Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kwa miaka 10 mfululizo, wawili hao walikuwa wakigawana tu tuzo ya Ballon d’or na hata sasa umri ukianza kuwapa kisogo, bado wanaendelea kutesa wakichuana kwenye tuzo mbalimbali zinazodhihirisha ubora wao ndani ya uwanja.
 
Lakini, kuna wachezaji hao wamepata bahati ya kucheza timu moja na masupastaa hao wote wawili na kutambua ubora wa kila mmoja.

Gerard Pique

Amecheza na Ronaldo: (Man United)

Amecheza na Messi: (Barcelona)
 
Beki wa kati, Gerard Pique ni mmoja wa wachezaji waliopata bahati ya kucheza na masupastaa wote hao wawili, ambapo mara ya kwanza alicheza na Ronaldo kuanzia mwak 2004 hadi 2008 huko kwneye kikosi cha Manchester United, kabla ya kuhamia Barcelona, mwaka 2008, ambako alikutana na Messi na kucyeza naye timu moja hadi sasa.
 
Paulo Dybala

Amecheza na Ronaldo: (Juventus)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Baada ya kuanza kuitumikia timu ya taifa ya Argentina chini ya kocha Gerardo Martino muda mfupi baada ya kutua Juventus akitokea Palermo, Paulo Dybala amechezea kikosi hicho mechi 28 tangu mwaka 2015, ambako kuna mechi kibao amekuwa kwenye timu moja na supastaa Messi.

Uhusiano wake mzuri kwenye kikosi hicho cha Argentin ulifanya Dybala kuna wakati ahusishwe na Barcelona. Lakini, kwa kuanzia 2018, Dybala amepata nafasi ya kucheza na supastaa mwingine, Ronaldo huko Juventus na hivyo kupata bahati hiyo ya kucheza na wakali hao wote wawili duniani.
 
Andre Gomes

Amecheza na Ronaldo: (Ureno)

Amecheza na Messi: (Barcelona)

Kiungo wa Everton, Andre Gomes kwa sasa anauguza majeraha yake ya kufanyiwa upasuaji baada ya kuvunjika enka, lakini mchezaji huyo amekuwa mmoja wa wale walipata nafasi ya kucheza na Ronaldo na Messi.

Gomes kwanza amepata nafasi ya kucheza na Ronaldo kwenye timu ya taifa ya Ureno tangu mwaka 2014, kabla ya mwaka 2016 kwenda Barcelona akitokea Valencia na hivyo kupata fursa ya kucheza timu moja na Messi huko Nou Camp. Maisha yake Barcelona hayakuwa mazuri na kuondoka kwenye timu hiyo akienda Italia kabla ya sasa kuwa staa mkubwa huko Goodison Park
 
Nelson Semedo

Amecheza na Ronaldo: (Ureno)

Amecheza na Messi: (Barcelona)

Nelson Semedo si mchezaji wa kwanza kwenye orodha hii kucheza na Messi akiwa kwenye kikosi cha Barcelona na Ronaldo kwenye timu ya taifa ya Ureno. Semedo na Ronaldo wamekuwa pamoja kwenye timu ya Ureno tangu mwaka 2015 na miaka miwili baadye, beki huyo wa pembeni alipata nafasi ya kucheza na Messi huko kwenye kikosi cha Barcelona.

Semedo amekuwa akitamba na Messi huko Nou Camp akiwahi kumtengenezea mabao matano supastaa huyo wa Kiargentina ikiwamo penalti nne. Ronaldo na Messi wote wamepata faida ya kucheza na Semedo.
 
Carlos Tevez

Amecheza na Ronaldo (Man United)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Carlos Tevez alianza kuichezea timu ya taifa ya Argentina mwaka 2004 chini ya kocha Marcelo Bielsa, lakini alisubiri hadi mwaka uliofuata kupata nafasi ya kucheza timu moja na Messi wakati wa mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2006.

Kiwango bora cha Tevez kilimfanya anaswe na West Ham United na kwenda England, ambako baada ya muda tu akanaswa na Manchester United, mahali ambako alikwenda kukutana na Ronaldo na kucheza timu moja mwaka 2007. Man United ya Tevez na Ronaldo ilikuwa moto wa kuotea mbali.
 
Gonzalo Higuain

Amecheza na Ronaldo: (Real Madrid) & (Juventus)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Straika, Gonzalo Higuain amepata nafasi ya kucheza na Ronaldo kwenye timu mbili tofauti, kwanza Real Madrid wakicheza kwa miaka miwili kabla ya sasa kuwa pamoja tena katika kikosi cha Juventus. Wawili hao wanaonekana kuwa vizuri wanapokuwa pamoja uwanjani.

Lakini, staa huyo aliyewahi kucheza kwa mkopo AC Milan na Chelsea, alipata nafasi pia ya kukipiga na Messi na walikutana katika timu ya taifa ya Argentina. Gonzalo amekuwa msaada mkubwa kwa Messi katika kuifanya Argentina kutamba kabla ya straika huyo kuamua kustaafu soka la kimataifa msimu uliopita.
 
Gabriel Heinze

Amecheza na Ronaldo: (Man United)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Gabriel Heinze alikuwa kwenye kikosi cha Sporting CP, timu ya utotoni ya Ronaldo na hakika walikuwa katika kipindi kimoja. Lakini, beki huyo wa Kiargentina alikuwa kwa mkopo huko Ulaya akikaa kwa muda kadhaa kabla ya kuanza kucheza. Alikwenda kupata nafasi rasmi ya kucheza na Ronaldo baada ya kujiunga na Man United, ambapo walicheza pamoja kuanzia 2004 hadi 2007.

Wakati huko Man United, Heinze akipata nafasi ya kucheza na Ronaldo, kwenye soka la kimataifa alikuwa akicheza pamoja na supastaa Messi. Hata mechi ya kwanza ambayo Messi alichezea timu yake ya taifa ya Argentina, Heinze alikuwamo uwanjani na kufunga bao la ushindi dhidi ya Hungary.
 
Fernando Gago

Amecheza na Ronaldo: (Real Madrid)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Beki, Fernando Gago ameingia kwenye orodha hii ya wanasoka waliopata nafasi ya kucheza na masupastaa wa nguvu kwenye soka, Ronaldo na Messi. Staa huyo, alipata nafasi ya kucheza na Messi kwenye mechi kibao za timu ya taifa ya Argentina, lakini pia aliwahi kuwapo kwenye kikosi cha Real Madrid, mahali ambako mara kadhaa alikuwa katika kikosi cha Los Blancos kilichokuwa na huduma ya Ronaldo ndani ya uwanja.

Hilo, lilimfanya Gago kutambua ubora wa washambuliaji wote hao wawili, kwamba wakati yupo Real Madrid alikuwa na kazi ya kumdhibiti Messi, lakini alipokuwa Argentina, ilikuwa shughuli ya kumkaba Ronaldo kwenye soka la kimataifa.
 
Angel Di Maria

Amecheza na Ronaldo: (Real Madrid)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Staa, Angel Di Maria aliwasili Real Madrid mwaka mmoja baad ya Ronaldo. Kwenye kikosi hicho cha Bernabeu, Di Maria alicheza mechi kibao sambamba na Ronaldo na kuna wakati alitengeneza kombinesheni matata kabisa kwenye fowadi sambamba na Karim Benzema. Walibeba mataji kibao kwa pamoja.

Ukimweka kando Ronaldo, Di Maria alipata pia nafasi ya kucheza na Messi, huko kwenye timu ya taifa ya Argentina. Wawili hao walikuwa na msaada mkubwa kwenye timu yao ya taifa wanapokuwa pamoja uwanjani. Messi na Ronaldo wote walifurahia kucheza na Di Maria.
 
Ezequiel Garay

Amecheza na Ronaldo: (Real Madrid)

Amecheza na Messi: (Argentina)

Unamkumbuka Ezequiel Garay? Mchezaji aliyetajwa kuwa na kipaji kikubwa, lakini hakuweza kufikia kiwango cha juu kabisa cha soka lake.

Aliibukia kwa kasi huko Real Madrid mwaka 2008 na mwak uliofuatia Ronaldo akatua hapo na kupata nafasi ya kucheza timu moja. Hata hivyo, hakucheza muda mrefu sana na Ronaldo, kwa sababu alitolewa kwa mkopo mara kadhaa.

Lakini, Garay yupo kwenye orodha hii ya mastaa waliopata nafasi ya kucheza na masupastaa wa dunia, Ronaldo na Messi, ambaye yeye alikipiga naye kwenye timu ya taifa ya Argentina, akisimama kwenye beki na Messi akiongoza mashambulizi.
 
Deco

Amecheza na Ronaldo: (Ureno)

Amecheza na Messi: (Barcelona)

Fundi wa mpira, Deco naye alipata nafasi hiyo ya kucheza na Ronaldo na Messi timu moja. Alikuwamo kwenye kikosi cha Barcelona, wakati Messi anacheza mechi yake ya kwanza huko na ilikuwa hivyo akiwa kwenye kikosi cha Ureno, wakati Ronaldo anacheza mechi yake ya kwanza kwenye timu ya taifa dhidi ya Kazakhstan.

Ronaldo na Deco walionyesha pacha bora kabisa kweye fowadi katika fainali za Euro 2004, ambapo kwa pamoja walihusika kwenye mabao sita.
 
Henrik Larsson

Amecheza na Ronaldo: (Man United)

Amecheza na Messi: (Barcelona)

Nyakati za Larsson kwenye timu za Barcelona na Manchester United zote zilikuwa fupi, lakini zenye kumbukumbu kibao.

Akitokea Scotland, alikotengeneza jina lake na kuwa juu kabisa, staa huyo wa Sweden alipata nafasi ya kuichezea Barcelona kwa misimu miwili na hivyo kuunda kikosi kilichokuwa na mastaa kama Ronaldinho, Samuel Eto’o na Deco.
 
Pia alipata nafasi ya kucheza na Messi ambapo walifanikiwa kufunga mabao kwenye mechi mbili za ligi tofauti. Januari 2007, Larsson alikwenda kujiunga na Man United kwa mkopo na huko alikwenda kukutana na Ronaldo, Wayne Rooney, Louis Saha na Ole Gunnar Solskjaer wakicheza kwenye fowadi.
 
Back
Top Bottom