Je ni imani za kweli kuwa kitovu cha mtoto mchanga kikiangukia uume huyo mtoto atakua hasimamishi?
Wajuvi wa mambo tunaomba mtusaidie.
Wajuvi wa mambo tunaomba mtusaidie.
- Tunachokijua
- Tohara ni upasuaji mdogo unaofanyika ili kuondoa ngozi ya mbele inayofunika sehemu za siri za mwanamme.
Asili ya utamaduni huu ni imani za kidini, ambazo baadae zilithibitishwa kuwa na faida kiafya. Leo, watu hutahiri kwa sababu za kiafya, au za kidini.
Mwanamme huzaliwa na ngozi inayofunika kichwa cha sehemu zake za siri hivyo kupitia tohara, ngozi hii huondolewa kwa kufanya upasuaji mdogo usiotumia muda mrefu sana, kati ya dakika 15-30. Kwa sababu za kiusalama, pamoja na kuhakikisha kuwa tendo hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa, ni vizuri kama likifanywa hospitalini.
Madai ya kitovu kufanya uume usisimane
Madai haya yamekuwepo kwa miaka mingi. Mathalani, blog moja imewahi kuchapisha makala inayohusu suala hili mwaka 2012.
Kwenye Jukwaa la JamiiForums, mada hii imeanza kujadiliwa kabla ya mwaka huo. Mei 20, 2008, mtumiaji mmoja wa jukwaa hili aliweka andiko lenye kichwa cha habari "UHANITHI baada ya Kitovu cha Mtoto kukatika na kudondokea Sehemu zake za Siri".
Pamoja na mambo mengine, mdau huyu alikiri kuwahi kusikia jambo hili na aliweka andiko lake ili kupata uthibitisho wa kitaalamu.
Pia, mitandao mingine kama Twitter imewahi kupata aina hii ya mjadala. Machi 29, 2021, ReganTesha_ alihoji ukweli wa nadharia hii.
Uthibitisho wa kisayansi
JamiiForums imezungumza na wataalam wa afya wenye ujuzi wa kutosha kuhusiana na afya ya binadamu na kufanya tohara. Katika mahojiano hayo, tumebaini mambo yafuatayo;
- Jambo hili halina uthibitisho wa kisayansi.
- Kitovu huwa na kazi kubwa ya kusafirisha hewa na virutubisho kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa takamwili kutoka kwa mtoto.
- Baada ya kuzaliwa, kitovu hukatwa. Mtoto huanza kujitegemea mwenyewe kama kiumbe kilichokamilika.
- Kutokusimama kwa umme (uhanithi) husababishwa na changamoto za kiafya anazokuwa nazo mwanaume ikiwemo kuathirika au kuharibika kwa mishipa ya fahamu ya uume, changamoto kwenye homoni za mwili, kupungua kwa msukumo wa damu kwenye uume, changamoto za afya ya akili na magonjwa sugu.
JamiiForums haikuishia kwenye kufahamu uhusiano wa kitovu na uhanithi pekee, bali imefuatilia pia kufahamu chanzo cha nadharia hii.
Wataalamu wa afya wamesisitiza kuwa pengine nadharia hii ilianzishwa ili kuweka mkazo kwenye kutunza usalama na usafi wa kitovu cha mtoto ambacho ni sehemu muhimu ya uhai.
Baada ya kukatwa, kitovu hiki hubaki na kidonda kinachoweza kumfanya mtoto apatwe na maambukizi makubwa yanayoweza hata kumfanya apoteze uhai ikiwa hakitatunzwa vizuri.
Utafiti uliofanyika nchini Kenya wenye kichwa cha habari "Association between umbilical cord hygiene and neonatal sepsis among neonates presenting to a primary care facility in Nairobi County, Kenya: a case-control study" wa PK Moraa (2019) unadai kuwa kutunza usafi wa kitovu cha watoto hupunguza maambukizi makali yanayoweza kupoteza uhai wa mtoto kwa zaidi ya 67%.
Maambukizi ya aina hii hutokea zaidi kwa watoto walio na umri chini ya siku 28.
Hata hivyo, pamoja na kukosa ukweli kisanyansi, hii ni mojawapo ya mila iliyosaidia wanawake wengi kuwa waangalifu kwenye kutunza kitovu cha mtoto hivyo kupunguza maambukizi yanayohusiana na kitovu ambayo ni chanzo kikubwa cha magonjwa hatari ya watoto yanayoanzia kwenye kitovu (cord sepsis na septicaemia), magonjwa yanaongoza kwa kuua vichanga.
Uthibitisho wa mdau wa JamiiForums
Uthibitisho mwingine wa madai haya kutokuwa na ukweli yanatolewa na mdau wa JamiiForums, aliyeshiriki katika mjadala wa Mei 20, 2008 kuhusu suala hili. Alisema;
"Hakuna lolote hapo because me mwanangu aliangukiwa kukawa na bonge la discussion kuhusiana na hiyo imani, ikanibidi nitafute msaada wa kidaktari ila wote walisema hakuna uhusiano wowote kati ya kipisi cha kitovu na udindaji wa dogo, rite this moment mtoto wangu hana shida hapo kabisa"
Pamoja na uthibitisho huu, JamiiForums inawaasa wazazi kuzingatia usafi wa kitovu cha mtoto baada ya kujifungua ili kumkinga dhidi ya magonjwa hatari yanayoweza kumfanya apoteze maisha.