Tayari presha inapanda na kushuka. Algeria iko tayari, Kenya ambayo imerejea kwenye fainali hizi kwa mara ya kwanza tangu ifanye hivyo mwaka 2004 chini ya uongozi wa Jacob 'Ghost' Mulee nayo imeanza kuvimba.
Mbali na Wanyama, katika mechi hii, itakayopigwa muda mfupi baada ya Mbwana Samatta kuiongoza Taifa Stars ya Tanzania kupambana na Simba wa Teranga, Kenya pia itamtegemea Straika wa Kashiwa Reysol ya Japan, Michael Olunga, kuongoza mashambulizi.
Kwa upande wao, Desert Warriors, ambao ni moja ya timu zinazopigwa upatu kutesa katika makala haya ya 32, wataingia dimbani wakiwa na uhakika wa kuiangamiza Kenya, hii ni kutokana na uwepo wa mkongwe Islam Slimani kikosini.
Akiizungumzia kikosi cha Algeria, Wanyama alisema amekutana mara kadhaa na Mahrez na Slimani, ambao alisema anafahamu uwezo, lakini akatahadharishha kuwa wamejipanga kuwazuia na kuongeza kwamba Stars imejipanga kwa ajili ya mapambano.
Mpaka hapa tulipofikia hatuna presha yoyote, Algeria ni timu nzuri sana, lakini nasi tuko vizuri na tumejipanga kuwakabili, haitakuwa rahisi kama wengi wanavyodhani. Nimekutana na Riyadh na Islam mara nyingi tu, nawafahamu uwezo wao, tutajitahidi kuwazuia," alisema Wanyama.
Kwa upande wake, Mahrez ambaye ni nahodha wa Algeria alisema hawataelekeza nguvu zao kwa Wanyama pekee yake maana wanatumbua uwepo wa Olunga, ambaye alisema ni hatari sana na kuongeza wako tayari kwa ajili ya kila mchezaji wa Kenya bila kubagua.
Wanyama ni mchezaji mzuri sana, anachezea timu kubwa England. Nimecheza dhidi yake mara nyingi, lakini hiyo haimaanishhi kuwa tutajikita katika kumuwaaza yeye tu, tumejipanga kutokukidharau kikosi kizima cha Kenya, hasa yule straika wao mrefu (Olunga)," alisema Mahrez.