Kabla ya kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua na vumbi.
Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.
Kuna aina mbili za upandaji wa mbegu za uyoga. Aina ya kwanza mkulima anaweza kuchukua mfuko wa nailoni, weka tabaka ya mali ghafi ya kuoteshea kiasi katika mfuko halafu tawanya mbegu juu yake.
Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya kuoteshea na kuweka mbegu juu yake.
Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifikie ujazo wa robo tatu ya mfuko.
Kumbuka: Tabaka la mwisho la juu lazima liwe la vioteshea.
Aina ya pili ni kuchanganya mali ghafi ya kuoteshea (baada ya kuchemsha na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1:25 (yaani mbegu moja kwa mali ghafi ya kuoteshea 25).
Kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp), mchanganyiko huu ujazwe katika mifuko ya nailoni yenye ukubwa wa sm 20 kwa sm 40, ambapo unaweza kujaza kilo moja hadi moja na nusu ya malighafi ya kutoshea. Katika njia zote mbili, funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.
Mbegu za uyoga zinaweza kuota vizuri hata zikikaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
• Unaweza kutumia chupa moja yenye ujazo wa mililita 300 kwenye kilo 15 za malighafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote kwenye chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa kwenye meza, chanja ya waya au miti. Lakini pia inaweza kuning’inizwa kwenye kamba. Unaweza kunyunyizia maji juu ya mifuko. Maji yawe yaliyochemshwa na kupoa na fanya hivyo mara tatu au zaidi kwa siku.
Tahadhari: Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yanaweza kuozesha uyoga. Aina nyingi za uyoga, huanza kutoa vichwa siku mbili hadi tatu baada ya kuwekwa kwenye mwanga.
Uyoga huwa tayari kuvunwa siku tatu baada ya vichwa kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.