KERO Vijana tulioshiriki katika Kampeni ya Chanjo ya Polio - Misungwi (Mei 2026) hatujalipwa posho zetu

KERO Vijana tulioshiriki katika Kampeni ya Chanjo ya Polio - Misungwi (Mei 2026) hatujalipwa posho zetu

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Vijana tulioshiriki katika kampeni ya chanjo ya polio iliyofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 10 Mei 2026 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati. Mimi nilifanya kazi katika Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, kama mhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 9.

Kabla ya kuanza kazi tulipatiwa mafunzo ya siku moja na baada ya kumaliza kampeni tulijaza na kusaini fomu za mahudhurio na malipo, kwa kuwa tulielezwa kuwa fedha zetu zingetumwa kupitia simu. Kampeni hiyo ilihusisha makundi mbalimbali, yakiwemo wahudumu wa afya (wachanjaji), wachukua takwimu kama walimu na watendaji, pamoja na wahamasishaji kutoka kwa wajumbe wa nyumba kumi, vijana na wazee wa maeneo husika.

Tarehe 14 Mei 2026, wachanjaji na baadhi ya wachukua takwimu walilipwa stahiki zao. Baada ya wiki moja, baadhi ya wahamasishaji nao walilipwa, lakini sisi wengine tulibaki bila malipo. Tangu wakati huo tumekuwa tukifuatilia haki yetu bila mafanikio.

Kutokana na ukosefu wa majibu, tarehe 15 Juni 2026 tulikwenda kwa pamoja kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, ambaye alituahidi kuwa suala hilo lingeshughulikiwa. Hata hivyo, hadi leo hakuna malipo yaliyofanyika na tumekuwa tukizungushwa bila maelezo ya kuridhisha.

Kwa taarifa tulizonazo, fedha za kampeni hizi hutolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na wadau wengine, na hupelekwa katika ngazi ya wilaya kwa ajili ya kuwalipa washiriki wote waliotekeleza zoezi hilo. Ndiyo maana tunashindwa kuelewa kwa nini baadhi ya watu walilipwa huku zaidi ya wahamasishaji 60 tukibaki bila stahiki zetu.

Tunaomba mamlaka husika, ikiwemo Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, kufanya uchunguzi wa suala hili na kuhakikisha wote tulioshiriki kampeni hiyo tunalipwa stahiki zetu. Tumefanya kazi tuliyopewa kwa uaminifu, hivyo tunaamini tuna haki ya kulipwa kama ilivyokuwa kwa wenzetu.
 
Poleni sana, usikute pesa zenu zipo kwenye mzunguko, mtalipwa tu.
 
Back
Top Bottom