Alichokisema shahidi ni kwamba alichokipata kutoka maabara ya Arusha ni mfuko ambao ndani yake kulikuwa na sampuli. Tunawezaje kutenganisha jaketi na sampuli alizozipokea pamoja?” Alihoji Jaji.
Jaji Maghimbi alilikataa pingamizi la mawakili wa utetezi na kukubali jaketi hilo lipokelewe kwa utambuzi, hivyo wakili Magafu akapata fursa ya kumhoji shahidi kuhusiana na ushahidi wake.
Alipoulizwa aliyemtajia majina yanayoonekana katika sampuli alizozipokea, shahidi huyo alidai majina hayo yalikuwapo katika nyaraka za utambuzi zilizowasilishwa kwake na RCO.
Magafu alimuuliza shahidi huyo kama anafahamu sampuli za damu na mate za washtakiwa hao eneo (place) zilikochukuliwa, alisema yeye hafahamu.
Kuhusu kama aliwahi kuletewa washtakiwa hao ili achukue upya sampuli za damu na mate, shahidi huyo alisisitiza kuwa sampuli alizoletewa alipelekewa na ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Magafu alimuuliza shahidi huyo kuwa anazungumziaje kauli ya wateja wake (washtakiwa) wanaosema hawakuwahi kuchukuliwa mate wala damu, yeye alisema hajui.
Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi inawakabili washtakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Mussa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Jabir na Ally Mussa.