UNAOGOPA NINI?
Ukichunguza utagundua, wengi wetu tumejawa hofu bila sababu za msingi; hofu ya kupoteza vile tulivyonavyo, tunahangaika kutumia nguvu nyingi kuvidhibiti visituponyoke ili asitokee mwingine wa kuvigusa. Tunafikiri kwa kuvificha, vitaendelea kubaki nasi na kuwa vyetu milele. Tunajidanganya. Mambo hayako hivyo, hayajawahi kuwa hivyo, na hayatokuwa hivyo kamwe.
Kama unafikiri kuna kitu chochote ulichonacho, kitadumu chini yako; iwe pesa, gari, nyumba, mpenzi, ni kujipumbaza akili. Ipo siku isiyokuwa na jina, vyote vinaweza kutoweka kwa pigo moja tu. Pigo moja tu, mtu wangu. Pesa kama ilivyotoka kwa wengine ikaja kwako, pia yamkini ikahamia kwa mwingine; binti yako kipenzi, siku akiolewa atakuacha na kwenda kuwa chini ya milki nyingine; mpenzi wako asipokuacha basi siku atakufa na hatokuwa wako tena.
Shida kubwa, wengi tunaogopa kuanza upya pale tunapopoteza vile tulivyokuwa navyo, ndo maana tunajilazimisha kuvizuia visiguswe na wengine. Kama leo umepata kitu cha thamani l, basi weka akilini kwamba, hakuna unachoweza kukipata halafu ukashindwa kukipoteza, hata iwe roho. Ni suala la muda tu. Hata uwe tajiri, bado hujafikia bado ukwasi kiasi cha kushindikana kuishiwa ndani ya dakika tu. Hata upendwe vipi au uwe mzuri vipi, hujafikia ujanja wa kumzuia akupendaye kuondoka muda wowote.
Kumbuka: Ulichonacho leo, jana hakikuwa chako na pengine kesho kisiwe chako tena. Kila unachokipata, utakiacha papahapa. Ulikuja mtupu na utaondoka mtupu.
Sasa unaogopa nini?
Vinavyotaka kuondoka acha viondoke. Madhali mapigo ya moyo yangali yanadunda vizuri, maadamu tundu za pua zingali zikinyonya hewa vizuri, alimradi damu inaendelea kupenya vizuri katika mishipa, basi unaweza kusimama - ukapamabana na kupata zaidi ya ulichopoteza. Kama uliweza kukipata mara ya kwanza, hutashindwa kukitwaa mara ya pili.