Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Na ni msingi gani unaotumika na Tanzania leo kudai eneo la Ziwa Nyasa? Na ni msingi upi unaotumika leo na nchi za Afrika kuweka pasi za kusafiria ndani ya Afrika na vikwazo vya viza na vyenginevyo. Kusupa atueleze kama uzalendo, Uafrika na udugu ndio chanzo cha umoja wa Afrika, kipi kinachoipa Tanzania kuhofia Kenya kuhusu ardhi na kufanya kazi bila kizuizi? Ni vyema tukawa wakweli na kuzitendea haki taaluma na nadhari zetu. Ni vyema pia kuwa na heshima kwa wenzetu kwa kutowauzia kasumba za ajabu za uzalendo pori kiasi hichi.
 
Jambo jengine ninaloomba kuwatanabahisha akina Kusupa ni kuwa asiwatishie nyau Wazanzibari kwa Sultani kama kwamba ni jinni linaloishi kuimeza Zanzibar wakati wowote ule kutapokuwa na mabadiliko katika siasa za Muungano. Anachojaribu kueleza ni kasumba iliyochakaa mno.
 
Kwanza, ni ukweli wa historia ambao akina Kusupa na hata wale walionunua na kutandika kasumba za akina Kusupa katika ofisi zao za mamlaka ya siasa Zanzibar kwamba baada ya suluhu ya Governor Canning ya 1860, Zanzibar na Oman zilitengana rasmi kiutawala. Sultani wa Zanzibar hakuwa tena na mamlaka Oman na wala Sultani wa Oman hakuwa tena na mamlaka Zanzibar
 
Kilichobaki ilikuwa historia ya udugu sawa na vile Mmasai, Mjaluo, Mngoni, Mhindi, Muarabu au Mzungu wa Tanzania anavyojua kuwa asili yake ni pahala fulani na inawezekana ana udugu na watu wa pahala fulani. Ndio maana Sultani alipopinduliwa hakwenda Oman, bali alikimbilia Uingereza. Hivyo kudai leo Sultani atarudi Zanzibar ni sawa na hadithi ya Alfu Lela-u-Lela, kwa sababu Sultani wa Zanzibar hayupo kimamlaka wala kiaila. Sultan wa leo wa Oman siye aliyekuwa Sultani wa Zanzibar na hivyo hana mamlaka ya kudai chochote Zanzibar wala hana sababu ya kufanya hivyo.
 
Pili, hata Sultani alipokuwepo Zanzibar ni ukweli wa kihistoria kwamba baada ya Mkataba wa Umahamiya (Protectorate Treaty) wa Juni 1890, Sultani alibaki pambo tu katika utawala. Dola na Serikali iliendeshwa na Uingereza. Waingereza walimleta Gerald Portal visiwani Zanzibar tarehe 6 Agosti 1891, ambaye kwanza alipelekwa Misri kujifunza mila za Kiarabu ili kuja kuanzisha rasmi Serikali.
 
Sultani mwenyewe akawekwa katika orodha ya kulipwa mshahara tu (Civil List). Waingereza ndio walioanzisha Mahkama za Kadhi mwaka 1897, Kamisheni ya Wakf mwaka 1907 na ndio waliotangaza kuwa Sheria za Kiislamu ndio zitakuwa Sheria Mama za Zanzibar mwaka 1897. Mfumo wa Serikali ulioasisiwa na Gerald Portal ulibadilishwa mwaka 1906, baada ya Bwana Edward Clarke kuletwa Zanzibar akitokea London kuja kuangalia mfumo wa Serikali ya Zanzibar na namna ya kuuboresha. Mapendekezo ya Edward Clarke yaliidhinishwa na mfumo mpya wa Serikali uliasisiwa tarehe 1 Julai 1906. Chini ya mfumo huo, Brigedia Jenerali Rakes aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi, Bwana Peter Grain ambaye alikuwa Hakimu Mkazi aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar na Bwana C. E. Akers aliteuliwa kuwa Waziri wa Kwanza wa Fedha na Biashara.
 
Nimetoa maelezo haya kwa kina ili akina Kusupa waelewe kwamba Serikali wala dola haikuendeshwa na Sultani. Mambo yote yalipangwa London, kuamuliwa London na kutekelezwa Zanzibar bila hata baadhi ya wakati Sultani kushauriwa. Ndiyo maana, katika Serikali mpya ya 1906 hamkuwa na Muarabu hata mmoja. Ushahidi mkubwa kuliko wote kwamba Zanzibar pamoja na Sultani mwenyewe ikiendeshwa na Uingereza ni pale mwaka 1913, ambapo pamoja na kuwepo Mkataba wa Umahamiya wa Juni 1890, Uingereza waliamua kuiendesha Zanzibar chini ya Ofisi ya Makoloni sawa na koloni jengine badala ya chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ambapo ndipo ilipostahiki.
 
Aidha, mwaka 1962 Uingereza ilimteua Bw. Robertson kuandaa taarifa ya utaratibu wa kuiendesha sehemu ya pwani ya Kenya ambayo Uingereza ilikuwa imeikodi kutoka kwa Sultani tokea mwaka 1895. Mapendekezo yake ndiyo yaliyopelekea sehemu hiyo kurejeshwa kuwa sehemu ya Kenya kuanzia tarehe 5 Oktoba 1963, bila ya shaka kwa maslahi ya kiuchumi ya Uingereza.

Ni kutokana na ushahidi huo wa dhahiri ndipo kasumba za akina Kusupa zinapowasuta. Kama Sultani ndiye aliyekuwa na mamlaka Zanzibar, ni vipi Uingereza ingetamalaki katika kila mamlaka ya Zanzibar.
 
HOJA YA ZANZIBAR KUTOKA KATIKA UMOJA WA MATAIFA

Mwinjilisti Kusupa analeta hoja ya kituko kwamba eti Zanzibar ilitolewa katika Umoja wa Mataifa, kwa sababu Sultani wa Zanzibar angekuwa kikwazo kwa uhuru wa kweli wa Afrika. Hivi ni Sultani yupi huyo? Huyu ambaye tumemuonesha kwa ushahidi wa hapo juu kama hakuwa na mamlaka ya mambo yake mwenyewe na ya nchi yake, awe na mamlaka ya kuzuia uhuru wa Afrika kiasi cha kuogopwa na mataifa makubwa? Huu ni uongo hadhir shahir ambao akina Kasupa wamekuwa wakiwauzia wale waliowatawala akili zao.
 
Sababu ya Muungano na hatimaye Zanzibar kutoka katika Umoja wa Mataifa zimeelezwa kwa ufasaha na kwa ushahidi katika taarifa ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ya mwaka 1967 ambayo iliondolewa katika kiwango cha Taarifa ya Siri ya kitaifa mwaka 2007.

Taarifa hiyo imeeleza wazi kwamba kiini cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni hofu ya mataifa makubwa juu ushawishi wa nchi za mashariki hasa China na Ujerumani Mashariki walizokuwa nao kwa Zanzibar. Aidha, imetaja wazi kuwa urafiki wa karibu sana wa akina Abdulrahman Babu, Ali Sultan Issa na hata Hassan Nassor Moyo na mataifa hayo ulileta uwezekano mkubwa wa nchi hizo kuitumia Zanzibar kueneza ukomunisti Afrika Mashariki na kuigeuza Zanzibar kuwa Cuba ya Afrika Mashariki. Imefafanua pia mbinu zilizotumika kumlazimisha Rais wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, kuingia katika Mkataba wa Muungano.
 
HOJA YA ZANZIBAR NA MAADUI WA MUUNGANO

Mwinjilisti Kusupa ameonyesha dhahiri kuwa yupo jikoni katika mtambo wao wa kasumba. Anahusisha hoja ya umiliki wa Zanzibar wa Latham na maadui wa Muungano. Hii ni nyimbo ya kale na bahati mbaya pamoja na kuwa ya kale haikuingia katika “Zilipendwa” na wala haikuingia katika ule msemo wa zamani wa “Old is Gold”.

Moja kati ya nguzo za udhaifu wa Muungano ni akina Kusupa kugombana na ukweli na kuufanya Muungano kuwa roho yake ni siasa tena siasa za kale ambapo wananchi waliamini na kufata kila lisemwalo na viongozi wa siasa. Siasa ya wakati ambapo maoni ya umma yalifata taasisi za siasa. Zama hizi kitovu cha maoni ya watu na sera za umma sio tena siasa wala taasisi za siasa. Kitovu ni mawasiliano kwa vile watu wanaelewa mengi, taarifa zinasambazwa kwa haraka kuliko kasi ya siasa na taasisi zake. Wanaomiliki maoni ya watu na sera za umma sasa hivi ni wanaomiliki mawasiliano. Hivyo kasumba hizi za kina Kusupa ni lazim ziwekwe pembeni kama Muungano wa kweli na endelevu unatakiwa uwepo.
 
Kama kuna Muungano wa kale ambao uliundwa kwa njia za mashauriano na ridhaa ni ule wa Uingereza na Scotland ambao ulianza mwaka 1603 wakati James Stuart aliposhika ufalme wa nchi mbili za Scotland na Uingereza lakini nchi hizo bado zikaendelea kuwa nchi mbili tofauti kwa zaidi ya miaka 104. Pamoja na juhudi kubwa za Mfalme James Stuart kuziunganisha nchi hizo kwa matamko ya kifalme lakini hakufanikiwa.

Ni hadi mwaka 1707 wakati Mabunge mawili ya Scotland na Uingereza yalipoidhinisha Mkataba wa Muungano. Hata hivyo, Muungano huo umekuwa katika majaribu mara kadhaa na hadi sasa umo katika majaribu. Muungano huo umevuuka majaribu kwa watu kuwa huru na wakweli kujadili udhaifu wa Muungano wao na kurekebisha kasoro zake sio kwa kuuza kasumba zilizochoka na kuwaita wabaya wanaokosoa Muungano.
 
Kwa miaka 52 sasa ya uhai wa Muungano, kumekuwa na kutuhumiana na kutiliana shaka baina ya nchi mbili zinazounda Muungano huu. Hakuna kuaminiana. Ukisoma historia ya Muungano, utaona mvutano ulianza mapema sana mwaka ule ule wa 1964 kuhusiana na Sera ya Mambo ya Nje (Foreign Policy) ya Muungano kuhusu uwepo wa Balozi za Ujerumani Magharibi iliyokuwa ikitambuliwa na Tanganyika na Ujerumani Mashariki iliyokuwa ikitambuliwa na Zanzibar. Mwaka 1965 kukaibuka mvutano mkubwa kuhusiana na uanachama wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Na tokea wakati huo, tumekuwa hatumalizi mwaka bila ya mvutano kuhusiana na uendeshaji wa Muungano huu.
 
Ni maoni ya wengi kwa upande wa Zanzibar kwamba sababu kuu ya mizozo na mivutano hiyo isiyokwisha ni msingi wenyewe wa Muungano na jinsi ulivyoanzishwa kama nilivyogusia kwa ufupi sana hapo juu. Bado wapo akina Kusupa kadhaa wanaodhani kwamba Muungano ni nyenzo ya kuidhibiti Zanzibar hasa kwa sababu ya imani ya dini ya wazanzibari walio wengi. Sina haja ya kuwataja kwa sababu tumepata fursa ya kuwasikia wakiyasema hayo hadharani kadamnasi. Wapo pia wanaodhani kuwa kwa sababu ya udogo wake, Zanzibar ni tegemezi tu wa Bara na itaendelea kuwa hivyo.
 
Tumeshindwa kujifunza historia na yanayotokea ulimwenguni. Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano na Malaysia mwaka 1965 ikiwa hahe hohe; fukara, haina mbele wala nyuma kiasi cha kumfanya aliyekuwa Waziri Mkuu wao wa mwanzo kuangua kilio. Miaka chini ya 30 baadae Singapore ilikuwa ngome ya uchumi wa Malaysia hasa katika kuuza bidhaa zake nje na soko la fedha. Wakati wa mtikisiko wa fedha (currency crisis) si siri kwa vile yapo maandiko ya Mshauri wa Waziri Mkuu Mahathir Bwana Sulong Wong katika kitabu chake “Notes to the Prime Minister” yanayobainisha ni kiasi gani Singapore ilisaidia ringeti ya Malaysia isianguke.
 
Aidha, tukiwauliza Wachina hii leo, hawafichi kwamba Hong Kong, Taiwan na Macau, visiwa vidogo vya China vilivyosaidia kuibadili China kiuchumi kupitia mitaji yao na umahiri wao kiuchumi. Bahati mbaya Muungano wetu hadi leo unapimwa kwa mezani ya kisiasa na wakati mwingi mezani ambayo tayari imeshatangulizwa mawe ya kasumba za akina Kusupa.
 
Wengi tuliona kuwa mchakato wa kuanzisha Katiba Mpya ungekuwa nafasi nzuri ya kufanya hayo. Ni bahati mbaya sana kwa kuongozwa na kasumba za watu kama Kasupa na siasa za kale ambao msingi wake umekuwa ule ule wa mmoja kutaka kumdhibiti mwengine, fursa hiyo tumeivuruga.

Hata hivyo, kama kweli pana nia njema basi bado fursa ipo. Marekani na Japan zilikuwa mahasimu wakubwa lakini leo ni washirika wakubwa. China na Japan walikuwa maadui wakubwa lakini leo wanashirikiana. Ujerumani imepigana vita na mataifa mengine ya Ulaya lakini leo wote ni wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU). Mifano ya aina hiyo ni mingi.

Tanganyika na Zanzibar hazikufikia uhasama kama uliokuwepo katika mifano niliyoitaja. Kuna haja ya kizazi kipya cha viongozi wa Zanzibar na Tanganyika kukaa pamoja na kuzungumza na kisha kukubaliana mfumo mpya wa Muungano utakaohakikisha haki za washirika wote wawili zinalindwa na pia mfumo utakaohakikisha Zanzibar na Tanganyika zinafaidika kwa pamoja na ushirika wao.
 
HITIMISHO

Ni maoni yangu ya dhati kwamba mahusiano baina ya pande mbili za Muungano hayajaimarishwa kwa misingi ambayo inaufanya Muungano kuwa endelevu na unaoweza kuhimili mabadiliko ya kidunia na ya kisiasa. Sababu kubwa ni kwamba tunatumia mbadala wa uwazi, ukweli, usawa na uadilifu katika kujenga Muungano. Tumesahau kwamba sasa hivi dunia haipo katika vita baridi ya kisiasa ya miaka ya 60, sasa hivi dunia ipo katika vita ya wazi ya kiuchumi; kudhibiti rasilimali, masoko na mitaji. Tanzania ya leo ijengwe katika msingi huo na sio udalali wa kasumba za akina Kusupa.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Othman Masoud Othman, ni mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar na wakili. Anapatikana kwa nambari ya simu: +255 777 411 175
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…