[h=2]Vikwazo vya uzazi wa mpango vinavyoikabili jamii yetu[/h]
WANAWAKE wengi nchini wana elimu ya kutosha kuhusu uzazi wa mpango. Wanajua kutokana kwa kuambiwa na rafiki zao, kujifunza kwa wazazi, kliniki na kwa kusoma kutoka vitabuni na mahali pengine.
Wanajifunza kwamba uzazi si kitu cha bahati mbaya. Kinasababishwa. Baadhi ya akina mama hawa wanataka kuepuka mimba zisizotarajiwa, wanaona hali mbaya ya uchumi, kipato duni na kazi ngumu ya kulea watoto wengi.
Wanawake wengi wanajifunza aina mbalimbali za kupanga uzazi, mfano za vijiti, vitanzi, sindano, kondomu, vidonge na nyingine za asili za kufuata kalenda ya mwili ama wenzi wao wa kiume kuishia nje. Ukizungumza na wanawake wengi, wasomi na wasio wasomi, wanasema kila njia ni nzuri kwa mtumiaji maadam ameona inafaa. Kwani njia moja inaweza kumfaa na mwingine isimfae. Hata hivyo, wapo baadhi ya watafiti wanaosema kwamba njia nyingi za uzazi wa mpango mbali na zile za asili zina madhara haya na yale. Katika kampeni yao ya kupanga uzazi, wanawake wengi wanapambana na vigingi viwili vikubwa.
Kimoja ni uhaba wa wataalamu wa kuelekeza utumiaji wa njia salama za uzazi wa mpango na kuadimika kwa njia hizo za kupanga uzazi. Kutokana na vikwazo hivyo, wanawake wengi wamejikuta ama kulazimika kutumia njia za uzazi ambazo hawazipendi, ama zisizo salama na zenye kuwaletea madhara.
Wengine wamejikuta, wakitumia njia ambazo, wanashindwa kuzifuata na hatimaye wanatumbukia kwenye mimba zisizotarajiwa na kuamua kuzitoa.
Bingwa wa Masuala ya Wanawake katika Hospitali, anasema, wanawake wengi wamekuwa wakishindwa kufuata mpango wa uzazi kutokana na
kukosa huduma wanazotaka au kukosa wataalamu wa kuelekeza njia mbalimbali za uzazi.

wanawake wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango wameanza kuongezeka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Anasema ukizungumza na wanawake, wanakubali kwamba wanatumia njia mbalimbali za kuzuia mimba, kupanga uzazi na kuzuia maradhi kwa lengo la kupata muda wa kutosha kufanya shughuli za ujasiriamali.
zahanati nyingi hazitoi huduma zote za kupanga uzazi na kwamba zipo baadhi zinatoa njia moja tu kati ya hizi; sindano, vidonge, vitanzi, vijiti, kondomu na kalenda ya mwili.
Ukienda vijijini/kijijini, kutokana na kukosekana kwa mtaalamu katika zahanati nyingi karibu zinashindwa kuendelea na njia yake ya sindano, watu wengi wanamua kuchukua vidonge tena pasipo maelekezo ya mtaalamu.
maeneo mengi au watu wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu vidonge, wakati mwingine alisahau kutumia vidonge, akajikuta amepata mimba ambayo hakupangilia. Matatizo kama hayo yanawakumba wanawake wengi, japo idadi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati ni nyingi nchini, lakini hakuna huduma ya kuaminika ya uzazi wa mpango.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii za 2006 zinaonesha kwamba kulikuwa na hospitali 219, vituo vya afya 481 na zahanati 4,679, ambavyo vingi vina uhaba wa wataalamu wa afya na hasa inayohusu uzazi. Kumekuwa na matatizo katika hospitali na vituo vingi vya afya na hata zahanati za kupata huduma hizo, kutokana na wanawake wengi kukosa uchaguzi wa aina ya njia wanazoona zinawafaa katika kupanga uzazi.
Wanawake wamekuwa wakifika hospitalini, vituo vya afya au zahanati na kulazimishwa kutumia sindano au kondomu, wakati wao wamezoea vijiti au vidonge.
Binti mmoja nilimuuliza anasema, alipoenda zahanati moja aliambiwa kuwa mtaalamu wa kuweka vijiti amesafiri hivyo asubiri hadi atakaporudi au
atumie vidonge. Kwa kupatikana huduma za vidonge tu, Binti huyo alikuwa na wakati mgumu na hivyo kwa hofu ya kupata ujauzito asiopangilia,
akaamua kuanza kutumia vidonge ambavyo haikuwa chaguo lake
Hayakuwa mapenzi yangu kabisa kutumia vidonge lakini kwa sababu ya kukosa mtaalamu wa kuniwekea vijiti, nikalazimika kutumia, anasema Binti huyo.
Binti huyu anakosa mtaalamu wa kumweka vijiti, hali ikoje mikoani, wilayani na vijijini ambako hakuna wahudumu wa kutosha?
Jibu ni kwamba wanawake wengi hawana uamuzi wa kuchagua njia za kupanga uzazi, wanapewa huduma zilizopo au vinginevyo
wapate mimba ambazo hawajapanga.

Mama mmoja nae niliongea nae katika kliniki moja, nilipomhojiwa ni njia gani anatumia katika kupanga uzazi, anasema alijaribukutumia kitanzi, lakini siku alipokwenda kliniki akaambiwa muuguzi wa kuweka kitanzi amehamishwa.
Kutokana na pilikapilika zake za ujasiriamali, akarudi nyumbani bila kupata huduma, na haukupita muda kwa sababu hakujua vizuri njia ya kufuata kalenda, akadaka mimba, akajifungua mtoto wa tano, jambo ambalo linampa wakati mgumu kulea kutokana na
kipato chake duni cha kuuza vitumbua.
Serikali ifanye kila linaloweza kuhakikisha kila zahanati, kituo cha afya na hospitali wanakuwa na wataalamu wa masuala ya uzazi wa
mpango.
Mama mmoja alipata tatizo kubwa kutokana na mumewe kutotaka kusikia kabisa habari ya mpango wa uzazi, hivyo akawa akidunga sindano
kwa siri. Siku moja alipoenda hospitalini, akakosa sindano, akaambiwa zipo tu kondomu, jambo hilo likawa gumu kwake kwani mumewe asingemwelewa kumwambia watumie kondomu. Hivyo akarudi amejiinamia kwamba atakwenda kupata mimba ambayo hakupanga apate wakati huo, na kweli ikawa hivyo na sasa analea moto ambaye hakumpangilia.
Kutokana na wanaume wengi kuwa wapinzani wa mpango wa uzazi, wakati umefika kuhimiza kampeni ya kuwapa elimu na umuhimu wa uzazi wa mpango katika kulea familia.
Mama huyu ni mmoja wa wanawake wengi, ambao wanaficha kadi zao hospitalini ili wanaume wao wasijue kuwa wanafuata mpango wa uzazi, na wengine wanasahau tarehe na kujishtukia wamepata mimba zisizotarajiwa.
Wanaume wanatakiwa kubadili mtazamo hasi na kuwasindikiza wanawake zao kwenda nao kliniki kujifunza elimu ya uzazi wa mpango.
Utoaji mimba kiholela umekithiri kutokana na wanawake wengi kupata mimba wasizotarajia, ambazo zinachangiwa na uhaba wa wahudumu na ukosefu wa elimu ya uzazi, uhaba wa huduma za uzazi wa mpango na ugumu wa wapenzi wao wa kiume.
Idadi ya wanawake wanaofika mahospitalini hapo baada ya kutoa mimba kienyeji ni kubwa, jambo ambalo linachangia wengine kupoteza maisha.
Kama elimu na matumizi ya vidhibiti mimba ingefuatwa, utaoji mimba nao ungepungua ama kuisha kabisa.

uhaba wa watalaamu wa huduma za mpango wa uzazi katika maeneo ya vijijini unachangia kwa kiasi kikubwa mimba
zisizotarajiwa. Upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango katika maeneo wanayoishi ni shida, wakati mwingine wanatakiwa kufuata umbali wa kilometa
kadhaa kwenda wilayani au mahali pengine, kufuata huduma hizo. Kutokana na uhaba wa wataalamu wa huduma za uzazi, kumeibua mimba za
utotoni na matatizo mengine katika jamii yakiwamo ya kuongezeka watoto wa mitaani, yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ambao wazazi wao
wanawatelekeza baada ya kuwazaa.
Vifo vya watoto na wanawake wajawazito, vimekuwa havipungui kwa kasi inayotakiwakutokana na wanawake wengi kuishia kuharibu mimba hizo na wakati mwingine wao wenyewe kufa.
Elimu ya uzazi wa mpango kwa kila Mtanzania ni muhimu kwani itasaidia kujua umuhimu wa wanawake kupanga aina ya uzazi na idadi
na watoto anaotaka.