Ni dhahiri unaweza kujifunza kutoka kwa Messi kuwa kuna wakati kwenye maisha tunazingatia mambo fulani zaidi na kuyasahau yale ya msingi. Mambo kama vile kazi, miradi na pesa vina nafasi yake lakini havitakiwi kuchukua nafasi ya ndugu, jamaa, marafiki na familia.
Nimeshuhudia watu wanaojiita ni wajasiriamali wakiangamiza ndoa na familia zao kwa kukosa muda wa kuwa karibu au kuzihudumia. Ni lazima ubainishe mambo ya muhimu zaidi kwenye maisha yako ili uwe mwenye tija zaidi.
Messi anafahamu madhara ya ubinafsi kwenye maisha na soka. Ni dhahiri kuwa watu wengi hawafanikiwi kwani hutazama mambo yao wenyewe. Nimeshuhudia biashara na miradi mingi ikifa kutokana na ubinafsi. Kwa mfano watu wanapatana kuanzisha mradi au biashara kwa pamoja, baada ya kupata mafanikio kila mtu anakimbia kuanzisha ya kwake na hatimaye zote zinakufa.
Ni wazi kuwa ni lazima kujikita kwenye malengo yenu kama kundi au timu ili muweze kufanikiwa. Siku zote jiwekee kauli mbiu hii “Mwingine kwanza, mimi baadaye”.
“Wakati mwingine ni lazima ukubali kuwa huwezi kushinda wakati wote”
Lionel Messi
Lionel anatukumbusha kuwa hakuna mtu au watu wanaoweza kushinda kila wakati. Wakati mwingine tunaendelea na kujifunza kutokana na kushindwa. Haupaswi kujisikia vibaya na kukata tamaa pale unaposhindwa. Hii ni sehemu ya mzunguko; jua haliwezi kuwaka siku zote, ni lazima mvua inyeshe pia.
Unaposhinda fanya bidii kuendelea mbele. Unaposhindwa pia, fanya bidii zaidi kuendelea mbele huku ukijifunza kutokana na makosa.
9. Uaminifu
Hivi leo uaminifu ni bidhaa adimu ambayo hauwezi kuipata kirahisi. Ni dhahiri kuwa kuna somo kubwa la kujifunza kutoka kwa Lionel Messi kuhusu uaminifu aliouonyesha kwa klabu yake ya Barcelona. Messi amekuwa akichezea klabu ya Barcelona zaidi ya miaka 12 licha ya kuitwa na klabu nyingine kwa ahadi za fedha nyingi. Ni wazi kuwa Messi alifahamu kuwa uaminifu na upendo wa dhati kwa klabu yake ungemjenga zaidi kisoka kuliko kuhamahama.