POVU la kazi gani sasa? Wala usibishe, sio sisi, huu ni utabiri wa mshambuliaji wa zamani wa England, Michael Owen, kuwa Manchester United itapigwa kwenye mechi yake ya Ligi Kuu England itakayocheza na Tottenham Hotspur keshokutwa Jumatatu.
Staa huyo aliyewahi kuzichezea klabu za Liverpool, Newcastle United, Man United yenyewe na Stoke City kwenye Ligi Kuu England amefika mbali na kutaja kabisa matokeo kwenye mechi hiyo, eti chama la Jose Mourinho litakumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa vijana wa Mauricio Pochettino, wanaoongozwa na straika matata kabisa, mwenye Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia, Harry Kane.