D A E M U S H I N
JF-Expert Member
- Dec 15, 2015
- 22,665
- 121,102
Msururu wa manowari zenye nguvu [tokea mwaka 2008] umekuwa ukifanya doria baharini … Zaidi ya mataifa thalathini yamepeleka meli za kivita – pamoja na manowari za kubebea ndege za kivita, manowari za kusindikiza, manowari za ulinzi na vyombo vyengine vyenye silaha nzito – pamoja na ndege nyengine za kisasa kabisa za kijeshi. Kwa maelezo rasmi, vikosi hivi vya baharini vinatoa ulinzi baharini dhidi ya maharamia – Wasomali walio ndani ya mashua ndogo waliozikamata meli za kibiashara na watumishi wao ili kupata fidia kabla ya kuwakomboa mateka wao. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mara kwa mara limekuwa likiidhinisha harakati za kijeshi baharini huku likitoa tahadhari ya vitisho vya maharamia kutishia kuwepo njia salama kwa meli za kimataifa na ‘vitisho vyao dhidi ya amani ya dunia na usalama katika kanda hiyo. (Dershowitz na Paul, 2012:14)
Mwezi Desemba 2006, Serikali ya Tanzania ilitoa idhini ya … kuwepo kwa Kikosi Kazi cha Pamoja Pembe ya Afrika, kuanzisha kuwepo kwa Kikosi cha Shughuli za Kiraia katika mwambao wa Uswahilini. Kikundi cha Shughuli za Kiraia (ambacho tumekipa jina la Kikosi cha Pamoja cha Afrika na Marekani – AFRICOM) kinaendesha miradi ya kibinadamu na kusaidia kujenga uwezo wa shughuli za kiraia na kijeshi katika Jeshi la Wananchi la Tanzania. (Ubalozi wa Marekani, 2009a)
Wengi, au wengi sana wa wazalishaji wakubwa wa mafuta wa Afrika – Nigeria, Angola, Kamerun, Gabon na Ginekweta – ni makaro ya ufisadi, umasikini na ufakiri uliokithiri. Lakini ili kuhakikisha upatikanaji wa kudumu wa nishati, masoko ya dunia yanazihitaji nchi hizi ziwe na utulivu wa kiasi fulani. (Coleman, 2009: 19)
Kuna ushirikiano mdogo wa Serikali ya Tanzania na wenziwe katika kanda juu ya masuala ya Kupambana na Ugaidi kwa kupitia Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo sasa inazijumuisha nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda pamoja na Tanzania. Mataifa matano haya yanashirikiana kwa kupitia Programu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya: Mkakati wa Kanda ya Afrika ya Mashariki wa Amani na Usalama … Mwisho wa mwaka 2007 Serikali ya Tanzania ilianzisha uhusiano na Serikali ya Sudan; hata hivyo kiwango cha ushirikiano wa kupambana na Ugaidi hakijulikani. Serikali ya Tanzania imefanyakazi kwa pamoja vile vile na serikali ya Kenya juu ya masuala ya Kupambana na Ugaidi hapo zamani na Tanzania ina nafasi ya kudumu katika ofisi ya Polisi wa Kimataifa iliyopo Nairobi. Zaidi ya hayo, Jeshi la Polisi la Taifa lina mawasiliano mazuri na majirani wao wa kanda wengi na limeshiriki katika programu za kikanda za kupambana na Ugaidi ikiwa ni pamoja na maafisa kutoka nchi za jirani kwa kupitia programu zinazogharamiwa na Serikali ya Marekani katika Chuo cha Kusimamia Sheria za Kimataifa kiliopo Gaborone, Botswana. (Ubalozi wa Marekani, 2008c)
Abdi alisema, miswada inayopitishwa na Bunge la Afrika ya Mashariki ina uwezo wa kisheria kwa wanachama wote. Abdi alisema masuala ya mipakani kama vile magendo na usafishaji wa pesa au labda mapambano dhidi ya ugaidi na uhakika wa haki za binadamu, ni maeneo ambayo Bunge la Afrika ya Mashariki linaweza kuwa na jukumu kubwa.