MANCHESTER United na Tottenham Hotspur ndiyo timu zilizokuwa ‘bize’ zaidi katika dirisha dogo la usajili, lakini je, ni kiasi gani kimetumika Januari miongoni mwa timu zote za Ligi Kuu England? Si kidogo.
Jumla ya Pauni 233 milioni imetumika katika usajili wa jumla wa wachezaji 31, wakati wa dirisha dogo la usajili, lakini ni kiasi gani kimetumiwa na timu yako Januari? Maana si zote zimesajili.
Kwa ujumla msimu huu imetumia Pauni 86 milioni zaidi ya zile zilizotumika katika usajili wa Januari wa mwaka jana, huku matumizi kamili yakiwa ni Pauni 188 milioni hii ni baada ya Pauni 45 milioni kurudi kutokana na baadhi ya timu kuuza wachezaji.
Tottenham imewaleta Steven Bergwijn na Giovani Lo Celso kwa dau la Pauni 27 milioni kila mmoja, Bergwijn ametua akitokea PSV Eindhoven na Lo Celso kwa Real Betis, huyu mwanzo alikuwa Spurs kwa mkopo.
West Ham imetumia Pauni 25 milioni kumsajili straika wa Hull City Jarrod Bowen, Sheffield United imemnasa kiungo wa Genk, Berge Sander kwa Pauni 22 milioni wakati Wolves imemchukua winga wa Olympiakos, Daniel Podence kwa dau la Pauni 16.9 milioni.
Man United imeongoza kwa matumizi kutokana na kutumia Pauni 67.7 kumsajili Fernandes, wamefuatiwa na Tottenham (Pauni 54 milioni), West Ham (Pauni 29 milioni), Sheffield United (Pauni 23 milioni), Wolves (Pauni 17.9 milioni) na Aston Villa (Pauni 10.9 milioni).
Liverpool (Pauni 7.3 milioni), Burnley (Pauni 7 milioni), Watford (Pauni 6.8 milioni), Brighton (Pauni 5 milioni), Norwich (Pauni 3.4 milioni) na Everton (Pauni 1 milioni ), lakini kuna klabu nane ambazo zimeshinda kutumia hata pesa kidogo kusajili Januari.
Manchester United ndiyo imetumia pesa ndefu zaidi Januari, lakini Kocha wa Spurs, Jose Mourinho ndiye aliyekuwa bize zaidi, akiwa ameichukua timu katikati ya msimu alikomaa na bosi wake Daniel Levy amletee watu na kweli jamaa hakumfelisha.
Spurs imeziba pengo la Christian Eriksen aliyetimkia Inter Milan kwa kumsajili Gedson Fernandes kutoka Benfica na kumchukua jumla Lo Celso kutoka Real Betis na pia kuimarisha safu yao ya ushambiliaji kwa kumsajili Bergwijn kutoka PSV Eindhoven.
Lakini, ilishindwa kusajili straika mpya wa kuziba pengo la majeruhi Harry Kane, hii ni baada ya kufeli kuwanasa kina Olivier Giroud, Willian Jose na Krzysztof Piatek , huku pia dili la dakika za mwisho la Gareth Bale likifeli.
Ila Mourinho atakuwa amefurahishwa na kitendo cha klabu kumpa sapoti sokoni. Hivyo anaamini wakati wa kiangazi mzigo utakuwepo na atatengeneza timu anayoitaka.
Tottenham ndiyo imepiga mkwanja mrefu zaidi kutokana na mauzo ya wachezaji baada ya kumuuza kiungo Eriksen kwa Pauni 16.9 milioni kwenda Inter Milan, staa huyo alikuwa anamaliza mkataba wake Spurs mwisho wa msimu
Wolves imeingiza Pauni 15 milioni kwa kumuuza Ivan Cavaleiro kwenda Fulham, wakati Burnley (Pauni 4 milioni), Liverpool (Pauni 3 milioni), Aston Villa (Pauni 2.7 milioni), Watford (Pauni 1.8 milioni) na Manchester United (Milioni 1.5 milioni), klabu zote zimepata japo kidogo kutokana na mauzo ya wachezaji.
Katika mwezi mzima ni klabu mbili tu za Ligi Kuu ambazo ziliingiza pesa ya kuridhisha kidogo kutokana na mauzo ya wachezaji. Spurs imeingiza Pauni 17 milioni na Wolves Pauni 15 milioni kwa mauzo ya Christian Eriksen na Ivan Cavaleiro.
Klabu iliyowafuatia ni Burnley, imepiga Pauni 4 milioni kwa kumuuza Nahki Wells kwenda Bristol City. Hii ni dalili kuwa timu za Ligi Kuu hazikuwa na uhitaji mkubwa sokoni.
Licha ya kuingiza pesa kwa mauzo ya Eriksen, Tottenham ina wastani wa kutumia Pauni 37.1 milioni, ikifuatiwa na West Ham (Pauni 29 milioni), Sheffield United (Pauni 23 milioni) na Aston Villa (Pauni 8.2 milioni) – kwa ujumla msimu huu wastani wa matumizi ni Pauni 100 milioni zaidi ya msimu uliopita.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.