Mbunge huyo alitoa kauli hiyo alipoomba mwongozo akitumia kanuni ya 47 kuhusu jambo la dharura bungeni na alipopewa nafasi alisema amekuwa akiwasiliana na Serikali lakini hakuna kinachoendelea na wahusika wamekaa kimya. Hoja yake ilimuinua Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyesema tatizo la maji ni la nchi nzima na kwamba halitakiwi kupuuzwa na kutaka wananchi watendewe haki maeneo yote.
Licha ya Waziri Mhagama kuagiza mawaziri wa Maji, Nishati na Fedha kukutana mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa, jambo hilo liliendelea kutikia Bunge
Mbunge wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia naye alieleza ukubwa wa tatizo hilo katika jimbo lake huku mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akieleza jinsi anavyojibiwa kisiasa na waziri Kamwelwe kuhusu maji.
Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alimuweka Mpina katika wakati mgumu baada ya kusema amekuwa na kiburi na kumtaka aache kwa kuwa anawaumiza wafugaji, akitolea mfano kamatakamata ya mifugo.
Nape alisema hakuna lililofanyika kwa wafugaji tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulipomalizika na kwamba kila wakati Serikali inafanya kazi ya zimamoto badala ya kujipanga na kushughulikia matatizo ya wananchi kikamilifu.
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salum Hussein, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama yai viza ambalo lina matumizi mazuri kwa wanaolitumia lakini likikosewa linanuka.
Mchungaji Msigwa naye aligusia wizara hiyo, kubainisha kuwa Kamati ya Maliasili imepokea malalamiko kutokana na hatua ya waziri Kigwangalla kufuta vitalu vya uwindaji.