Kiasi cha miezi miwili kutoka siku hiyo aliyokuja Karume gerezani, natumai ilikuwa taarikh 14 Ramadhan, Disemba 1968, kiasi cha saa 12 za magharibi muda mchache kabla ya kulia kwa kin'gora, alitujia sajini wa magereza na alitutaka tuchukue futari zetu tumfuate kwani wakati huo tulikuwa tumesha letewa mapande yetu ya muhogo wa kutokosa na majani mapevu ya kisamvu.
Tulichukua na tulimfuata mpaka katika uwanja wa 'kotagadi' alituambia tukae hapo. Kiasi cha muda mdogo, kin'gora kililia na tuliruhusiwa kwenda kutawadha na kusali, tulifuturu na kiasi cha kumaliza tu, taa zote za 'kotagadi' zilizimwa kumekuwa kiza totoroo! Mara lango la gereza lilifunguliwa na gari la magereza likaingia ndani kinyume nyume. Roho zilitubakuka, vinywa vilijaa mate, mradi kila mmoja hajijui, hajitambui. Muda si muda, tuliambiwa tuingie katika hiyo gari. Msafara wetu haukuwa mkubwa sana kwani ulimalizikia kwenye gereza la kwa "Ba Mkwe" au kwa jina lengine, "Mlango wa Nyuma". Wakati huo, wenzetu wawili, AhmedRashad Ali na Ali Manara, wao walikwisha achiliwa huru.