Mchicha ni aina mojawapo ya mboga za majani ambayo hulimwa sehemu nyingi za Tanzania. Mbegu na majani yake yana vitamini A, C, madini ya aina ya chokaa na chuma kwa wingi
Majani ya mchicha hutumika kwa mboga na mbegu zake zinaweza kusagwa na unga wake kutayarishwa chakula cha mtoto au huchanganywa na unga wa aina nyingine kama vile ngano, mahindi, mtama kwa ajili ya vitafunio.
KUTAYARISHA BUSTANI
Tayarisha bustani kwa kufyeka majani, lima na tifua ardhi mwezi mmoja kabla ya kupanda. Weka mbolea ya samadi ya kuku au mboji ili kuongeza rutuba. Tumia debe moja la mbolea katika eneo la mita moja za mraba. Changanya vizuri udongo na mbolea kisha sawazisha.
KUPANDA
Mbegu za mchicha zinaweza kupandwa moja kwa moja bustanini kwa kutawanya au kupanda kufuata mstari. Baadaye miche inaweza kupunguzwa ili kuipa miche iliyobakia nafasi ya kukua vizuri.
Njia nyingine ya kupanda mchicha ni ile ya kuotesha mbegu kwenye kitalu na baadaye kuhamishia kwenye bustani. Mbegu hizi zinaoteshwa kwenye tuta kwa njia ya kusia kufuata mstari. Aina za mchicha ambazo zinafaa kuoteshwa kwenye kitalu ni ile yenye mbegu nyeupe na majani mapana.
KUHAMISHA MICHE
Miche ya mchicha inakuwa tayari kuhamishiwa kwenye bustani baada ya wiki mbili. Siku moja kabla ya kuhamisha, miche imwagiliwe maji ili kurahisisha ung'oaji wake.
Wakati wa kupandikiza miche ipandikizwe katika nafasi zifuatazo:
- Aina fupi za mchicha, miche ipandwe katika nafasi ya sentimita 15 hadi 22 toka shimo hadi shimo na sentimita 28 hadi 30 kati ya mstari na mstari;
Magonjwa na wadudu waharibifu
Mchicha hushambuliwa zaidi na ugonjwa wa kinyeusi. Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia miche michanga kwenye shina usawa wa ardhi. Shina lililoshambuliwa hukauka na hatimaye mmea wote hunyauka na kukauka.
Wadudu ambao hushambulia mchicha ni pamoja na utitiri, vidukari, mbawakau, na kinyambisi au kinyafungo.
Utitiri
- Hawa ni wadudu wadogo sana wenye rangi ya machungwa, nyekundu au kahawia. Wadudu hawa huishi chini ya jani na kufyonza utomvu wake. Jani lililoshambulliwa hugeuka rangi na kuwa manjano, husinyaa, hujikunja na hatimaye kunyauka.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.