Huko nchini Mexico kuna kisiwa kinachojulikana kama "La Isla de las Muñecas" yaani kisiwa cha midoli. Jina hili limetokana na uwepo wa midoli mingi ya ajabu ajabu iliyoning'inizwa kwenye miti ya eneo ilo. Simulizi hii inahusishwa na Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Don Julian ambaye ndiye alikua anaishi eneo ilo. Don Julian alidai kuwa kisa cha kuning'iniza midoli hiyo katika miti kilianza muda mfupi baada ya kuhamia katika kisiwa hiko, alikutana na tukio la kutisha, alikuta mwili wa msichana mdogo ufukweni mwa kisiwa, na muda mfupi baada ya tukio hili, Don Julian aliona mdoli akielea majini karibu na alipokuta mwili wa mtoto yule. Kwa kuwa alikuwa akiishi kisiwani peke yake, Don Julian alichukua mdoli yule, akamtundika juu ya mti kama njia ya kutuliza roho ya msichana yule mdogo aliyekufa. Lakini hakuishia hapo miaka iliyofuata aliendelea kutundika midoli ya kila aina. Don Julian muda mwingine alikua akiokota midoli iliyotupwa jalalani na kuwatundika kwenye miti kisiwa chote. Alikua hachagui mdoli wa kuokota, aliokota vipande vya mdoli, visivyo na kichwa, miguu, macho yote aliokota. Kwa kawaida ni midoli ambayo inatisha ukiitazama. Watu wengi walimuona kama ana matatizo ya akili hawakuamini kuhusu hadithi yake kuhusu msichana mdogo aliekufa, waliona ni kama hadithi ya kutungwa tu aliyoianzisha. Lakini jambo la kutisha katika hadithi hii ni jinsi mwisho wa maisha yake unavyoungana moja kwa moja na hadithi ya msichana mdogo aliyekufa. Don Julian alikufa 2001. Mwili wake ulikutwa sehemu ile ile ambayo kila wakati alidai kuwa alikuta mwili wa msichana mdogo amekufa.