliondoka kuelekea kazini kama kawaida.
Sasa ilipofika mida ya saa 3 asubuhi nikiwa tu ndo nimeanza kazi,alinipigia simu Ally Mpemba.
Ally Mpemba "Kaka salama?"
Mimi "Salama kabisa,vipi wewe huko?"
Ally Mpemba "Huku naendelea vema ila narudi wiki ijayo"
Mimi "Sawa kaka,nambie"
Ally Mpemba "Kuna mtu nimempa namba yako atakupigia simu ana mzigo wangu utaenda atakupatia"
Mimi "Sawa kaka ni mzigo gani?"
Ally Mpemba "Ni pesa,hakikisha akikupatia utanipelekea Benki Crdb,nitakutumia vielelezo"
Mimi "Sawa kaka hakuna tatizo"
Ally Mpemba "Pia nimemwambia Farah kuna pesa atakupatia,utachukua utanunua mahitaji yale kama kawaida na itakayobaki utatumia "
Mimi "Nashukuru sana Kaka Ally"
Ally Mpemba "wala huna haja ya kunishukuru,mimi ndiye ninapaswa kukushukuru "
Aliendelea "Nitakufanyia mambo makubwa sana kwa uaminifu wako"
Mimi "Sawa kaka nitashukuru sana"
Baada ya mazungumzo yale mafupi Ally Mpemba akawa amekata simu.
Ilipofika mida ya saa 7 mchana,kuna namba ngeni ikawa imenipigia simu,ilikuwa ni sauti ya mwanamke ambaye alijitambulisha kama Warda.
Mimi "Ndiye mimi"
Warda "Ally kaniambia kuna mzigo wake nikupatie,sijui nakupataje?"
Mimi "Wewe uko wapi?"
Warda "Njoo hapa mtaa wa mkunguni ukifika uniambie"
Mimi "Sawa nakuja muda si mrefu"
Mimi "Aunt Farah samahani naomba unitazamie hapo narudi mara moja"
Farah "Kwani ndo unafunga?"
Mimi "Hapana,kuna mahali nafika mara moja ila nawahi kurudi"
Farah "Ooh sawa kuna hela Ally ameniambia nikupatie,hivyo ukitaka kuondoka utaniambia"
Mimi "Sawa nawahi kurudi"
Itaendelea........