*UNDANI KIFO CHA SOKOINE*
WAZIRI Mkuu (sasa ni marehemu) Edward Moringe Sokoine alikuwa Dodoma kwenye kikao cha Bunge akiwa ni kiongozi wa shughuli za serikali na alimaliza kikao chake Aprili 11, 1984.
Aliandaliwa usafiri wa ndege ili asafiri na ujumbe wake wakati wa kurejea Dar es Salaam kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa lakini alikataa.
“Safari hii sitaki kurudi Dar es Salaam kwa ndege, nataka kurudi kwa gari ili nione hali ya mazao ya wakulima njiani,” alikaririwa afisa mmoja wa Ikulu akimkariri Waziri Mkuu Sokoine mara baada ya kujulishwa habari ya usafiri wa kumrejesha Dar.
Aprili 12, 1984 msafara wake ulianza akitokea Dodoma huku ukisindikizwa na magari ya polisi na wana usalama wa taifa.
Msafara wake mchana ulipofika eneo la Wami mkoani Morogoro, jirani na palipojengwa makao makuu ya sasa ya Wilaya ya Mvomero, gari yake ilipata ajali kwa kugongwa na gari lingine aina ya Toyota Land Cruiser.
Sokoine alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, madaktari walithibitisha kifo chake.
Rais (wa wakati huo), Mwalimu Julius Kambarage Nyerere siku hiyo majira ya jioni alilitangazia taifa kifo cha waziri mkuu wao. Mwalimu Nyerere, alishindwa kuhutubia kutokana na majonzi aliyokuwa nayo.
Miaka kumi baada ya kifo chache, daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sokoine baada ya kifo, aliweka wazi taarifa ya chanzo cha kifo chake.
Sehemu ya taarifa hiyo ilisema kuwa baada ya ajali, Sokoine alivunjika shingo ambayo ilisababisha kubana mishipa ya fahamu (spinal cord) ambayo ilikata mawasiliano kati ya ubongo na sehemu nyingine za mwili.
Kabla ya kifo chake, Sokoine alikuwa pia Mbunge wa Jimbo la Monduli na mwili wake ulizikwa huko kwa heshima zote za kiserikali, japokuwa mila za Kimasai pia zilipewa nafasi katika mazishi hayo.
Mahali alipopatia ajali Sokoine mara baada ya ajali hiyo panaitwa Wami Sokoine na pamejengwa mnara wa kumbukumbu ya kifo chake.
Maadhimisho ya miaka 34 ya kifo cha Hayati Edward Sokoine yanatarajia kufanyika April 12 Moringe Juu, Arusha. Kutakuwa na ibada maalum pamoja na fursa ya kutembelea kaburi la Sokoine. Tuungane kwa pamoja. Karibuni sana.