Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,067
- 10,938
Watu nane wakazi wa eneo la Porikwapori wilayani Kiteto mkoani Manyara, wamefikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mmoja kwa kushirikiana.
Watuhumiwa hao kwa pamoja wamesomewa shtaka hilo leo Jumatatu Agosti 28, 2023 wakiwa mahakama ya Wilaya ya Kiteto chini ya Hakimu wa mahakama hiyo, Mosi Sasy.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Salumu Issa, akiwa mahakamani hapo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Elia Jonas (18), Yajobo Ngoda (20), Abdul Alfa (20), Amos Chales (20), Chales Kiweresa (31), Konja Frank (19), Amos Msalia (18) na Mkombozi William (20).
Watuhumiwa hao walisomewa shitaka kuwa huko Porikwapori wakiwa kwenye sherehe nyakati za usiku walitenda kosa kinyume na Kifungu 131 A (1), (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2022.
Hakimu sasi aliwauliza watuhumiwa hao hapo mahakamani kama walitenda kosa hilo ambapo walikana shtaka lao hilo, huku mwendesha mashitaka wa Serikali Salumu Issa akimweleza Hakimu Sasy kuwa upelelezi umekamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 12, 2023 na kuelezwa kuwa dhamana kwa washitakiwa iko wazi na kutakiwa wafuate masharti yaliyowekwa na mahakama hiyo.
Mwananchi