Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), leo Mei 5, 2025 kimezindua ripoti ya hali ya haki za binadamu nchini kwa mwaka 2024.
Ripoti hiyo imezinduliwa Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ripoti ya 23 tokea walipoanza utaratibu huo, ambapo wadau mbalimbali wameshiriki uzinduzi akiwemo uwakilishu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora, wawakilishi wa Balozi na taasisi mbalimbali zinazohusika na utetezi wa haki za binadamu.
Ripoti inaangazia mambo kadhaa muhimu. Kwanza, ripoti inaonesha kwamba ingawa kuna hatua zimepigwa katika maeneo fulani ya haki za binadamu, bado changamoto nyingi zinaendelea, hasa katika uhuru wa kujieleza, haki za wafanyakazi, na upatikanaji wa huduma za msingi kama maji na afya .
Changamoto zilizotajwa ni pamoja na ukandamizaji wa wanaharakati na waandishi wa habari, ucheleweshaji wa mishahara na michango ya hifadhi ya jamii (mfano NSSF), pamoja na ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto. Ripoti pia imesisitiza matatizo ya ardhi na migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa ni jambo linaloendelea kuibua mvutano nchini .
Mapendekezo muhimu yaliyotolewa ni pamoja na: kuimarisha taasisi za haki za binadamu, kuhakikisha uwajibikaji kwa wale wanaokiuka haki za binadamu, na kuendeleza elimu kwa umma kuhusu haki zao. Ripoti inahimiza serikali kushirikiana na asasi za kiraia ili kuleta mabadiliko ya kweli katika ulinzi wa haki za binadamu nchini .
Ripoti LHRC: Mwaka 2024 Watu 600 walikamatwa na kuwekwa kizuizini bila kuzingatia sheria
Akizungumzia mambo mbalimbali ambayo yamebainishwa kwenye ripoti ya mwaka 2024 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambayo imezinduliwa leo Mei 5, 2025, Mratibu wa Utafiti, Wakili Fundikila Wazambi amesema kwamba ripoti hiyo inaonesha wimbi watu kukamatwa na kutiwa kizuizini bila kufuata Sheria.
Amesema kwamba katika ripoti hiyo, matukio zaidi ya 600 ya watu kukamatwa na kutiwa kizuizini yaliripotwa kwa mwaka 2024.
Aidha Wakili huyo amesema kwamba bado hakuna kasi katika utekelezwaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yaliyotolewa kwa Rais Samia Suluhu Hassan hali ambayo inaendelea kupelekea uwepo wa changamoto nyingi kwenye mifumo ya Haki Jinai nchini.
Watoto wameendelea kuwa waathirika wakuu wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu
Ripoti inayonyesha kwamba watoto wameendelea kuwa waathirika wakuu wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu (asilimia 41), kama ilivyokuwa mwaka 2023, ambapo asilimia 47 ya waathirika walikuwa ni watoto.
Wanawake wamechukua nafasi ya pili wakiwa na asilimia 29, wakifuatiwa na wanaume (asilimia 15), wazee (asilimia 11), na watu wenye ulemavu (asilimia 4). Asilimia ya waathirika wanawake ilipungua kwa asilimia 1, huku asilimia za waathirika wanaume, wazee, na watu wenye ulemavu zikiongezeka kidogo kwa asilimia 5, 1, na 1. Hii inaonyesha haja ya kuongeza juhudi za kukuza na kulinda haki za makundi maalum".
