APRIL 2014, Steven Gerrard alionekana akilia baada ya kuongea kwa hisia kali baada ya kuwakusanya wenzake katikati ya dimba la Anfield na kutoa maneno yenye hisia kali baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Manchester City.
Ubingwa wa Ligi Kuu ya England ulikuwa unanukia baada ya miaka 24 ya kuambulia tupu. Anfield ilikuwa imejaa hamasa. Gerrard, mtoto wa mtaani Merseyside alikuwa kiongozi wa vita. Hakuamini hisia zake kwamba yeye na wenzake walikuwa wanakaribia kukata kiu za mashabiki wa Anfield.
Siku chache zilizofuata, yeye mwenyewe alikuwa sababu ya Liverpool kukosa ubingwa. Aliteleza katika mechi muhimu dhidi ya Chelsea. Demba Ba akachukua mpira na kufunga. Ni katika nyakati hizo Liverpool walikuwa wameongoza Ligi kwa tofauti ya pointi tisa kufikia mwezi April lakini bado bingwa akawa Manchester City.
Tumerudi tena katika hisia hizo. Sahau kuhusu kilichotokea juzi Etihad ambapo Liverpool walichapwa mechi yao ya kwanza Anfield, bado kuna maswali ya kujiuliza. Wanaweza kushikilia kamba mpaka mwisho. Kwa sasa ndio timu tishio zaidi duniani. Lakini wanaweza kushikilia kamba mpaka mwisho?
Wana wachezaji halafu wana timu. Vitu viwili tofauti hivyo lakini Liverpool wanavyo vyote. Wana watu wa maana halafu wana watu wanaocheza kitimu. Swali ni lile lile tu Anfield. Wanaweza kushikilia kamba wakavuka mto?
Wanapocheza Ulaya sina hofu na Liverpool. Wana yule mdudu katika vifua vyao ambaye anawaaminisha kwamba wanaweza kuchukua ubingwa wa Ulaya. Na huwa wanafanya kweli. Hata msimu uliopita niliwawekea dhamana ya kutwaa ubingwa wa Ulaya mbele ya Real Madrid na mpaka sasa naamini kwamba bila ya Mohamed Salah kuumizwa na Sergio Ramos huenda hadithi ingekuwa tofauti.
Tazama jinsi walivyopenya katika kundi lao michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Walifungwa mechi zote za ugenini lakini wakapenya siku ya mwisho. Napoli walikosa bao katika dakika za mwisho na hadithi ingeweza kuwa tofauti. Lakini hivyo ndivyo walivyo Liverpool linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Wanapenya katika njia ambazo hauwezi kuamini.
Katika Ligi moyo bado unasita kuwashikia dhamana. Yule mdudu waliye naye moyoni ni tofauti na tule waliye naye moyoni katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Nini kitatokea mbeleni?
Baada ya mechi ya juzi nimezidi kupata hamu ya kujua ambacho kitawatokea Liverpool ikifika Mei. Kwanza ni kwa jinsi ambavyo walimaliza mechi wakiikandamiza City katika lango lao. Pili ni kwa namna ambavyo baada ya mwamuzi, Anthony Taylor kumaliza mechi hawakuonekana kama walikuwa wamevunjiika mioyo. Labda kwa sababu kuna mechi 17 mkononi.
Huenda huu ukawa msimu wao. Tatizo ni kwamba kwa kikosi hiki ambacho wanacho kwa sasa, kama Liverpool haitachukua ubingwa wa England msimu huu kuna uwezekano mkubwa kikosi kikaanza kushuka chini msimu ujao.
Kitu kinachoitwa uchovu wa msimu wa pili au kwa kiingereza, Second season syndrome kinaweza pia kumpata mtu aliyefukuzia ubingwa kwa nguvu kubwa lakini akaukosa. Msimu unaofuata sio lazima achukue kwa sababu kuna uchovu ambao unawaingia wachezaji na kocha kwa ujumla. Na ndio maana Liverpool inabidi wamalize kazi msimu huu.