Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Juan Martín del Potro

- Boca Juniors

Nadal si staa pekee wa mchezo wa tenisi mwenye mapenzi na soka. Muargentina, Juan Martin del Potro ni mkali mwingine ambaye amekuwa akitumia muda wake wa ziada asipokuwa na mechi na mazoezi kwenda kuifuatilia timu yake anayoipenda Boca Juniors. Amekuwa akijiunga na kundi la mashabiki wa timu hiyo na wakati mwingine amekuwa akitazama mechi za Boca kupata mzuka kabla ya kuingia uwanjani kwenye mechi zake za tenisi. Del Potro ni swahiba wa staa sa zamani wa Italia, Mauro Camoranesi, ambaye walikulia pamoja katika jiji la Tandil. Jambo hilo lilimfanya pia kuifuatilia Juventus kwa sababu alikuwa akiichezea rafiki yake, Camoranesi kwa miaka minane kati ya 2002 na 2010.
 
Lewis Hamilton

- Arsenal

Wakati mkali wa Formula One, Lewis Hamilton asipokuwa kwenye mashindano hayo ya mbio za magari, amekuwa akitumia muda huo kuifuatilia timu yake anayoshabikia ambayo ni Arsenal. Mapenzi yake kwenye soka ni makubwa kwelikweli kiasi kwamba kuna wakati alihitaji kujiendeleza kwenye mchezo huo kwa sababu huko nyuma aliwahi kucheza timu moja na Ashley Young walipokuwa watoto, lakini yeye aliamua kujikita zaidi kwenye mbio za magari. Hamilton amekuwa akiifuatilia Arsenal waziwazi na amekuwa akishiriki kwenye mijadala mbalimbali ya kuhusu timu hiyo huko kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter na Instagram na kufuatilia kila kitu.
 
Michael Schumacher

– FC Koln

Gwiji wa Formula One, Michael Schumacher alitumia muda wake mwingi akiwa hashiriki michezo yake kucheza mpira na kwa kipindi chote amekuwa shabiki wa FC Koln inayokipiga kwenye Bundesliga. Akiwa amekulia karibu na Hurth, Schumacher alipata nafasi ya kuifuatilia timu hiyo ya mtaani kwa karibu sana huku mwenyewe akionyesha kuwa na kipaji kikubwa cha kucheza soka kama alivyokuwa akifanya kwenye mechi mbalimbali za hisani. FC Koln ilikuwa moja ya timu za kwanza kabisa kuonyesha kuguswa na ajali iliyompata Schumacher wakati alipoanguka kwenye michezo ya kuteleza kwenye barafu mwaka 2013 huku familia yake ikiwa bado inashabikia timu hiyo hadi sasa.
 
Usain Bolt

- Manchester United

Mwanariadha supastaa wa Jamaica, Usain Bolt alikuwa mkali wa mbio fupi zilizomfanya kubeba medali kibao za dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki. Bolt, ambaye baadaye alienda kucheza soka kwenye timu moja huko Australia hakutaka kuweka kificho kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa Manchester United. Mwanariadha huyo alikuwa akimfuatilia straika wa Kidachi, Ruud van Nistelrooy, ambaye alikuwa moto Old Trafford kati ya 2001 na 2006 na hilo likamfanya awe na mapenzi na timu hiyo. Man United ilimwalika kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2011 na tangu kipindi hicho Bolt amekuwa na uhusiano wa karibu sana na timu hiyo.
 
Steve Nash

- Tottenham Hotspur

Mmoja wa wakali matata kabisa kwenye historia ya mpira wa kikapu kwenye NBA, Steve Nash sehemu kubwa ya utotoni mwake alikuwa akicheza soka. Babu yake alikuwa shabiki mkubwa wa Tottenham Hotspur na baba yake alikulia hatua chache sana kutoka kwenye uwanja wa wa Spurs, White Hart Lane, jambo lililofanya familia hiyo kuwa na mapenzi makubwa kwa timu hiyo. Tangu wakati huo, Nash amekuwa akiishabikia timu hiyo na sasa akiwa amestaafu kwenye mchezo wake, amekuwa akitumia muda wake kuketi kwenye televisheni kutazama mechi za Spurs kila inashuka uwanjani. Spurs sasa inanolewa na Jose Mourinho.
 
Tiger Woods

- Barcelona

Bingwa mara tano wa mashindano ya dunia ya gofu, Tiger Woods amehakikisha kwamba kwenye maisha yake yote amekuwa mpenzi wa miamba ya La Liga, Barcelona. Staa huyo wa gofu mara kibao amekuwa akionekana amepiga picha akiwa na jezi za timu hiyo na aliwahi kuhudhuria pia kipute cha El Clasico kilichopigwa Miami, Marekani mwaka 2017. Woods alitumia mechi hiyo yeye na watoto wake kukutana na mastaa Lionel Messi na Luis Suarez pamoja na kocha Ernesto Valverde na kujenga ukaribu mkubwa tangu siku hiyo.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…