LONDON,England.UKIFUNGUA simu za mashabiki wa Manchester United pale England, kila mmoja povu linamtoka, utakuta meseji aliyotuma au kutumiwa ama akimtukana kocha au kumdhihaki na meseji nyingine zinaweza kuwa za kuwatukana au kuwashutumu wachezaji.
Mwanzoni kabla ya mchezo wa Everton na Manchester United, ilikuwa tambo, lakini kadiri muda ulivyokuwa unakwenda mambo yalibadilika. Dakika 90 zilipotimia matokeo yalikuwa Everton 4 na Manchester United 0.
Walioleta balaa lote hilo ni Richarlison, Sigurdsson, Digne na Walcott walioipa Everton mabao hayo muhimu dhidi ya Manchester Utd.
Jioni ya jana kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wameanza kukosa subira na kocha wao, Ole Gunnar Solskijaer, wakikumbuka machungu waliokuwa wameyasahau ya Jose Mourinho.
Mmoja wa mashabiki wa timu hiyo aliposti: “Man Utd walipaswa kusubiri hadi mwisho wa msimu, ilikuwa wamfanyie tathmini kwanza, Ole Gunnar Solskjaer kabla ya kufanya uamuzi mzito.
Shabiki mwingine aliandika: “Mabosi wa Old Trafford ni kama walikurupuka kumpa mkataba wa kudumu. Wamempa majukumu mazito. Kwani nani alikuwa anataka kumuona akiwa hapa kesho, soka ni mchezo wa maajabu.”
Mwingine aliyeumizwa na matokeo aliandika: “Haya si tu matokeo mabaya hata mechi yenyewe ilikuwa ovyo kuwahi kutokea katika historia ya Man United siku za karibuni...nusu ya wachezaji lazima wamwagwe mwisho wa msimu.”
Mchezo wa jana ni wa sita kwa Solskjaer kupoteza kati ya mechi nane za mashindano yote tangu akabidhiwe rasmi mikoba ya timu hiyo.
Kipigo hicho kimeipoteza Manchester United kwenye ramani ya kuwania Top Four, na inaendelea kubaki kwenye nafasi yake ya sita ikiwa na pointi 64 na imebakisha mechi nne ambazo endapo itashinda zote itafikisha pointi 76, ambazo tayari zimeshavukwa na Manchester City (86) na Liverpool (85) kabla ya mechi ya jana dhidi ya Cardiff.
Kilichowakera mashabiki wa timu hiyo, ni Everton iliyokuwa nafasi ya tisa kabla ya kupanda hadi nafasi ya saba ikiwa na pointi 49, kutawala mchezo huo kwa sehemu kubwa.
Muuaji wa Everton, Theo Walcott, alizungumza na Sky Sports baada ya mchezo: “Tulicheza kwa umoja, tulipambana na matokeo yameonekana - kikubwa ni mashabiki wetu wamefurahi.
“Tulijua kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini mwisho wa siku tumeshinda, tuliajindaa kimazoezi na tumeonyesha tunaweza.”
Lakini Solskijaer aliwatuliza mashabiki akisema: “Unapopoteza mchezo kila mmoja anaona maisha yamevurugika, tumepoteza mchezo na Barcelona, kila mchezaji ilimchanganya, na kumrudisha mchezaji mchezoni si suala la usiku mmoja.
“Watu wanataka kuona timu ikicheza mpira wake.
Tumefungwa kirahisi sana, tulipoteana. Lilikuwa suala la wazi, kinachotakiwa ni kujipanga.
“Tunatakiwa kushinda mechi zote nne zilizosalia, na hiyo itatusaidia walau kuingia kwenye Top Four. Ni kazi kubwa, lakini tutaiweza tu.”
Katika mchezo huo, Gylfi Sigurdsson na Lucas Digne walifunga mabao ya mbali wakati Richarlison alifunga bao la kifundi katika mpambano huo uliopigwa Goodison Park.
Man United, ambayo bado ina majeraha ya kufungwa na Barcelona Jumanne iliyopita Ligi ya Mabingwa, hawakuonyesha soka la maana zaidi ya kupiga shuti moja dakika ya 86.
Marcus Rashford alikuwa kwenye eneo zuri, aliwatoka mabeki wa Everton na kupiga mkwaju uliopaa juu ya lango la Jordan Pickford.
Endapo Everton itabakia nafasi ya saba, itakata tiketi ya michuano ya Europa League msimu ujao.