Mwanamuziki Diamond Platnumz, wiki hii amejikuta mashakani kwa kukutana na ukosoaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kuonekana kwa bendera inayoonekana inaunga mkono vitendo vya ubaguzi wa rangi na utumwa.
Sehemu ya video ya wimbo huo unaoitwa 'Gidi' iliyotoka hivi karibuni inamuonyesha msanii huyo akiwa amesimama kwenye sehemu inayoonekana ya kuuzia vinjwaji 'kaunta' sehemu nyuma yake kwa juu ya kaunta hiyo kuna bendera hizo zinazofahamika kama 'Confederate flags'.
Ukosoaji huo ulianza kushika kasi zaidi mara baada ya mmoja wa wasanii wa muziki wa hip Hop Tanzania, Webiro Wakazi Wassira, ambaye pia ni mwanasiasa wa Chama cha ACT Wazalendo, kukosoa uwepo wa bendera hizo kwenye video hiyo alipoandika kupitia mtandao wake wa Twitter.
Wakazi alimtaka Diamond kurekebisha vipande vya video vinavyozionyesha bendera hiyo.
Nini asili ya Bendera za Confederate Flag?
Bendera hizi zinawakilisha muungano ulioitwa Confederate States of America (CSA au Confederacy), ulioanzishwa mwaka 1861 baada ya majimbo 11 ya Marekani kuamua kujitenga katika nchi hiyo iliyokuwa na umri wa takribani miaka 85.
Majimbo hayo ni Alabama, Arkansas, Florida, Georgia, Louisiana, Mississippi, North Carolina, South Carolina, Tennessee, Virginia na Texas.
Uasi wa majimbo hayo 11 ulichochewa zaidi na kuchaguliwa kwa Abraham Lincoln kuwa rais. Rais Lincoln alikuwa na msimamo wa kusitishwa kwa biashara ya utumwa, huku majimbo hayo yalikuwa yanatetea vitendo hivyo.
Kukazuka vita kubwa kati ya majimbo hao na majeshi ya Marekani. Ni vita vilivyodumu kwa miaka 4, vikionekana kama vita kati ya watu weupe na watu weusi, kabla ya kumalizwa mwaka 1865, ikionekana kama ushindi dhidi ya utumwa na ubaguzi wa rangi.
Baada ya vita hiyo, kumekuwa na harakati za muda mrefu za kukabiliana na utumwa, kwa zaidi ya miaka 155 nchini Marekani, lakini harakati zinazoonekana kuwa tata, wamarekani wengi weupe, hasa wa Kaskazini mwa taifa hilo, wameonekana kutojitoa sana kupambana dhidi ya ubaguzi.
Kupigwa marufuku kwa bendera za"Confederate Flag'
Bendera na viashiria vyote vinavyoonekana kutukuza utumwa na ubaguzi wa rangi, vilianza kutoweka kidokigo ikiwemo makao makuu ya Bunge la Marekani, huku maeneo mengine mengi wakipiga marufuku.
Wachuuzi wa bendera walitangaza kutoziuza kutokana na namna zinavyochukuliwa, huku kifo cha mmarekani mweusi, George Floyd, kilichocheza zaidi hasira za kutokomezwa kwa viashiria vya ubaguzi ikiwemo bendera hizo.
Ingawa ni zaidi ya miaka 150 sasa tangu majimbo hayo 11 yashindwe vita kutetea utumwa, bado bendera hiyo inaendelea kuigawa Marekani, lakini kuleta msigano pia hata nje ya taifa hilo hasa kwa watu weusi.
Watu wanaoonekana kuwa na bendera hizo katika himaya zao wanachukuliwa kama ni watu wanaotukuza vitendo vya utumwa na ubaguzi wa rangi.
Kwa watu weusi, bendera hiyo inawapa hasira wakirejea mateso na maumivu ya utumwa na ubagunzi yaliyofanyika kwa miaka mingi wakati wa utumwa. Watu wengi weupe hasa nchini Marekani wanaopeperusha bendera hizo hukutana na mashambulizi ya mara kwa mara na wengine wakihukumiwa.
Haishangazi, ukosoaji unaofanyika sasa dhidi ya Msanii Diamond, ni kwa dhana hiyo hiyo ya kwamba ni bendera isiyofaa kutokana na kuhusishwa kwake na vitendo vya kitumwa na kibaguzi.
Wako watu wengi maarufu waliojikuta matatizoni kwa sababu ya bendera hizo. Hawa ni baadhi ya wasanii wengine maarufu waliojikuta matatani kutokana na kutumia bendera za "Confederate Flag' kwenye kazi zao za Sanaa.
KANYE WEST
Mwaka 2013, Kanye West alipigwa picha akionekana amevalia jaketi ambalo lilikuwa limenakshiwa na bendera za Confederate flag' kabla ya kuuzwa kwenye mdana wakati wa tamasha lake la Yeezus.
Wengi walimshambulia kabla ya kujitokeza huko Los Angeles na kufafanua kwa nini alivaa kama alivyonukuliwa na mtandao wa the dailybeast.com:
"Semeni mnavyotaka," West alisema wakati huo. "Nguvu yoyote ni nguvu. The Confederate flag inawakilisha utumwa kwa namna fulani. Hicho ndicho nachofahamu. Kwa hiyo niliandaa wimbo 'New Slaves.' Nikatumia bendera hiyo."
LUDACRIS
Msanii wa Hip Hop wa Marekani ambaye alishambuliwa vikali baada ya kuvaa mavazi yenye bendera hiyo ya 'Confederate flag' wakati akitumbuiza wimbo wake uliovuma "Georgia" kwenye tuzo za VIBE, huko Atlanta.
Ludacris ilibidi ajitokeze kuweka sawa hali ya hewa, na kusema hakulenga kutukuza ubaguzi bali kupinga.
"Bendera hii inawakilisha ukandamizaji ambao sisi waafrika tumepitia kwa miaka mingi; hii ni alama ubaguzi sio tu Kusini lakini ni Marekani. Mi nilivaa kuwakilisha tulipotoka kwa sababu ya ubaguzi. Mwishowe nilivua na kuvaa bendera nyingine yenye rangi nyeusi, nyekundu na kijani, hizo ni rangi za Afrika,” alisema Luda.
ANDRÉ LAUREN BENJAMIN 'ANDRE 3000'
Huyu ni mmoja wa wasanii wawili wanaounda Kundi la OutKast. Mwaka 2000 Andre 3000 na yeye alishambuliwa na baadhi ya Wamarekani baada ya kuonekana kwenye moja ya video za OutKast akiwa na bendera ya Confederate flag.
Andre 3000 alionekana na bendera hizo kwenye mkanda wake wa suruali kwenye moja ya video maarufu za kundi hilo ya "Ms. Jackson."
Licha ya kutojitokeza hadharani kueleza kinagaubaga kwa nini alivaa, watu wengi waliendelea kwa muda mrefu kumsakama.
Msanii wa kufokafoka wa muziki wa Crunk, kama ilivyo kwa Diamond na yeye ameonekana akiwa na bendera hizo kwenye wimbo wake maarufu wa "This Tha City" uliotoka mwaka 2000.
LIL JON
Lil Jon & the Eastside Boyz's kupitia kava ya albamu yao iliyoitwa Put Yo Hood Up na kuibua makelele.
Source: bbc