Halafu humo humo Babu alimpa Manning darsa za kisiasa, maadili, sheria na za historia. Kwa mfano, alimnukuu Fidel Castro aliyewahi kusema kwamba hakuna kazi iliyo ngumu “kushinda kumshtaki mtu asiye na hatia.” Babu alimuelezea Castro kuwa “mpiganiaji thabiti, adhimu na shujaa wa haki za umma.”
Kadhalika, Babu alimwandikia Manning hivi: ““Tatizo la kijamii, naliwe kubwa vipi na lenye kutisha vipi, linaweza tu kutanzuliwa kwa njia za kijamii na siyo kwa ukandamizaji.”
Halafu Babu akamtajia Manning Jenerali Francisco Franco, aliyekuwa dikteta wa Hispania tangu 1939 hadi alipofariki 1975. Babu aliandika: “Franco alijaribu kukandamiza, na tazama mchirizo wa damu na uvundo aliouacha.”