NDIYO hivyo, Real Madrid wamebeba tena taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya usiku wa jana Jumamosi, kilainii wakajipigia Liverpool 3-1 katika fainali iliyofanyika mjini Kiev, Ukraine.
Liverpool hawatamsahau Gareth Bale, aliyetokea benchi na kuja kupiga mabao mawili matata kabisa, la kwanza la tick-tack, la pili la umbali wa ‘hapa na Mbagala’ unaambiwa. Kwenye fainali hiyo kama kuna mtu alikuwa na usiku mbaya, basi ni kipa wa Majogoo wa Anfield, Loris Karius, ambaye alitoa zawadi ya bao la kwanza, lililofungwa na Karim Benzema na lile la tatu, ambalo alijaribu kudaka shuti la Bale, ambalo lilipigwa kisawasawa. Liverpool wao walipata bao lao la kujifariji kupitia kwa Sadio Mane, lakini kwa fainali hiyo ya usiku wa jana, mabao yote yalipigwa kipindi cha pili, huku Real Madrid wakiweka rekodi ya kubeba ubingwa wa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo, huku ikiwa mara yao ya 13 katika historia.